Kipindi cha Pasaka
Mwaka wa liturujia |
---|
Magharibi |
Mashariki |
Kipindi cha Pasaka ni kipindi maalumu cha mwaka wa Kanisa katika madhehebu mbalimbali ya Ukristo.
Ni kwamba Wayahudi wanaadhimisha Pasaka ya kale, ukumbusho wa kuvuka pakavu kati ya bahari, kutoka utumwani kuelekea uhuru. Kumbe Wakristo wanaadhimisha Pasaka mpya, ukumbusho wa sadaka ya Agano Jipya la milele ambayo pamoja na Yesu wanavuka toka dunia hii kwenda kwa Baba: Kristo asingefufuka imani hiyo ingekuwa bure.
Maelezo yafuatayo yanatokana na mpango wa Kanisa Katoliki, lakini kwa kiasi kikubwa yanafaa pia kwa madhehebu mengine, kama vile Anglikana.
Adhimisho
[hariri | hariri chanzo]Kile cha Pasaka, kikiwa na siku hamsini, ndicho kirefu zaidi kati ya vipindi vikuu vinne vya mwaka wa Kanisa (vingine vikiwa Majilio, Noeli na Kwaresima).
Wakati wa Pasaka Agano la Kale halisomwi kwa kuwa yaliyotabiriwa nalo yameshatimia katika Kristo. Badala yake yanasomwa karibu mfululizo Matendo ya Mitume yanayoelekeza safari yote ya Kanisa. Masomo mengine, sala na nyimbo vinasema hasa juu ya Kristo kufufuka na kuwa na watu wake kwa namna mpya, pia juu ya paji la Roho Mtakatifu alilowapatia.
Katika maisha ya kawaida watu wanafanya sherehe mbalimbali, si za dini tu. Sikukuu yoyote inatokeza furaha ya kuishi: usipokuwa na mtazamo wa kuridhika na maisha, kumwaga pesa katika anasa hakuondoi huzuni ya kukata tamaa. Sikukuu yoyote ni adhimisho la pamoja: inatokana na watu kukubaliana katika kujali mambo fulanifulani au walau kuheshimiana; pia inajenga jamii kwa kurudisha furaha ya kuwa pamoja.
Kwa Wakristo sherehe kuu kuliko zote ni Pasaka: ndiyo sikukuu yenyewe ambayo inadumu siku hamsini mfululizo hadi Pentekoste na inaitwa Dominika kubwa. Kwa kweli Pasaka si sherehe mojawapo tu wala kipindi kimojawapo tu katika mwaka wa liturujia, bali ndiyo kiini chake, kama vile Dominika (Pasaka ndogo ya kila wiki) ilivyo kiini cha juma zima. Ni adhimisho la uzima mpya na wa milele ambao Kristo mfufuka anaushirikisha kwa njia ya sakramenti: ubatizo na kipaimara kwa Wakristo wachanga, kitubio kwa waliobatizwa zamani, hasa ekaristi kwa wote; humo Yesu hakumbukwi tu, bali waaminu wanakutana naye, hai tena mtukufu. Adhimisho hilo ni la pamoja kwa sababu wamekuwa moyo mmoja na roho moja katika Kristo kwa kumiminiwa Roho Mtakatifu. Kwa kumega mkate mmoja wanaimarisha ushirika wao na kuwajibika kumtambua Yesu katika wale wote wanaokutana nao, hasa maskini.
Mang’amuzi hayo ya imani yanachochea kuimba mfululizo Aleluya! Bila shaka inaimbwa na watu wakiwa njiani kuelekea kwao: hawajafikia pale watakapoimba katika heri ya starehe ya milele. Wanaimba wasije wakalemewa na mzigo wa maisha. Augustino wa Hippo alionya: “Imba anavyofanya msafiri. Imba lakini tembea, usahau uchovu wako kwa kuimba, lakini jihadhari na uvivu. Imba na tembea”. Aleluya inatokeza vizuri furaha na tumaini: ndiyo sababu ikaririwa sana. Pamoja na hayo, uhuru wa Kikristo unawadai waamini wAUshuhudie kwa matendo na hasa kwa kuwakomboa ndugu zao wanaodhulumiwa.
Kristo amefufuka kweli na atawafufua wote pia: waamini wake wataishi naye kwa Baba katika umoja wa Roho Mtakatifu. Hata sasa yu pamoja nao (ndiyo maana ya mshumaa wa Pasaka). Wakiwa naye maisha yanawanogea, kwa kuwa yote yameinuliwa tena na kufanywa mapya. Wanaamini wamekombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mauti, wamekuwa wana wa Mungu na kuishi kwa uhuru wa upendo wakiongozwa na Roho Mtakatifu. Kristo amekuwa Bwana na anaendelea kueneza ufalme wake. Hawawezi kuogopa chochote tena kwa kuwa historia ni yake yeye aliye Alfa na Omega.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Easter Season Resource Library - Crossroads Initiative Ilihifadhiwa 11 Oktoba 2012 kwenye Wayback Machine.
- Normae Universales de Anno Liturgico et de Calendario
- French translation
- Writings on Easter, Eastertide and Lent liturgical days
- Liturgy of Hours of Eastertide Ilihifadhiwa 11 Julai 2011 kwenye Wayback Machine.
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kipindi cha Pasaka kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |