Antoni Maria Claret

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mtakatifu Antoni Maria Claret katika mavazi ya kiaskofu.

Antoni Maria Claret i Clarà (23 Desemba 1807 - 24 Oktoba 1870) alikuwa askofu wa Kanisa Katoliki kutoka Hispania na mwanzilishi wa mashirika mawili ya kitawa ya kimisionari.

Alitangazwa na Papa Pius XI kuwa mwenye heri tarehe 25 Februari 1934, halafu Papa Pius XII alimtangaza mtakatifu tarehe 7 Mei 1950.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila tarehe 24 Oktoba[1].

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Antoni Maria Claret alizaliwa huko Sallent, karibu na Barcelona (katika mkoa wa Catalonia nchini Hispania) tarehe 23 Desemba 1807, akiwa mtoto wa mtengeneza sufu.

Alisoma shule katika kijiji chake, na alipotimiza miaka 12 akawa mfumaji.

Baadaye alikwenda Barcelona kufanya biashara, akabaki huko hadi alipotimiza umri wa miaka 20. Hata hivyo, alitenga muda wake kujisomea na kujifunza Kilatini na Kifaransa.

Baada ya kutambua wito wake mtakatifu katika maisha yake ya dini, aliondoka Barcelona.

Alitaka kuwa Mkartusi, lakini alijiunga na Seminari ya Vic mwaka 1829, na alipewa daraja takatifu ya upadri tarehe 13 Juni 1835. Alipokea zawadi kutoka Parokia yake, ambako aliendelea kusoma teolojia hadi mwaka 1839; lakini kwa kuwa wito wa umisionari ulizidi kuwa mkubwa alikwenda Roma (Italia).

Huko alijiunga na shirika la Yesu (Wajesuiti), lakini akaona hajalifurahia kwa maisha yalivyokuwa, hivyo alirudi muda mfupi tu Hispania na alifanya kazi ya uchungaji huko Viladrau na Girona, akiwavutia wengi kwa juhudi zake za kutetea maskini.

Aliitwa na wakubwa wake huko Vic, na kufanya kazi za kimisionari wakati wote akiwa Catalonia.

Mwaka 1848 alipelekwa Visiwa vya Canary ambako alifanya mafungo kwa miezi 15. Alirudi tena Vic, na kuanzisha Shirika la Kimisionari la Wana wa Moyo Safi wa Maria (Congregation of the Missionary Sons of the Immaculate Heart of Mary) tarehe 16 Julai 1849. Pia alianzisha Maktaba kuu ya Barcelona iliyoitwa "Librería Religiosa" (na sasa inaitwa Librería Claret), na iliyoweza kutoa mamilioni ya nakala kwa kazi nzuri zilizofanywa na Kanisa Katoliki zamani.

Kutokana na kazi yake nzuri na maombi ya Malkia Isabella II wa Hispania, Papa Pius IX alimteua kuwa askofu mkuu wa Santiago (Cuba) mwaka 1849.

Alipofika huko, alianza barabara kazi yake ya mageuzi/matengenezo katika Seminari ya Santiago, iliyobadilika na kuwa imara na yenye nidhamu. Kwa miaka miwili ya kwanza katika utumishi wake huko, zaidi ya ndoa 9,000, nyingi zikiwa za sheria za kimila, zilihalalishwa chini ya utaratibu wa Kikatoliki. Alijenga hospitali na shule kadhaa.

Katika matukio matatu tofauti, Claret alifanya ziara zenye mpangilio katika jimbo zima, zikiwemo misheni za wenyeji.

Mapenzi kwa kazi yake njema kulizua upinzani na wasiopenda maendeleo wa wakati huo, kama ilivyokuwa imetokea awali huko Hispania. Si chini ya majaribio 15 yalifanywa dhidi ya uhai wa Claret; taya lake liliachanishwa wazi kutoka sikio hadi kidevu kwa kisu cha mauaji huko mashariki mwa jimbo/eneo kuu la Holguin.

Mnamo Februari 1857, aliitwa na Malkia Isabella II wa Hispania, na kufanywa kuwa muungamishi wake. Alipata ruhusa ya kutorudi Cuba tena na aliteuliwa kwenda Trajanopolis. Kwa nyongeza alikuwa mshauri wa kiroho wa Malkia, na ndipo mvuto wake ulielekea zaidi katika kuwasaidia maskini na uenezaji wa elimu; aliishi kwa umakini na uadilifu mkubwa na alilazimika kuwa na makazi ndani ya hospitali huko Italia (yaani wanamolelewa maskini wasiojiweza).

Kwa miaka tisa alikuwa gombera wa seminari ya Escorial alikoanzisha maabara ya sayansi, makumbusho (museum) ya vitu halisi vya kihistoria, maktaba, chuo, na shule za muziki na lugha.

Malengo yake ya baadaye yaliharibiwa na Mapinduzi ya mwaka 1868, yaliyotupilia mbali utawala wa Malkia Isabella II na hivyo kuanzisha Jamhuri ya Hispania.

Mwaka 1869, Claret alirudi tena Roma kuandaa Mtaguso wa kwanza wa Vatikano. Kutokana na afya yake kutokuwa nzuri, alikwenda Prades (Ufaransa), ambako alikuwa bado akisumbuliwa na Wahispania maadui wake; muda si mrefu baada ya kuacha abasia ya Wasitoo huko Fontfroide, Narbonne, kusini mwa Ufaransa, alifariki dunia tarehe 24 Oktoba 1870 akiwa na umri wa miaka 63.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.