Krismasi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Uchoraji wa Kiorthodoksi unaoonyesha kuzaliwa kwake Kristo. Yesu anaonekana amevikwa sanda na kulazwa kaburini, kwa maana alizaliwa ili awakomboe watu kwa kifo chake.

Krismasi (pia Noeli) ni sikukuu ambayo Wakristo wengi husheherekea kuzaliwa kwake Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita.

Kwa kawaida husheherekewa tarehe 25 Desemba katika Ukristo wa magharibi na tarehe 6 Januari katika ule wa mashariki.

Jina[hariri | hariri chanzo]

Kuna majina mawili yaliyo kawaida kwa Kiswahili kwa ajili ya sikukuu hii.

  • Noeli inatokana na neno la Kiingereza "Noel" (au "Nowell") ambalo limepokewa kutoka lugha ya Kifaransa "Noël". Hilo ni ufupisho wa neno la Kilatini "Natalis (dies)", "(siku ya) kuzaliwa".

Historia ya Krismasi[hariri | hariri chanzo]

Tarehe halisi ya kuzaliwa kwake Yesu haijulikani kwa sababu utamaduni wa Wayahudi wa wakati ule haukuwa na sherehe au kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa.

Lakini baadaye Ukristo ulienea katika Dola la Roma kati ya mataifa yaliyokuwa na kawaida ya kuzingatia siku ya kuzaliwa. Hivyo ilijitokeza hamu ya kusheherekea pia sikukuu ya kuzaliwa kwake Kristo. Ndiyo asili ya sikukuu ya Krismasi.

Tangu mwanzo wa karne ya 3 BK kuna kumbukumbu ya waandishi mbalimbali waliojadili tarehe ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo.

Habari za kwanza kabisa za makadirio ya tarehe ya kuzaliwa kwake Yesu zinapatikana kutoka Misri mnamo mwaka 200. Mwandishi Mkristo Klemens wa Alexandria [1] alilalamikia udadisi wa wataalamu kadhaa wa Misri waliodai kwamba wamekadiria tarehe hiyo katika mwezi Mei, wengine katika Aprili. Alisema pia kuwa kikundi cha Kikristo cha wafuasi wa Basilides huko Misri walisheherekea Epifania pamoja na kuzaliwa kwake Yesu tarehe 6 Januari.

Labda kadirio la tarehe ya 25 Desemba pia lina asili katika Misri. Kuanzia mwaka 200 (kwa mara ya kwanza katika maandishi ya Sixtus Julius Africanus) tunasikia kwamba wataalamu wa Misri walifikiri tarehe 25 Machi ilikuwa tarehe ya kufa kwake Kristo na pia siku ya utungaji mimba wake. Kwa kuongeza miezi tisa ya mimba inajitokeza 25 Desemba kama tarehe ya kuzaliwa.

Mwaka wa liturujia
Magharibi
Mashariki

Inaonekana tarehe 25 Desemba ilijitokeza wakati huo. Kuna taarifa ya mwaka 204 kutoka Ipolito wa Roma kwamba tarehe 25 Desemba ilikuwa sikukuu ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo.

Krismasi na sikukuu ya Sol Invictus[hariri | hariri chanzo]

Wataalamu mbalimbali walidai kwamba Kanisa lilipachika sikukuu ya Kristo kwenye tarehe hiyo kwa nia ya kufanya ichukue nafasi ya sikukuu ya jua kama mungu "Sol invictus" (yaani "Jua lisiloshindika").

Lakini pengine mambo yalikwenda kinyume, yaani kwamba Makaisari walianzisha sikukuu hiyo, halafu wakaipanga tarehe ya Krismasi ili kushindana na Ukristo uliokuwa bado chini ya dhuluma ya serikali yao lakini ulikuwa unazidi kuenea.

Aliyeingiza sikukuu ya "Kuzaliwa Jua" (Mitra) huko Roma ni Eliogabalus (kaisari kuanzia 218 hadi 222). Baadaye kaisari Aurelianus akaithibitisha rasmi mwaka 273, hatimaye ikahamishiwa tarehe 25 Desemba.

Wakati wa kaisari Licinius (308-324) sikukuu hiyo ilikuwa ikiadhimishwa bado tarehe 19 Desemba. [2].

