Janani Luwum

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Picha halisi ya Askofu Janani Luwum wa Kanisa la Anglikana la Uganda aliyeuawa na Idi Amin.
Sanamu ya Janani Luwum (kulia) pamoja na mashahidi wengine wa Kikristo wa karne ya 20 kwenye ukuta wa mbele wa kanisa la Westminster, Uingereza.
Sanamu ya Askofu Janani Luwum kwa ukubwa zaidi.

Janani Jakaliya Luwum (1922 - 16 Februari 1977) alikuwa askofu mkuu wa Kanisa Anglikana la Uganda kati ya miaka 1974 na 1977. Alihesabiwa kuwa kati ya viongozi muhimu wa Kanisa la kikristo katika Afrika. Mwaka 1977 aliuawa ama na Idi Amin mwenyewe au kwa amri yake.

Anaheshimiwa na Waanglikana kama mtakatifu mfiadini.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 17 Februari. Sanamu yake iko kati ya zile za wafiadini wa karne ya 20 katika ukuta wa mbele wa Abasia ya Westminster, London.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Luwum alizaliwa Wilaya ya Kitgum kaskazini mwa Uganda katika familia ya Waacholi. Akasoma shule ya sekondari na chuo cha ualimu akawa mwalimu wa shule ya msingi.

Mwaka 1948 akawa Mkristo akaendelea kusomea uchungaji. Alikuwa dikoni mwaka 1953, akapadrishwa mwaka 1954 akihudumia kanisa lake katika dayosisi za Upper Nile na baadaye Mbale.

Mwaka 1969 alichaguliwa kuwa askofu wa dayosisi ya Gulu katika Uganda kaskazini.

Baada ya miaka 5 akawa askofu mkuu wa jimbo la Kanisa Anglikana katika Uganda, Rwanda, Burundi na Boga-Zaire akiwa Mwafrika wa pili aliyeshika nafasi hiyo mwaka 1974.

Kifodini[hariri | hariri chanzo]

Luwum alikuwa askofu mkuu wakati wa utawala wa kidikteta wa Idi Amin aliyetwaa urais wa Uganda tangu mwaka 1971.

Mwaka 1977 Luwum alipinga wazi matendo ya serikali iliyozidi kuwakamata na kuua wananchi ovyo. Amin alikasirika akamshutumu Luwum kuwa msaliti. Kosa lake lilikuwa kwamba hakunyamazia maovu, akiandika barua pamoja na viongozi wengine wa Kanisa kwa rais huyo kulaumu matendo mabaya ya wanajeshi wa serikali waliowatesa wananchi. Alijua hatari, lakini aliona ni wajibu wake kuwalinda Wakristo wake.

Tarehe 16 Februari 1977 Luwum alikamatwa pamoja na mawaziri 2. Wakamatwa walipelekwa mbele ya mkutano mkubwa mjini Kampala walipoonyeshwa mbele ya wananchi kama wasaliti waliotaka kumpindua Amin na kumrudisha rais wa awali Milton Obote.

Siku iliyofuata Redio Uganda ilileta tangazo kuwa wote watatu walikufa katika ajali ya gari walipojaribu kumshika dereva katika jaribio la kukimbia.

Lakini wakati wa mazishi ya Luwum ilionekana ya kwamba mwili wake ulitobolewa na risasi. Henry Kyemba aliyekuwa waziri wa afya chini ya Amin aliandika baadaye "Askofu mkuu alipigwa risasi mdomoni na mara tatu kifuani".

Mashahidi waliokuja mbele baada ya utawala wa Amin walisema ya kwamba wafungwa walipelekwa kwenye kambi la kijeshi walipopigwa na kuuawa. Wengine walisema ni Amin mwenyewe aliyepiga risasi, lakini wengine hawakukubali.

Luwum aliacha na mjane Mary Lawinyo Luwum na watoto 9.

Askofu Luwum anakumbukwa mpaka leo kama shahidi wa imani, yupo katika mfuatano wa mashahidi wengi tangu mwanzo wa Ukristo. Kifo chake kilisikitisha sana. Lakini vilevile kiliwapa Wakristo moyo wa kutonyamaza mbele ya uongo na maovu. Moyo huo umeonekana tangu mwanzo katika Ukristo.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]