Mariolojia ya Kikatoliki
Mariolojia ya Kikatoliki inategemea Biblia ya Kikristo pamoja na Mapokeo ya Mitume yanayojitokeza hasa katika maandishi ya Mababu wa Kanisa wa Mashariki na wa Magharibi. Hayo yote yaliongoza Mapapa na maaskofu wenzao wa Kanisa Katoliki kutangaza hasa dogma nne kuhusu Bikira Maria.
Mafundisho makuu hayo ni lazima kila Mkatoliki ayasadiki kutokana na ufunuo wa Mungu:
- B. Maria mkingiwa dhambi ya asili
- B. Maria Mama wa Mungu
- B. Maria Bikira daima
- B. Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho
Mkingiwa Dhambi ya Asili
[hariri | hariri chanzo]Malaika Gabrieli alimsalimia Maria “umejaa neema” (Lk 1:28) maana ndiye tunda bora la ukombozi ulioletwa na Yesu. Ni imani ya Wakatoliki kwamba kwa stahili za Mwanae alikingiwa asirithi kwa wazazi dhambi ya asili na madonda yanayotokana nayo, wala asitende dhambi maisha yake yote. Kwa maneno mengine, Bikira Maria tangu atungwe mimba Mungu alimkinga na kila doa la dhambi kwa kutazamia stahili za Yesu Kristo aliye Mkombozi wa binadamu wote. Maria ndiye aliyekombolewa kwa namna bora kushinda viungo vyote vya Kanisa. Maisha yake yote hakutenda dhambi hata moja. Mapokeo ya mashariki yanamuita “A Panagia” = “Mtakatifu tu”. Dogma hiyo ilitangazwa na papa Pius IX mwaka 1854, halafu mwaka 1858 Bikira Maria alijitambulisha kama Mkingiwa kwa Bernadeta Soubirous huko Lurdi (Ufaransa) kadiri ya njozi zilizokubaliwa na Kanisa hilo. Tena waumini wake wanaelekezwa kuamini kwamba mwaka 1917 huko Fatima (Ureno) aliwafunulia Lusia, Fransisko na Yasinta Marto moyo wake safi usio na doa.
Mama wa Mungu
[hariri | hariri chanzo]Injili ya Yohane inaanza kwa kishindo, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu” (Yoh 1:1). Huyo Mungu Mwana alitwaa ubinadamu katika Bikira Maria akazaliwa mtoto, jina lake Yesu, maana yake Mungu Mwokozi. Huyo ni binadamu kama sisi katika yote isipokuwa dhambi. Ubinadamu wa Yesu unategemea Nafsi yake ya Kimungu: akisema, ‘Mimi’, ni kwa Nafsi yake hiyo. Ndiyo maana aliwaambia Wayahudi, “Kweli nawaambia, kabla Abrahamu hajazaliwa, nalikuwepo” (Yoh 8:50). “Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo alivyomjalia Mwanae kuwa asili ya uhai” (Yoh 5:26).
Mtume Paulo akaeleza, “Wakati maalumu ulipotimia Mungu alimtuma Mwanae aliyezaliwa na mwanamke” (Gal 4:4). Bikira Maria ni Mama wa Mungu kwanzia wakati huo: tangu Bikira Maria alipojaliwa kumchukua mimba, kumzaa, kumnyonyesha na kumlea mtu ambaye kwa asili ni Mungu. Cheo hicho kimemuinua juu kuliko hata malaika. “Malaika alimwambia, ‘Hicho kitakachozaliwa kitaitwa Kitakatifu, Mwana wa Mungu’” (Lk 1:35).
Dogma hiyo ilitangazwa mwaka 431 kwenye Mtaguso wa Efeso uliomuita “Mzazi wa Mungu”, ukisema Maria anastahili kuitwa hivyo kwa sababu Mwana wa milele wa Mungu, ambaye ni Mungu sawa na Baba, alifanyika mtu toka kwake. Akiwa mja mzito alishangiliwa: “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?” (Lk 1:42-43). Ungamo hilo la Elizabeti likakamilishwa na Mtume Thoma aliyemuambia Yesu mfufuka: “Bwana wangu na Mungu wangu!” (Yoh 20:28).
Bikira na Mama
[hariri | hariri chanzo]Wakristo na Waislamu wote wanakiri kuwa Yesu alitungwa bila ya mchango wa mwanamume. La ajabu zaidi katika imani hiyo ni kwamba hata uzazi wenyewe haukuondoa ubikira wa Maria, bali uliutakasa: ni Bikira daima. Ingawa akili inasita, ni lazima kukiri na malaika, “Hakuna lisilowezekana kwa Mungu” (Lk 1:38). Yosefu, ingawa kisheria alikuwa mume wake, hakutenda naye tendo la ndoa.
Ni imani ya Wakatoliki na Waorthodoksi kuwa Mama wa Yesu anastahili kuitwa “Bikira daima” kwa sababu alimchukua mimba akiwa bikira, akamzaa bila ya kupotewa na ubikira, akabaki bikira hadi mwisho wa maisha yake. Hamu yake ya kuwa bikira hata kisha kuchumbiwa inajitokeza katika jibu alilompa malaika aliyemtabiria mimba: “Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?” (Lk 1:35). Ni kielelezo cha Wakristo ambao Mtume Paulo aliwaandikia: “Nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi” (2Kor 11:2), “mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine” (1Kor 7:35).
