Nenda kwa yaliyomo

Elizabeti (Injili)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mchoro wa karne ya 15 kuhusu Uzazi wa Mt. Yohane Mbatizaji, Elizabeti akiwa upande wa kushoto.
Mt. Zakaria akiandika jina la Mbatizaji kadiri ya Rogier van der Weyden.

Elizabeti (au Elisabeti, kwa Kiebrania אֱלִישֶׁבַע / אֱלִישָׁבַע, Elišévaʿ; kwa Kigiriki Ἐλισάβετ, Elisabet; kwa Kiarabu أليصابات, Alyassabat; maana yake ni "Mungu ameapa") alikuwa mwanamke wa ukoo wa Haruni aliyeolewa na Zakaria, kuhani mwaminifu wa Israeli katika karne ya 1 KK.

Hawakupata mtoto hadi uzeeni kutokana na utasa wa Elizabeti, lakini hatimaye walijaliwa kumzaa Yohane Mbatizaji.

Wote wanaheshimiwa kama watakatifu. Sikukuu ya wazazi ni tarehe 5 au 23 Septemba[1], kadiri ya madhehebu. Pengine wanaheshimiwa pamoja na mtoto wao tarehe 24 Juni.

Katika Injili[hariri | hariri chanzo]

Elizabeti (kushoto) akitembelewa na Bikira Maria kadiri ya Philippe de Champaigne.

Habari hizo zinapatikana hasa katika Injili ya Luka, sura ya 1 na ya 2. Humo inaelezwa Zakaria alivyopashwa na malaika Gabrieli kwamba atapata mtoto wa kiume ambaye atakakuwa nabii mkuu na kumtangulia Bwana[2].

Ingawa Zakaria hakusadiki mara, na kwa sababu hiyo aliadhibiwa kwa kufanywa bubu na kiziwi hadi ahadi itimie, siku ya kumtahiri mtoto alifungua tena kinywa chake na kutoa unabii.

Katikati ya matukio hayo, Elizabeti alitembelewa na jamaa yake, Bikira Maria, akiwa pia mja mzito[3]. Kabla ya kuongea lolote, salamu ya Maria ilimfanya Yohane aruke kwa shangwe tumboni mwa mamaye, na kusababisha Elizabeti atambue hali ya Maria na kumtolea kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu maneno ya sifa kwa imani yake na ujauzito wake wa pekee [4].

Katika Kurani[hariri | hariri chanzo]

Hata Kurani inamzungumzia bila kumtaja kwa jina, ikieleza Mungu alivyoponya utasa wake aweze kumzaa nabii Yahya, hasa katika sura ya 21.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Martyrologium Romanum
  2. 1:5 Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha Abia. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni. 6 Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama. 7 Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana. 8 Siku moja, ilipokuwa zamu yake ya kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu, 9 Zakariya alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani. 10 Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani. 11 Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani. 12 Zakariya alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. 13 Lakini malaika akamwambia, "Zakariya, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane. 14 Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. 15 Atakuwa mkuu mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake. 16 Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao. 17 Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake." 18 Zakariya akamwambia huyo malaika, "Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu." 19 Malaika akamjibu, "Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu, na nimetumwa niseme nawe, nikuletee hii habari njema. 20 Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia." 21 Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakariya huku wakishangaa juu ya kukawia kwake Hekaluni. 22 Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono Hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu. 23 Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani. 24 Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema: 25 "Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu."
  3. Lk 1:26 Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, 27 kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. 28 Malaika akamwendea, akamwambia, "Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe." 29 Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini? 30 Malaika akamwambia, "Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. 31 Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu. 32 Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. 33 Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho." 34 Maria akamjibu, "Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?" 35 Malaika akamjibu, "Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. 36 Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa. 37 Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu." 38 Maria akasema, "Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema." Kisha yule malaika akaenda zake.
  4. https://www.santiebeati.it/dettaglio/76150

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Elizabeti (Injili) kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.