Mti wa Krismasi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Glade jul, mchoro wa Viggo Johansen (1891).
Msichana akipamba mti wa Krismasi, mchoro wa mwaka 1898: Marcel Rieder (1862-1942).

Mti wa Krismasi ni mti unaopambwa ili kuadhimisha Noeli (Krismasi).

Historia[hariri | hariri chanzo]

Desturi hiyo ilianzia katika Ujerumani; kuna ushuhuda kutoka karne ya 15 kuhusu miti ya Krismasi, hasa kutoka sehemu za kusini-magharibi za Ujerumani. Hapo huitwa Weihnachtsbaum au Christbaum) [1][2]

Maana yake kiasili ni mti wa Paradiso. Katika kalenda ya kanisa tarehe 24 Desemba ilikuwa siku ya kukumbuka Adamu na Eva. Hivyo ilikuwa kawaida kuwa na maigizo kanisani yaliyosimulia habari za Biblia zinazotokea katika masomo ya liturgia ya Krismasi. Mti wa Paradiso unahusiana na masimulizi ya dhambi ya asili na ujumbe wa Kristo kama Mwokozi anayekuja kuondoa dhambi hiyo.

Kutoka maigizo ya kanisani ishara ya mti uliopambwa matunda na vyakula mbalimbali iliingia katika nyumba za Wakristo ambako ulipambwa zaidi kwa matunda, keki tamu na pipi kwa watoto. Umekuwa mapambo ya nyumbani kwa majira ya Krismasi.

Ilienea nje ya Ujerumani katika nusu ya pili ya karne ya 19, kwanza katika matabaka ya juu.[3]

Katika karne ya 18 ulianza kupambwa kwa mishumaa ambayo baadaye walibadilishwa na taa za umeme.

Siku hizi kuna mapambo ya aina nyingi kulingana na utamaduni wa mahali. Pengine juu ya mti unawekwa malaika kumwakilisha Malaika Gabrieli, au nyota kuwakilisha ile iliyongoza Mamajusi kutoka mashariki.

Papa Yohane Paulo II aliingiza desturi hiyo huko Vatikani mwaka 1982, ingawa kulikuwa na upinzani fulani.

Tangu Krismasi kuwa nafasi muhimu kwa uchumi kuna pia maduka mengi yanayoweka miti hii na katika mazingira ya kibiashara uhusiano wake na mti wa Paradiso umesahauliwa mara nyingi.

Chaguo la mti[hariri | hariri chanzo]

Katika mazingira ya Ulaya, ambako mti wa Krismasi ulibuniwa, sikukuu inatokea wakati wa majira ya baridi. Hapo miti karibu yote inapotewa na majani yao na kukauka. Ni miti ya aina ya misonobari pekee inayoendelea kuwa na majani na kupatikana kama miti mibichi wakati wa baridi. Kwa hiyo ni misonobari, misprusi hasa, iliyotumiwa tangu mwanzo kama miti ya Krismasi, mwanzoni msprusi wa Norwei lakini sikuhizi spishi nyingine pia.

Katika nchi kadhaa za Ulaya na Marekani misonobari hupandwa kwenye mashamba maalumu na kukatwa kabla ya Krismasi kwa matumizi ya majira ya Krismasi. Katika miaka ya nyuma desturi ya kuweka miti ya Krismasi kama mapambo kwenye nyumba, mitaa na maduka imeenea katika nchi nyingi hata pasipo Wakristo.

Siku hizi miti bandia ya Krismasi hutengenezwa kwa plastiki na kutumiwa hasa pasipo misonobari au pia katika mazingira ya mjini ambako misitu iko mbali. Miti bandia inaweza kupunguza hatari ya moto zinazotokea kila mwaka nyumbani wakati wa sikukuu.

Picha[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. "History of Christmas Trees". History. Iliwekwa mnamo 15 December 2012.  Check date values in: |accessdate= (help)
  2. Christmas trees were hung in St. George's Church, Sélestat since 1521:Selestat.fr - Office de la Culture de Sélestat - The history of the Christmas tree since 1521 Archived 18 Desemba 2013 at the Wayback Machine.
  3. Ingeborg Weber-Kellermann (1978). Das Weihnachtsfest. Eine Kultur- und Sozialgeschichte der Weihnachtszeit [Christmas: A cultural and social history of Christmastide] (kwa German). Bucher. uk. 22. ISBN 3-7658-0273-5. Man kann als sicher annehmen daß die Luzienbräuche gemeinsam mit dem Weinachtsbaum in Laufe des 19. Jahrhunderts aus Deutschland über die gesellschaftliche Oberschicht der Herrenhöfe nach Schweden gekommen sind. (English: One can assume with certainty that traditions of lighting, together with the Christmas tree, crossed from the upper classes to the manor houses, from Germany to Sweden in the 19th century.) 

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mti wa Krismasi kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.