Kutoka Roma, uliokuwa mji mkuu wa Dola la Roma, sherehe ya 25 Desemba ilienea kote katika Ukristo.

Wakristo wengi husheherekea tarehe 25 Desemba (Wakatoliki na sehemu ya Waprotestanti na Waorthodoksi). Kati ya Waorthodoksi kuna tarehe nyingine, hasa 6 Januari kutokana na tofauti katika kalenda.

Habari za Krismasi katika Biblia[hariri | hariri chanzo]

Habari za Krismasi kama sherehe hazipatikani katika Biblia kwa sababu zilizotajwa hapa juu na kwa sababu mwanzoni mwa Kanisa mkazo ulikuwa juu ya kifo na ufufuko wa Yesu, tunavyoona hasa katika barua za Mtume Paulo.

Baadaye tu, Wakristo walichunguza zaidi asili ya huyo aliyesadikiwa nao kuwa alikufa na kufufuka.

Hasa vitabu viwili vya Agano Jipya vina habari za kuzaliwa kwake Yesu, yaani Injili za Mathayo na Luka.

Katika Injili ya Mathayo[hariri | hariri chanzo]

Mathayo anasimulia habari hizo katika mlango wa kwanza kuanzia aya 18 na katika mlango wa pili.

Bikira Maria, Mama wa Yesu, alipata mimba wakati alipokuwa mchumba wa Yosefu. Yosefu alitaka kumwacha lakini aliambiwa na malaika aanze kuishi naye na kumkubali mtoto kama wake kwa kumpa jina "Yesu".

Mamajusi kutoka mashariki waliwatembelea kijijini Bethlehemu na kuwaletea zawadi kwa sababu waliona nyota ya pekee iliyokuwa kwao alama ya kuzaliwa kwa mfalme mpya katika Uyahudi ikawaongoza hadi mjini Yerusalemu. Lakini walipompitia mfalme Herode Mkuu, huyo alikasirika akimwogopa mfalme mpya. Hata hivyo aliwaelekeza Bethlehemu kadiri ya utabiri wa nabii Mika.

Yosefu alipata tena ujumbe kutoka kwa malaika akaondoka na mtoto na Maria kukimbilia Misri kabla ya askari wa Herode hawajaweza kumuua Yesu.

Baada ya kifo cha Herode walirudi kutoka Misri lakini hawakuenda tena Bethlehemu bali walihamia Nazareti katika mkoa wa Galilaya.

Katika Injili ya Luka[hariri | hariri chanzo]

Katika taarifa ya Luka (mlango wa 1 na 2) Maria alipokea huko Nazareti ujumbe wa malaika mkuu Gabrieli kwamba atapata mimba halafu mtoto wa pekee.

Yosefu na Maria walikwenda Bethlehemu kwa sababu ya sensa iliyowataka kwenda katika mji asili wa ukoo wa Yosefu, mjukuu wa mfalme Daudi. Hapo Yesu alizaliwa katika hori la kulishia wanyama; wachungaji mabondeni walitangaziwa na malaika habari hiyo wakaja kumwona mtoto.

Baada ya kuzaliwa wazazi walimpeleka Yesu Yerusalemu katika hekalu kufuatana na sheria ya Agano la Kale (Kitabu cha Kutoka 13,2; 13,15) halafu wakarudi kwao Nazareti.

Habari za Krismasi katika Korani[hariri | hariri chanzo]

Korani pia ina habari za kuzaliwa kwake Yesu (nabii Isa).

Sura ya tatu (Al Imran, 42-47) ina habari za tangazo la malaika kwa Bikira Mariamu zinazofanana na Luka 1.

Sura ya 19 (Mariamu, 16-34) inarudia tangazo la malaika kwa Mariamu na inasimulia kuzaliwa kwake Yesu chini ya mti wa mtende, halafu majadiliano kati ya Mariamu na ndugu zake. Mtoto mchanga Yesu akaanza kusema wakati wa kuzaliwa akimtetea mama yake dhidi ya ndugu zake.

Krismasi katika liturujia[hariri | hariri chanzo]

Kama kawaida, imani na liturujia ya Kikristo zinaitikia haja za binadamu.

Mojawapo ni kukutana na watu wa kupendeza kwa wema wao.

