Katerina wa Genoa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Katerina wa Genoa (kwa Kiitalia Caterina Fieschi Adorno) aliishi Genova nchini Italia (5 Aprili 1447 - 15 Septemba 1510).

Anaheshimiwa na Kanisa Katoliki kama mtakatifu tangu tarehe 23 Aprili 1737, alipotangazwa na Papa Klementi XII; kabla ya hapo aliheshimiwa kama mwenye heri kuanzia tarehe 6 Aprili 1675.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 15 Septemba kila mwaka.

Anajulikana hasa kwa kitabu chake kuhusu Purgatorio, alichokiandika kutokana na mang'amuzi yake katika kuwaombea marehemu wa toharani.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Katerina alikuwa binti wa Giacomo Fieschi, sharifu wa Genova aliyewahi kuwa naibu mfalme wa Napoli na ndugu wa Papa Inosenti IV. Mama yake aliitwa Francesca di Negro.

Alilelewa kadiri ya masharti ya wakati ule kwa watu wa koo bora, akisoma fasihi za Kilatini, Kigiriki na Kiitalia, pamoja na vitabu vya dini ya Ukristo.

Tarehe 13 Januari 1463, aliolewa na sharifu Giuliano Adorno; lengo la ndoa lilikuwa kumaliza mgogoro kati ya koo zao kuhusu kutawala mji huo. Hivyo mwenendo wao haukuwa wa familia bora, wala hawakupata watoto.

Baada ya miaka 10 Katerina aliongoka kutokana na njozi aliyojaliwa tarehe 24 Machi 1473; baada yake hata mumewe aliongoka, hivyo maisha yao yalibadilika kabisa, wakaenda kuishi katika nyumba duni karibu na hospitali, walipohudumia wagonjwa. Hatimaye yeye akawa mkurugenzi wake, wakati mumewe alijiunga na Utawa wa Tatu wa Mt. Fransisko.

Kazi yake ikaleta uamsho mkubwa katika Kanisa Katoliki ulioenea kote nchini Italia.

Katerina aliendelea kujaliwa karama za pekee akaandika vitabu viwili juu ya maisha ya kiroho aliyokuwanayo, Dialogo spirituale na Trattato del Purgatorio.

Katika kuhudumia waliopatwa na tauni mwaka 1493 aliambukizwa lakini akapona.

Mafundisho[hariri | hariri chanzo]

Katerina alisisitiza umuhimu wa kupambana na umimi. Kwake Mungu ni wa kupendwa kwa ajili yake, si kwa kuogopa adhabu yake wala kwa kutamani tuzo lake. Lengo ni kufikia kumpenda hivyo kikamilifu tu. Ili atusaidie kufikia hatua hiyo, Mungu anaruhusu tupatwe na mateso hapa duniani na toharani.

Maandishi[hariri | hariri chanzo]

  • Trattato del Purgatorio su PagineCattoliche.it
  • Caterina da Genova (santa), Trattato del purgatorio e altri scritti, Curatore: Giuggia T., Gribaudi, 1996
  • Caterina Freschi Adorno, Dialoghi dell'anima e del corpo, Edizioni L'Arca Felice, Salerno 2008

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]