Nenda kwa yaliyomo

Maria Mshenga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sanamu ya mwaka 1948.

Maria Mshenga ni jina la heshima linalotolewa na Kanisa Katoliki kwa Bikira Maria, mama wa Yesu Kristo[1][2][3] .

Kadiri ya imani hiyo hatuwezi kuzungumzia kazi ya Kristo kwa mwili wake wa fumbo tusidokeze juu ya msaada wa mama Maria. Wakristo kadhaa hawaoni haja ya kumkimbilia Maria ili kuungana na Mwokozi kwa undani zaidi. Kuhusu hilo, Alois Maria wa Montfort aliwasema “walimu ambao wanamjua Mama wa Mungu kinadharia tu, kwa namna kavu, tasa na baridi, na wanaogopa heshima kwa Bikira mtakatifu itatumika vibaya hivi kwamba, kwa kumheshimu mno Mama mtakatifu, Bwana atachukizwa. Wakiongelea heshima kwa Maria ni kwa kuzuia namna zake zisizofaa kuliko kwa kuihimiza”; unaweza kudhani wanamuona ni kizuio kwa kufikia muungano na Mungu! Kumbe muungano huo unasaidiwa na heshima halisi na kubwa kwa Maria. Ni kiburi kutowajali wasaidizi tuliojaliwa kwa udhaifu wetu.

Ufafanuzi wa ushenga[hariri | hariri chanzo]

Thoma wa Akwino aliandika, “Kazi ya mshenga ni kuwasogeza karibu na kuwaunganisha wale ambao amewekwa katikati yao: kwa kuwa pande mbili zinaungana kwa njia ya mshenga. Basi, kuunganisha watu na Mungu ni kazi hasa ya Kristo, kwa kuwa ndiye aliyewapatanisha na Mungu alivyosema Mt. Paulo: ‘Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake’ (2Kor 5:19). Kwa hiyo mshenga kamili kati ya Mungu na watu ni Kristo tu, kwa kuwa kwa kifo chake amewapatanisha watu na Mungu. Hata Mt. Paulo aliposema: ‘mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, mwanadamu Kristo Yesu’ akaongeza, ‘ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote’ (1Tim 2:5-6). Lakini hakuna kinachozuia wengine wasiitwe kwa namna fulani washenga kati ya Mungu na watu kwa kuwa wanachangia muungano wa Mungu na watu kwa kuhudumia ugawaji”. Kwa maana hiyo manabii na makuhani wa Agano la Kale wanaweza kuitwa washenga; kama vile mapadri wa Agano Jipya, walio wahudumu wa mshenga halisi. Mwalimu huyo akaongeza kuwa “ni kwa utu wake kwamba Kristo ni mshenga: kwa sababu ni kama binadamu kuwa yupo kati ya pande mbili: chini ya Mungu kwa umbile, juu ya watu kwa ukuu wa neema na utukufu. Tena kama binadamu anawaunganisha watu na Mungu akiwatolea amri na zawadi za Mungu, na kutoa fidia na sala kwa ajili yao”. Yesu alifidia na kustahili kama binadamu, ambaye fidia na stahili zake zilikuwa na thamani isiyo na mipaka kutokana na Nafsi yake ya Kimungu. Hapo tuna ushenga wa aina mbili, wa kushuka na wa kupanda, yaani wa kuwapa watu mwanga na neema ya Mungu na wa kumtolea Mungu ibada na malipizi anayostahili kwa ajili ya watu. Chini ya Kristo, hakuna kinachozuia uwepo wa washenga washiriki. Maria hakuteuliwa awe mhudumu, bali mshiriki wa pekee na wa dhati wa ukombozi wa wanadamu, “kadiri ya maneno, ‘nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye’ (Mwa 2:18)” (Alberto Mkuu).

Wanateolojia wengine wanafikia hatua ya kufundishwa kwamba kama Mama wa Mungu alikusudiwa kuwa mshenga kwa wote na yote kati ya Mungu na watu Papa Benedikto XVI aliruhusu majimbo ya Ubelgiji kuadhimisha kila mwaka sikukuu ya Maria, Mshenga wa neema zote tarehe 31 Mei.[4][5][6]. Akiwa kiumbe yuko chini sana kuliko Mungu na Kristo; lakini ameinuliwa juu ya watu wote kwa kufanywa Mama wa Mungu, na kwa ukamilifu wa neema ambao alijaliwa tangu achukuliwe mimba hali amekingiwa dhambi asili, ukaongezeka moja kwa moja hadi kifo chake. Naye hakuteuliwa tu awe mshenga kutokana na umama wake wa Kimungu, bali kweli alikabidhiwa na kutekeleza kazi hiyo inayomfaa kwa sababu: 1° alichangia sadaka ya msalabani kwa malipizi na stahili zake; 2° haachi kutuombea, kutupatia na kutugawia neema zote tunazopokea. Ndio ushenga wa kupanda na kushuka tunaopaswa kuuzingatia ili kuufaidi kila siku zaidi.

Maria mshenga kwa kuchangia sadaka ya msalabani[hariri | hariri chanzo]

Maisha yake yote bikira Maria alichangia sadaka ya Mwanae hadi aliposema, “Imekwisha” (Yoh 19:30). Kwanza ili fumbo la umwilisho lifanyike ilihitajika ridhaa yake, aliyoitoa alipopashwa habari na malaika, kana kwamba Mungu alisubiri kibali cha binadamu kwa sauti ya Maria. Hapo alichangia sadaka ya msalabani kwa kutupatia kuhani na kafara yake.

Aliichangia pia kwa kumleta hekaluni Mwanae, ambaye mzee Simeoni kwa mwanga wa kinabii alimuona ndiye wokovu ulioletwa na Mungu “tayari machoni pa watu wote; nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, na kuwa utukufu wa watu wako Israeli” (Lk 2:31-32). Maria akiwa ameangaziwa kuliko yeye, alimtoa Mwanae na kuanza kuteseka pamoja naye, akitabiriwa kwamba mtoto amewekwa “kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako” (Lk 2:34-35).

Hasa chini ya msalaba Maria alichangia sadaka ya Kristo, akiungana naye kwa undani usioelezeka. Baadhi ya watakatifu, hasa waliotiwa madonda ya Mwokozi, waliungana na mateso na stahili zake kwa namna ya pekee, lakini kidogo kuliko Maria aliyemtoa Mwanae kama mwenyewe alivyojitoa. Yesu angeweza kuzuia kwa urahisi ukatili wa watesi wake usimuue, lakini alitoa kwa hiari uzima wake: “Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena” (Yoh 10:18). Alijinyima haki ya kuishi, akijitoa mhanga kwa wokovu wetu. Maria alisimama “penye msalaba wake Yesu” (Yoh 19:25), akiungana naye kwa dhati katika kuteseka na kujitoa, “akijinyima haki zake za kimama kuhusu Mwanae kwa wokovu wa watu wote” (Papa Benedikto XV). Alikubali kifodini cha Kristo na kukitoa kwa ajili yetu. Upendo wa Bikira ulipita ule wa watakatifu wote. Hivyo alionja kuliko wote uchungu wa Mwanae katika mwili na katika roho; alisikitishwa na dhambi kadiri ya upendo wake: kwa Mungu, anayechukizwa nayo; kwa Mwanae, aliyesulubiwa nayo; kwa watu wanaoangamizwa nayo.

Alichangia sadaka ya msalabani kama malipizi kwa kumtolea Mungu kwa niaba yetu, kwa uchungu mwingi na upendo mkuu, uhai wa Mwanae mpenzi, aliyemuabudu na kumpenda kuliko alivyojipenda. Saa hiyo Mwokozi alitulipia kwa msingi wa haki, kwa matendo yake ya kibinadamu yaliyoshiriki thamani isiyo na mipaka ya nafsi yake ya Kimungu, yenye uwezo wa kufidia dhambi zote na zaidi tena. Upendo wake ulimpendeza Mungu kuliko anavyochukizwa na dhambi zote. Ndio kiini cha fumbo la ukombozi. Maria, akiungana na Mwanae, alitulipia kwa msingi si wa haki yenyewe, bali wa urafiki wa ndani uliomuunganisha na Mungu. Mwanae alipokuwa akifa msalabani kama mtu aliyeshindwa na kutupwa, Maria hakuacha hata kidogo kumuamini. Ndilo tendo kuu la imani; ndilo pia tendo kuu la upendo baada ya lile la Kristo mwenyewe. Tendo hilo limemfanya Maria malkia wa mashahidi, kwa kuwa si tu shahidi kwa ajili ya Kristo, bali pamoja naye, hivi kwamba msalaba mmoja uliwatosha Mwana na Mama aliyesulubiwa kwa namna fulani kutokana na upendo wake kwa Kristo. Hivyo akawa mkombozi mshiriki kwa maana alikomboa binadamu pamoja naye, kwa njia yake na ndani mwake.

