Zakaria (Injili)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mchoro wa karne ya 15 kuhusu Uzazi wa Mt. Yohane Mbatizaji, Elizabeti akiwa upande wa kushoto.
Mt. Zakaria akiandika jina la Mbatizaji kadiri ya Rogier van der Weyden.
Zakaria na Yohane Mbatizaji katika picha ya ukutani ya Kigeorgia iliyoko Yerusalemu.

Zakaria (kwa Kiebrania זכריה, Zekariah; kwa Kigiriki Ζαχαρίας, Zakarias; kwa Kiarabu زَكَرِيَّا, Zakariya; maana yake ni "YHWH amekumbuka") alikuwa kuhani mwaminifu wa Israeli katika karne ya 1 KK. Mke wake aliitwa Elizabeti, naye pia alikuwa wa ukoo wa Haruni.

Hawakupata mtoto hadi uzeeni kutokana na utasa wa mwanamke, lakini hatimaye walijaliwa kumzaa Yohane Mbatizaji.

Wote wanaheshimiwa kama watakatifu. Sikukuu ya wazazi ni tarehe 5 au 23 Septemba[1], kadiri ya madhehebu. Pengine wanaheshimiwa pamoja na mtoto wao tarehe 24 Juni.

Katika Injili[hariri | hariri chanzo]

Habari hizo zinapatikana hasa katika Injili ya Luka, sura ya 1 na ya 2. Humo inaelezwa alivyopashwa na malaika Gabrieli kwamba atapata mtoto wa kiume ambaye atakakuwa nabii mkuu na kumtangulia Bwana[2].

Ingawa Zakaria hakusadiki mara, na kwa sababu hiyo aliadhibiwa kwa kufanywa bubu na kiziwi hadi ahadi itimie, siku ya kumtahiri mtoto alifungua tena kinywa chake na kutoa unabii.

Kadiri ya Lk 1:68-79, siku hiyo Zakaria alitunga wimbo ambao ni maarufu kwa jina la neno la kwanza katika tafsiri ya Kilatini, Benedictus (yaani "Asifiwe"). Katika madhehebu mbalimbali ya Ukristo, wimbo huo wa Kiinjili unatumika kila siku katika Masifu ya asubuhi.

Katika Kurani[hariri | hariri chanzo]

Hata Kurani inamtaja mara kadhaa kama nabii na mzazi wa nabii Yahya, hasa katika sura ya 3 na ya 19.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Martyrologium Romanum
  2. 1:5 Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha Abia. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni. 6 Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama. 7 Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana. 8 Siku moja, ilipokuwa zamu yake ya kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu, 9 Zakariya alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani. 10 Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani. 11 Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani. 12 Zakariya alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. 13 Lakini malaika akamwambia, "Zakariya, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane. 14 Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. 15 Atakuwa mkuu mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake. 16 Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao. 17 Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake." 18 Zakariya akamwambia huyo malaika, "Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu." 19 Malaika akamjibu, "Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu, na nimetumwa niseme nawe, nikuletee hii habari njema. 20 Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia." 21 Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakariya huku wakishangaa juu ya kukawia kwake Hekaluni. 22 Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono Hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu. 23 Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani. 24 Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema: 25 "Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu."

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:


Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Zakaria (Injili) kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.