Nenda kwa yaliyomo

Upendo safi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sehemu ya mfululizo wa makala kuhusu mapendo

Moyo katika mapokeo ya Ulaya
ni mchoro unaowakilisha mapendo.
Vipengele Msingi
Mapendo kadiri ya sayansi
Mapendo kadiri ya utamaduni
Upendo (fadhila)
Upendo safi
Kihistoria
Mapendo ya kiuchumba
Mapendo ya kidini
Aina za hisia
Mapendo ya kiashiki
Mapendo ya kitaamuli
Mapendo ya kifamilia
Mapendo ya kimahaba
Tazama pia
Mafungamano ya binadamu
Jinsia
Tendo la ndoa
Maradhi ya zinaa
Siku ya wapendanao

Upendo safi ni suala la teolojia ya Kikristo lililotolewa hasa baada ya Watulivu kukataliwa na Kanisa Katoliki, na baadhi yao kupunguza ukali wa msimamo wao. Hata hivyo walihukumiwa tena kwa uzushi.

Utulivuupande

[hariri | hariri chanzo]

Kosa kuu la huo Utulivuupande lilikuwa kufundisha kwamba, katika hali ya sala kamili ya kumiminiwa, mtu anaingia aina ya maangamizi matimilifu, ambapo yuko mbele ya Mwenyezi Mungu akikubali matakwa yake matakatifu, asijali kuokoka wala kulaaniwa.

Hivyo wajibu wa tumaini la Kikristo ulipuuzwa, kwa kusahau kwamba kujinyima hamu ya wokovu ni sawa na kujinyima upendo wenyewe unaotuelekeza kumtukuza Mungu milele. Maagizo yake kuhusu tumaini na upendo hayapingani, bali yanaimarishana. Kwa njia ya tumaini tunatamani kumpata Mungu bila kumfanya chombo chetu; kwa njia ya upendo, unaohuisha tumaini usiliangamize, tunampenda Mungu kwa ajili yake, hivyo tunatamani wokovu wetu na wa wengine ili atukuzwe milele.

Makosa yao yanajumlishwa katika manne yafuatayo: 1) Katika maisha haya kuna hali ya kudumu ya upendo safi ambapo hapana tena hamu ya wokovu wa milele. 2) Katika majaribu ya mwisho ya maisha ya Kiroho mtu anaweza akawa na hakika isiyoshindikana ya kwamba anastahili kulaaniwa na Mungu, na kwa hakika hiyo akajinyima heri ya milele. 3) Katika hali ya upendo safi mtu hajali ukamilifu wake wala matendo ya maadili. 4) Wanasala hasa katika hali kadhaa wanapotewa na mtazamo maalumu wa kihisi na wa kimawazo kwa Yesu Kristo.

Kadiri ya Kanisa Katoliki ukweli ni kwamba: 1) Katika waliokamilika hamu ya heri inahuishwa mara nyingi na upendo, na kuna nafasi ambapo hawafikirii wazi wokovu wao. 2) Ikiwa mtakatifu fulani alihisi atalaaniwa, haikuwa hakika ya mawazo; tena ikiwa alijinyima wokovu wake, alifanya hivyo kwa sharti tu, si moja kwa moja. 3) Hata katika hali za juu za ukamilifu, watakatifu wanahimiza kushughulikia maendeleo ya roho na maadili muhimu zaidi. 4) Hata katika muungano unaotugeuza, watakatifu wengi walijaliwa kuuona ubinadamu wa Mwokozi, ila katika nafasi kadhaa mtu aliyezama ndani ya Mungu hamfikirii Yesu wazi.

Katika karne ya 20

[hariri | hariri chanzo]
Dante na Beatrice wakikazia macho mbingu za juu; mchoro wa Gustave Doré kuhusu Divine Comedy, Paradiso, Canto XXXI.

Suala hilo lilifufuliwa na Anders Nygren kwa kupinganisha agape na eros, na kujadiliwa na Paul Tillich, Karl Rahner, Hans Urs von Balthasar, C.S. Lewis, Daniel Day Williams na wengine katika karne ya 20.

Mwanzoni mwa karne ya 21, Papa Benedikto XVI[1] alionyesha kwamba hata eros, yaani pendo la kijinsia, ina nafasi katika utekelezaji wa agape.

Upendo safi na umimi

[hariri | hariri chanzo]

Suala zima ni hili: je, upendo wetu kwa Mungu utaathiriwa na umimi daima? Je, upendo safi unawezekana? Ukiwezekana, unahusiana vipi na pendo la nafsi yetu lililo kiini cha maelekeo ya umbile letu? Aina za udanganyifu za kuepwa zinapingana; ukweli unainuka kama kilele kati na juu ya hizo.

Kadiri ya Thoma wa Akwino elekeo la umbile letu la kumpenda Mungu kama asili ya uhai wetu limepunguzwa na dhambi (ya asili na za binafsi), lakini linadumu ndani ya utashi wetu, na adili la upendo linaliinua upya tumpende Mungu kama asili ya neema kuliko tunavyojipenda. Kwa hiyo, tukipenda kiadilifu sehemu ya juu ya utu wetu, tunampenda zaidi Muumba wetu; kumbe tusipotaka ukamilifu wetu tunasogea mbali naye.

Katika matakaso ya Kimungu upendo kwa Mungu na kwa jirani unazidi kuwa safi mpaka upendo motomoto wa ari kwa utukufu wa Mungu na kwa wokovu wa watu ushinde kabisa umimi.

Utekelezaji wa upendo safi ni kujiachilia kwa maongozi ya Mungu kuhusu mambo yajayo: tendo hilo linatokana na imani, tumaini na upendo kwake ulio safi kila siku zaidi. Watulivu walidanganyika walipoondoa tumaini katika ukamilifu: kinachotakiwa tu ni kwamba liwe chini ya upendo na kuhuishwa nao, hatimaye liwe la kishujaa “kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa” (Rom 4:18). Walidanganyika pia walipoondoa katika ukamilifu juhudi za kutekeleza maadili na kushinda vishawishi. Hawakuzingatia kujiachilia kwa matakwa ya Mungu yasiyo wazi bado kunavyotakiwa kuendane na utekelezaji wa matakwa ya Mungu yaliyokwishadhihirishwa na amri, mashauri na matukio. Uaminifu wa kudumu kwa matakwa hayo yanayodhihirika nukta baada ya nukta, ndio unaotuwezesha kujiachilia kwa ukweli, tumaini na upendo kwa yale yajayo.

Tendo la upendo safi linaweza kutazamwa namna tatu: 1) kama tendo la pekee na la nadra; 2) kama tendo la kudumu; 3) kama tendo la kawaida analoliweza kila Mkristo.

1) Tendo la pekee na la nadra la upendo safi ni muungano wa dhati na wa juu na Mungu unaopatikana tu katika waliokwishatakata, ambao kwa uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu hawafikirii tena heri yao kwa namna wazi. 2) Utekelezaji wa mfululizo wa tendo hilo la upendo safi unawezekana mbinguni tu. 3) Tendo la kawaida la upendo safi wanaloliweza Wakristo wote ni lile la kumpenda Mungu kwa kumthamini kuliko yote na kuelekea kumpenda kwa dhati kuliko yote huko mbinguni.

  1. Barua "Deus caritas est".
  • Thomas Jay Oord: The Nature of Love: A Theology. Chalice Press, 2010. ISBN|978-0-8272-0828-5
  • Charles W Kegley, ed, The Philosophy and Theology of Anders Nygren, (Carbondale, IL: Southern Illinois University Press, 1970)
  • Drummond, Henry (1884). "The Greatest Thing in the World Ilihifadhiwa 26 Februari 2023 kwenye Wayback Machine.". Address first delivered in Northfield, England.
  • Hein, David. "Christianity and Honor." The Living Church, August 18, 2013, pp. 8–10.
  • Heinlein, Robert A. (1973). Time Enough for Love. New York: Ace Books. ISBN 0-7394-1944-7.
  • Kierkegaard, Søren (1998) [1847]. Works of Love. Princeton: Princeton University Press. ISBN 978-0-691-05916-7.
  • Oord, Thomas Jay (2010). The Nature of Love: A Theology. St. Louis, Mo.: Chalice Press. ISBN 978-0-8272-0828-5.
  • Outka, Gene H. (1972). Agape: An Ethical Analysis. Description & Contents. Yale University Press. ISBN|0-300-02122-4

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Upendo safi kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.