Madina
Madina (pia: Medina; kwa Kiarabu: المدينة المنورة madinat-ul-munawwara yaani mji ulioangazwa) ni mji wa Saudia ya magharibi takriban km 320 kaskazini kwa Makka. Unaheshimiwa na kutembelewa na Waislamu kwa sababu ni mahali pa kuzikwa kwa Mtume Muhammad. Kumbe ni marufuku kwa wasio Waislamu wasiingie sawa na Makka.
Madina ina wakazi mnamo 900,000. Jina asilia ya mji lilikuwa Yathrib. Neno "madina" lamaanisha "mji".
Madina ina nafasi muhimu katika imani ya Kiislamu. Kufuatana na mapokeo ya Kiislamu Muhammad alifika huko mwaka 622 kwa njia ya hijra alipoondoka Makka kwa sababu ya upinzani dhidi yake.
Yathrib alipokewa vizuri na kuwa kiongozi wa kisiasa pamoja na kiongozi wa kiroho. Ndipo jina la "madinat-un-Nabii" (mji wa Mtume) lilianza kutumiwa.
Kwa kawaida huhesabiwa kuwa mji mtakatifu wa pili katika Uislamu baada ya Makka. Kuna msikiti wa Mtume penye kaburi la Muhammad mahali panapoaminiwa ni mahali pa nyumba yake alipoaga dunia. Kando yake kuna makaburi ya wenzake Muhammad.