Kipindi cha Noeli kinatimiza haja hiyo, kwa kuwa kinaadhimisha kuzaliwa kwa mtu mpya kabisa ambaye anatuvutia kwa wema wake na ambaye tukimuona tumemuona Mungu, tena tukimpokea tunazaliwa upya kama wana wa Mungu.

“Leo amezaliwa kwa ajili yenu Mwokozi, ndiye Kristo Bwana”. Tunapoadhimisha Noeli tangazo hilo la malaika kwa wachungaji linatufikia sisi. Si kujidanganya, kana kwamba Yesu angezaliwa leo, wala hatukumbuki tu tukio la zamani, bali fumbo la kuzaliwa Bwana linatufikia leo katika liturujia na kutuletea neema zake. Hivyo tunaweza tukazaliwa upya kwa kushiriki kuzaliwa kwa kichwa chetu.

Liturujia inashangilia hivi, “Lo! Mabadilishano ya ajabu! Mwana wa Mungu anakuwa mtu kusudi mtu awe mwana wa Mungu!”. Tena si binadamu tu, bali viumbe vyote vinapata heshima mpya kwa Neno wa milele kujifanya kiumbe.

Desturi za Krismasi[hariri | hariri chanzo]

Sherehe ya Krismasi imekuwa sikukuu muhimu sana katika tamaduni za mataifa yaliyoathiriwa na Ukristo. Kuna desturi nyingi zilizojitokeza katika karne zote za kusheherekea Krismasi. Sehemu ya desturi hizi zimeenea pia nje ya nchi za asili na hata kutumiwa na watu wasiofuata imani ya Kikristo.

  • Mti wa Krismasi - ni ishara ya pekee ya Krismasi yenye asili katika Ujerumani kusini-magharibi ya karne ya 16 hivi. Asili yake iko katika maigizo yaliyosimulia hadithi za Biblia na mti wa Paradiso unaohusiana na masimulizi ya dhambi la kwanza na ujumbe wa Kristo kama mwokozi anayekuja kuondoa dhambi hilo. Kutoka maigizo ya kanisani ishara ya mti uliopambwa matunda uliingia katika nyumba za Wakristo ambako ulipambwa zaidi kwa matunda, keki tamu na pipi kwa watoto. Umekuwa mapambo ya nyumbani kwa majira ya Krismasi. Tangu Krismasi kuwa nafasi muhimu kwa uchumi kuna pia maduka mengi yanayoweka miti hii na katika mazingira ya kibiashara uhusiano wake na mti wa Paradiso umesahauliwa mara nyingi.
  • Zawadi za Krismasi - Martin Luther alitaka kuongeza umuhimu wa Krismasi kwa Wakristo ambao wakati wake walikuwa na desturi ya kuwazawadia watoto kwenye siku ya Mtakatifu Nikolasi tarehe 6 Desemba, wiki 2 kabla ya sikukuu. Hapo Luther alipendekeza kuhamisha zawadi kwa watoto kwenda siku ya kuzaliwa kwake Yesu ili wamkumbuke zaidi Yesu kuliko mtakatifu huyo. Hapo alirejea zawadi zilizopelekwa kwa Yesu na mamajusi kutoka mashariki kufuatana na taarifa ya Injili ya Mathayo mlango 2. Desturi ya kuwazawadia watoto kwenye sikukuu hii ilienea hadi kuwa desturi ya kupeana zawadi kati ya watu wa kila umri. Katika karne ya 20 desturi ilienea kiasi cha kuwa nafasi muhimu ya biashara. Katika nchi nyingi mwezi wa Desemba umekuwa mwezi wa mapato makubwa kushinda miezi mingine. Hata katika miji mikubwa ya nchi kama Dubai au Japani ambako Wakristo ni wachache desturi ya kupeana zawadi imeenea na mapambo ya Krismasi katika maduka yanataka kuwahamasisha wateja kununua zawadi za majira.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. (kitabu cha Stromateis I, xxi)
  2. Taz. maandishi yaliyotajwa na Allan S. Hoey katika ukurasa 480 (rejeo 128) wa Official Policy towards Oriental Cults in the Roman Army, Transactions and Proceedings of the American Philological Association (70) 1939, pp 456-481)

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]