Watulivu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Miguel de Molinos anahesabiwa kuwa mwanzilishi wa Utulivu.

Watulivu (kwa Kiingereza: Quietists) walikuwa Wakristo wa karne ya 17 walioshindana na viongozi wa Kanisa Katoliki kuhusu maisha ya Kiroho. Hatimaye mwaka 1687 maneno yao kadhaa yalilaaniwa na Papa Inosenti XI kama ya kizushi.

Mafundisho ya Watulivu[hariri | hariri chanzo]

Kadiri yao mtu anapaswa kunyamazisha vipawa vyake, kwa sababu kutaka kutenda ni chukizo kwa Mungu anayetaka kutenda peke yake ndani mwetu. Utendaji ni adui wa neema, nadhiri ya kutenda jambo ni kizuio cha ukamilifu, roho isipotenda inajiangamiza na kuirudia asili yake: hapo Mungu anatawala na kuishi ndani yake. Ndiyo njia ya Kiroho ambapo mtu hatendi kwa kumjua wala kumpenda Mungu, tena hafikirii uzima wa milele wala adhabu za motoni. Mtu hatakiwi kutamani ajue kama anampendeza Mungu au la, wala kufikiria matendo na makosa yake ili kujirekebisha; hatakiwi kutamani ukamilifu na wokovu wa milele, wala kumuomba Mungu neno maalumu; hahitaji kupambana na vishawishi, ila asivijali.

Kwa kufundisha hayo, M. Molinos alifuta kwa mkupuo mmoja juhudi zote na utekelezaji wa maadili ambayo ndiyo maandalizi halisi ya sala ya kumiminiwa na ya muungano na Mungu. Hivyo aliweza kupotosha maisha yote ya Kiroho.

Mafundisho ya Watulivu yanaweza kujumlishwa hivi: 1) Kuna njia moja tu, yaani sala ya kumiminiwa, ambayo tunaweza kujipatia kwa neema ya kawaida tukikoma kutenda lolote. Basi tuiingie mapema iwezekanavyo. 2) Tendo la sala ya kumiminiwa linaweza kudumu miaka, hata maisha yote, usingizini pia, bila kuchochewa. 3) Kwa kuwa sala ya kumiminiwa ni ya kudumu, inaturuhusu tuache kutekeleza maadili (k.mf. imani, tumaini, ibada na toba); hayo yanawafaa wanaoanza tu. 4) Kumfikiria Yesu na mafumbo yake ni kasoro; kuzama katika umungu tu ni kwa lazima, tena kunatosha. Anayetumia picha au mawazo hamuabudu Mungu katika Roho na ukweli. 5) Katika hali ya sala ya kumiminiwa tunatakiwa kutojali lolote, hata utakatifu na wokovu wetu, bali tupoteze tumaini ili upendo usiwe wa kujitafutia faida. 6) Tusisumbuke kupinga vishawishi: mawazo na matendo machafu ni majaribu yaliyowapata watakatifu pia; hayana lawama kwa sababu ni kazi ya shetani, hivyo hatutakiwi kuyaungama. Ndivyo tunavyofikia kujidharau na kuungana kwa ndani na Mungu.

Mafundisho ya Kikatoliki yanayopinga hayo kama uzushi ni kama ifuatavyo: 1) Kuna hali ya kutendewa ambapo Mungu mwenyewe anatenda ndani mwetu; lakini kwa kawaida tunaifikia baada tu ya kutekeleza muda mrefu maadili na tafakuri. 2) Kwa kawaida tendo la sala ya kumiminiwa linadumu muda mfupi, ingawa hali ya roho inayotokana nalo inaweza ikadumu siku kadhaa. 3) Sala ya kumiminiwa, inayoendana na tendo la kumpenda Mungu, inatimiliza maadili yote, lakini haituruhusu tuache kuyatekeleza nje ya sala. 4) Jambo kuu ambalo tuzame ndani yake ni Mungu mwenyewe, lakini Yesu ndiye la pili; nje ya tendo la sala ya kumiminiwa tusiache kumfikiria mshenga huyo wa lazima wala kumuendea Mungu tusimpitie. 5) Kujiachilia kitakatifu ni njia kamili, lakini bila kufikia hatua ya kutojali wokovu wa milele; kinyume chake tunapaswa kuutamani, kuutumaini na kuuomba. 6) Katika majaribu ya Kiroho ubunifu na hisi vinaweza vikavurugika, huku sehemu ya juu ya roho ikifurahia amani; lakini utashi unapaswa daima kupinga vishawishi (walau kwa kutovizingatia au kwa kupoteza lengo) usije ukavikubali.

