YHWH

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Jina YHWH kwa alfabeti ya Kiebrania cha zamani (karne ya 10 KK hadi 135 BK), ya Kiaramu cha zamani (karne ya 10 KK hadi karne ya 4 BK) na ya mraba (karne ya 3 hadi sasa).

Herufi nne יהוה (YHWH) ni konsonanti za jina la Mungu linalopatikana mara 6,828 hivi katika Biblia ya Kiebrania kuanzia Mwa 2:4.

Jina hilo halipatikani kabisa katika vitabu vya Wimbo Ulio Bora, Kitabu cha Mhubiri na Kitabu cha Esta.

Wayahudi walizidi kuliheshimu jina hilo hata wakaacha kulitamka wakati wa kulikuta katika Maandiko Matakatifu; badala yake walikuwa wanasoma אֲדֹנָי, Adonai, yaani Bwana.

Labda kwa sababu hiyo watafsiri wa kwanza wa Biblia kwenda lugha ya Kigiriki (LXX) walilitafsiri Κύριος, Kyurios, yaani Bwana.

Kwa kuzoea hivyo, katika kutoa madondoo ya Agano la Kale, Wakristo wa kwanza walitumia tafsiri hiyohiyo.

Ndiyo sababu, katika Agano Jipya jina hilo halipatikani, isipokuwa kifupi kama Yah, hasa katika shangilio la Kiebrania Aleluya, yaani Msifuni Bwana.

Herufi zenyewe[hariri | hariri chanzo]

Ukuta wa mbele wa Basilika la Mt. Louis, lililojengwa mwaka 1834 huko St. Louis, Missouri, una jina hilo upande wa juu.

Herufi hizo nne, zikisomwa kutoka kulia kwenda kushoto ni:

Kiebrania Jina la herufi Matamshi
י Yodh "Y"
ה He "H"
ו Waw "W", "O" au "U")
ה He "H" (au kimya mwishoni mwa neno)

Matamshi[hariri | hariri chanzo]

Kwa kuwa jina liliachwa kutajwa, na maandishi asili hayakuwa na vokali, matamshi yake sahihi hayajulikani kwa hakika.

Hata hivyo, leo wataalamu wengi wanakubaliana kulitamka Yahweh, si Yehova kama miaka ya nyuma.