Kwa sababu hiyohiyo, yale yote ambayo Kristo msalabani alitustahilia kwa msingi wa haki, Maria alitustahilia kwa msingi wa upendo uliomuunganisha na Mungu. Kristo tu, akiwa kichwa cha binadamu wote, aliweza kustahili kwa haki tushirikishwe uhai wa Kimungu, lakini ilikuwa inafaa Mungu azingatie pia stahili za Maria aliyeungana naye katika kazi ya wokovu. Mapokeo yote ya mashariki na magharibi yanamuita Eva mpya, Mama wa wote upande wa roho, kama vile Eva alivyokuwa upande wa mwili. Basi Mama wa Kiroho wa watu wote anatakiwa kuwapa uzima wa Kiroho, ingawa si kama asili yake kuu. Msingi wa mafundisho hayo ni maneno ya Yesu kufani: “alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, ‘Mama, tazama mwanao’. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, ‘Tazama mama yako’. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake” (Yoh 19:26-27). Maneno hayo yalimhusu kwanza Yohane, lakini mtume huyo aliwakilisha watu wote waliokombolewa msalabani. Kwa kuwa Mungu anasema si tu kwa maneno, bali pia kwa matukio na watu ambao mikononi mwake wanamaanisha yale anayoyataka. Kama vile neno la Yesu lilivyosababisha ndani ya Maria mapendo makubwa ya kimama kwa mwanafunzi mpendwa, vilevile hayo mapendo yakaenea kwa wote na kumfanya kweli mama yao wa Kiroho. Basi, ikiwa mama mwema kwa uadilifu wake anaweza kuwastahilia watoto wake neema nyingi, zaidi Maria kwa ukamilifu wa upendo wake anawastahilia watu wote, ingawa si kwa msingi wa haki.

Kwa msingi huo kuna umuhimu wa kufanya mara nyingi sala ya washenga, yaani kuanza kuongea na Maria kwa tumaini kubwa atuunganishe na Mwanae kwa dhati, halafu kwa njia ya Mwokozi tuinukie muungano na Mungu.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. The term "Mediatrix" was applied to her in the dogmatic constitution Lumen gentium of the Second Vatican Council. "This, however, is to be so understood that it neither takes away from nor adds anything to the dignity and efficaciousness of Christ the one Mediator." Second Vatican Council, Lumen gentium, §62, November 21, 1964
  2. With special reference to Mary, the Catechism of the Catholic Church, quoting the Second Vatican Council, which in its document Lumen gentium referred to Mary as "'Advocate, Auxiliatrix, Adjutrix and Mediatrix," says: {{Quote|Taken up to heaven she did not lay aside this saving office but by her manifold intercession continues to bring us the gifts of eternal salvation. ...Therefore the Blessed Virgin is invoked in the Church under the titles of Advocate, Helper, Benefactress, and Mediatrix [Lumen gentium, 62]. Mary's function as mother of men in no way obscures or diminishes this unique mediation of Christ, but rather shows its power. But the Blessed Virgin's salutary influence on men ... flows forth from the superabundance of the merits of Christ, rests on his mediation, depends entirely on it, and draws all its power from it [Lumen gentium, 60]. No creature could ever be counted along with the Incarnate Word and Redeemer; but just as the priesthood of Christ is shared in various ways both by his ministers and the faithful, and as the one goodness of God is radiated in different ways among his creatures, so also the unique mediation of the Redeemer does not exclude but rather gives rise to a manifold cooperation which is but a sharing in this one source [Lumen gentium, 62]. Catechism of the Catholic Church, 969–970
  3. "Declaration of the Theological Commission of the Pontifical International Marian Academy", L'Osservatore Romano
  4. Mark Miravalle, 2008, Mariology: A Guide for Priests, Deacons, seminarians, and Consecrated Persons, Queenship Publishing ISBN|1-57918-355-7 page 448
  5. See also: the 1957 printing, late-1920s printing. Archived 1 Machi 2020 at the Wayback Machine., the Blessed Virgin Mary Queen of All Saints and Mother of Fair Love and Our Lady of the Sacred Heart of Jesus.
  6. Calendrier liturgique francophone 2010-2011