Utulivuupande[hariri | hariri chanzo]

Baada ya Utulivu huo kukataliwa na Kanisa, wafuasi wake walipunguza ukali wa msimamo wao. Hata hivyo walihukumiwa tena kwa uzushi kuhusu upendo safi.

Kosa kuu la huo Utulivuupande lilikuwa kufundisha kwamba, katika hali ya sala kamili ya kumiminiwa, mtu anaingia aina ya maangamizi matimilifu, ambapo yuko mbele ya Mwenyezi Mungu akikubali matakwa yake matakatifu, asijali kuokoka wala kulaaniwa.

Hivyo wajibu wa tumaini la Kikristo ulipuuzwa, kwa kusahau kwamba kujinyima hamu ya wokovu ni sawa na kujinyima upendo wenyewe unaotuelekeza kumtukuza Mungu milele. Maagizo yake kuhusu tumaini na upendo hayapingani, bali yanaimarishana. Kwa njia ya tumaini tunatamani kumpata Mungu bila kumfanya chombo chetu; kwa njia ya upendo, unaohuisha tumaini usiliangamize, tunampenda Mungu kwa ajili yake, hivyo tunatamani wokovu wetu na wa wengine ili atukuzwe milele.

Makosa yao yanajumlishwa katika manne yafuatayo: 1) Katika maisha haya kuna hali ya kudumu ya upendo safi ambapo hapana tena hamu ya wokovu wa milele. 2) Katika majaribu ya mwisho ya maisha ya Kiroho mtu anaweza akawa na hakika isiyoshindikana ya kwamba anastahili kulaaniwa na Mungu, na kwa hakika hiyo akajinyima heri ya milele. 3) Katika hali ya upendo safi mtu hajali ukamilifu wake wala matendo ya maadili. 4) Wanasala hasa katika hali kadhaa wanapotewa na mtazamo maalumu wa kihisi na wa kimawazo kwa Yesu Kristo.

Kadiri ya Kanisa Katoliki ukweli ni kwamba: 1) Katika waliokamilika hamu ya heri inahuishwa mara nyingi na upendo, na kuna nafasi ambapo hawafikirii wazi wokovu wao. 2) Ikiwa mtakatifu fulani alihisi atalaaniwa, haikuwa hakika ya mawazo; tena ikiwa alijinyima wokovu wake, alifanya hivyo kwa sharti tu, si moja kwa moja. 3) Hata katika hali za juu za ukamilifu, watakatifu wanahimiza kushughulikia maendeleo ya roho na maadili muhimu zaidi. 4) Hata katika muungano unaotugeuza, watakatifu wengi walijaliwa kuuona ubinadamu wa Mwokozi, ila katika nafasi kadhaa mtu aliyezama ndani ya Mungu hamfikirii Yesu wazi.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Dandelion, P., A Sociological Analysis of the Theology of Quakers: The Silent Revolution New York, Ontario & Lampeter: Edwin Mellen Press, 1996.
  • Renoux, Christian, "Quietism", in The Papacy: An Encyclopedia, vol 3, edited by Philippe Levillain, 3 vols, (London: Routledge, 2002)
  • de Molinos, Miguel, The Spiritual Guide, ed and trans by Robert P. Baird, (New York: Paulist Press, 2010)
  • Bayley, Peter (1999). "What was Quietism Subversive of?". Seventeenth-Century French Studies 21 (1): 195–204. ISSN 0265-1068. doi:10.1179/c17.1999.21.1.195. 
  • Rulmu, Callia (2010). "Between Ambition and Quietism: the Socio-political Background of 1 Thessalonians 4,9-12". Biblica 91 (3): 393–417. JSTOR 42614996. 
  • Wainwright, Geoffrey (2009). "Revolution and Quietism: Two Political Attitudes in Theological Perspective". Scottish Journal of Theology 29 (6): 535–55. doi:10.1017/S0036930600000727. 
  • Tolles, Frederick B. (January 1945). "Quietism versus Enthusiasm: The Philadelphia Quakers and the Great Awakening". The Pennsylvania Magazine of History and Biography 69 (1): 26–49. JSTOR 20087728.  Check date values in: |date= (help)

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Watulivu kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.