Wanaosemwa katika Injili “ndugu zake Yesu” si watoto wa Bikira Maria, bali ndugu wa ukoo waliokuwa jirani sana na familia hiyo takatifu. Kama Bikira Maria angekuwa na watoto wengine, Yesu angekuwa amefanya kosa la kuwanyang’anya Mama yao na kumfanya awe Mama wa mtume Yohane alipomkabidhi msalabani, “‘Mwana, tazama Mama yako’. Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake” (Yoh 19:27).
Katika Agano Jipya yupo Yakobo anayeitwa na mtume Paulo “ndugu yake Bwana” (Gal 1:19): Yakobo huyo alikuwa maarufu katika Kanisa la Yerusalemu (Mdo 12:7; 15:13-21; 21:18-20; Gal 2:9). Yakobo huyo si mtume Yakobo kaka yake Yohane (Lk 6:12-16), bali ni Yakobo ndugu yake Yose na mama yao kwenye Injili anaitwa “Maria mwingine”, si Maria Mama wa Yesu. “Walikuwepo pia wanawake waliotazama kwa mbali. Miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome na Maria mama wa akina Yakobo mdogo na Yose” (Mk 15:40). Maria lilikuwa jina la kawaida kwa Wayahudi: akina Maria wakiwa wengi hivyo, tujue kuwatofautisha kwenye Injili, ambazo zinamtaja Bikira Maria kama “Mama wa Yesu”.
Kupalizwa Mbinguni mwili na roho
[hariri | hariri chanzo]Baada ya maisha haya ya duniani Bikira Maria alipalizwa mbinguni mwili na roho, ishara ya mwanamke mshindi. “Ishara kubwa ikaonekana mbinguni, ambapo mwanamke aliyevikwa jua, pia na mwezi chini ya miguu yake, na taji la nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake” (Ufu 12:1). Maneno ya shangilio lake yametimia: Mungu “amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; na wanyonge amewakweza” (Lk 1:52).
Imani hiyo ya mapokeo ya kale, yanavyoshuhudiwa na Mababu wa Kanisa, ilitangazwa rasmi na Papa Pius XII kwa niaba ya maaskofu wote mwaka 1950.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Benedict XVI; Walker, Adrian; Von Balthasar, Hans Urs (Oktoba 1, 2005). Mary: The Church at the Source. ISBN 1-58617-018-X.
{{cite book}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - Hauke, Manfred (2008). "The Mother of God". Mariology: A Guide for Priests, Deacons, Seminarians, and Consecrated Persons. Queenship Publishing. ISBN 978-1-57918-355-4.
- Louis de Montfort True Devotion to Mary ISBN 1-59330-470-6, also available as online text [1]
- Luigi Gambero, 1999, Mary and the Fathers of the Church, Ignatius Press ISBN|0-89870-686-6
- Michael Schmaus, Mariologie, Katholische Dogmatik, München Vol V, 1955
- K Algermissen, Boes, Egelhard, Feckes, Michael Schmaus, Lexikon der Marienkunde, Verlag Friedrich Pustet, Regensburg, 1967
- Remigius Bäumer, Leo Scheffczyk (Hrsg.) Marienlexikon Gesamtausgabe, Institutum Marianum Regensburg, 1994, ISBN|3-88096-891-8 (cit. Bäumer)
- Stefano De Fiores, (Marianum) Maria, sintesi di valori. Storia culturale di mariologia. Cinisello Balsamo 2005;
- Stefano de Fiores, (Marianum), Maria. Nuovissimo dizionario. 2 Vols. Bologna 2006;
- Mariology Society of America [2]
- Acta Apostolicae Sedis, referenced as AAS by year.
- Pope Pius IX, Apostolic Constitution
- Pope Pius XII:Apostolic Constitution Munificentissimus Deus on the Vatican Website
- Pope John Paul II, apostolic letters and addresses
Marejeo mengine
[hariri | hariri chanzo]- Burke, Raymond L.; na wenz. (2008). Mariology: A Guide for Priests, Deacons, Seminarians, and Consecrated Persons. Goleta, California: Queenship Pub. Co. ISBN 978-1-57918-355-4. OCLC 225875371.
- Haffner, Paul (2004). The Mystery of Mary. Hillenbrand Books studies series. Leominster, Herefordshire: Gracewing Press. ISBN 0-85244-650-0. OCLC 58964281.
- Miravalle, Mark I. (1993). Introduction to Mary: The Heart of Marian Doctrine and Devotion. Santa Barbara, California: Queenship Pub. Co. ISBN 978-1-882972-06-7. OCLC 28849399.
- Pohle, Joseph (1948) [1914]. Preuss, Arthur (mhr.). Mariology; A Dogmatic Treatise on the Blessed Virgin Mary, Mother of God. St. Louis, Mo: Herder Book. OCLC 1453529.
- Schroedel, Jenny; Schroedel, John (2006). The Everything Mary Book. Everything profiles series. Avon, Mass: Adams Media. ISBN 1-59337-713-4. OCLC 70167611.