Ahera

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mchoro wa Misri ya Kale unaoonyesha safari ya kwenda ahera.

Ahera (pia: Akhera, kutoka neno la Kiarabu; kwa Kiingereza afterlife, yaani life after death au hereafter) ni neno linalotegemea imani ya kwamba baada ya mtu kufariki dunia anaendelea kuishi kwa namna nyingine, si kwamba anakoma kabisa.

Imani hiyo inaweza kutokana na hoja za falsafa lakini zaidi na mafundisho ya dini. Ili mtu aweze kukubali, ni lazima aone kwamba yeye si mwili tu, kwa sababu ni wazi kwamba kifo ni mwisho wa uhai wake duniani na kinaleta uharibifu wa mwili huo.

Wengi wanakubali ubora wa binadamu kati ya wanyama ni uwemo wa roho ndani yake, na kwamba ndiyo inayoweza kuendelea kuishi baada ya kutengana na mwili wake.

Hali hiyo ni ile ya mzimu na makazi yake yanaitwa kuzimu, walau mpaka siku ya kiyama au ya unyakuo, kadiri ya imani ya dini mbalimbali.

Wengi kati ya wanaomuamini Mungu pekee, kama vile Wayahudi, Wakristo na Waislamu, wanasadiki kwamba yeye anahukumu hizo roho na kuzipa tuzo au adhabu, ama mara baada ya kufa ama siku ya ufufuko: ndiyo hali za paradiso na jehanamu.

Wengine, hasa Wahindu, wanasadiki kwamba baada ya kifo roho inatwaa mwili mwingine, wa mtu au kiumbehai yeyote kulingana na stahili zake katika maisha yaliyokwisha.

Kwa msingi huohuo, Wabudha wanajitahidi kuachana na tamaa za kidunia ili hatimaye watoweke kabisa, wasizaliwe tena, kwa sababu kwao maisha ni mateso.

Wengine, hasa wakanamungu na watu wasio na dini, wanaona hakuna haja ya kujitahidi hivyo, kwa sababu kwao kufa ni mwisho wa yote moja kwa moja: mtu akifa amekufa tu, hakuna tarajio lolote.

Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.