Maisha ya Bikira Maria
Mandhari
Maisha ya Bikira Maria kadiri ya historia yanajulikana hasa kutokana na habari zilizomo katika Injili nne zinazotumiwa na Wakristo pamoja na Matendo ya Mitume.
Humo tunasikia jinsi Bikira Maria:
- alivyokuwa ameposwa na Yosefu (Math 1:18),
- alivyopashwa habari na malaika Gabrieli kwamba ameteuliwa na Mungu kumzaa Yesu na alivyoitikia kwa imani na utiifu huko Nazareti (Lk 1:26-39),
- alivyosafiri haraka ili kumhudumia Elizabeti kwa muda wa miezi mitatu (Lk 1:30-56),
- alivyokwenda kuishi na Yosefu bila mahusiano ya kimwili (Math 1:24-25),
- alivyosafiri naye kwa ajili ya sensa (Lk 2:1-5),
- alivyomzaa Yesu karibu na Bethlehemu na kumvika nguo za kitoto na kumlaza horini (Lk 2:6-18),
- alivyotafakari sana habari za Mwanae (Lk 2:19, 51),
- alivyomtoa kwa Mungu katika hekalu la Yerusalemu siku arubaini baadaye (Lk 2:22-38),
- alivyomuonyesha kwa mamajusi kutoka mashariki na kupokea zawadi zao (Math 2:11),
- alivyokimbia Misri kwa usalama wa mtoto (Math 2:13-15),
- alivyorudi Palestina baada ya kifo cha mfalme Herode Mkuu (Math 2:19-21),
- alivyokwenda kuishi tena Nazareti (Math 2:22-23; Lk 2:39, 51),
- alivyokuwa akienda kuhiji Yerusalemu hasa kwa Pasaka (Lk 2:41),
- alivyopotewa na Mwanae kwa siku tatu huko Yerusalemu alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili (Lk 2:42-50),
- alivyoshiriki arusi ya Kana pamoja na Mwanae na kumuomba awasaidie wanaharusi kufanikisha sherehe (2:1-11),
- alivyomfuata Kapernaumu (Yoh 2:12),
- alivyomtembelea Yesu akiwa katika mizunguko ya utume wake (Mk 3:31),
- alivyosimama chini ya msalaba wa Yesu na kukabidhiwa naye mtume Yohane kama mwana (Yoh 19:25-27),
- alivyokwenda kuishi naye (Yoh 19:27),
- alivyodumu katika sala na Wakristo wa kwanza katika kumuomba Roho Mtakatifu awashukie (Mdo 1:14).
Habari nyingine zinapatikana katika Injili ya Yakobo na maandishi mengine, ikiwemo Kurani, tena katika mapokeo ya Kanisa, lakini hazikubaliwi na wote.
Kuhusu suala la Maria kuzaa watoto wengine, katika Biblia ya Kikristo hakuna habari hiyo; ingawa wanatajwa ndugu wa Yesu, yeye tu anaitwa "mwana wa Maria" (Mk 6:3).
Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Maisha ya Bikira Maria kama historia yake au athari wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |