Nenda kwa yaliyomo

Kolumbani

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sura yake inavyoonekana katika dirisha la kanisa la abasia ya Bobbio, Italia, ambapo alifariki akazikwa.

Kolumbani abati (Columbán, maana yake "Njiwa mweupe"; 540 - 23 Novemba 615) alikuwa mmonaki mmisionari kutoka Ireland, maarufu kwa kuanzisha monasteri nyingi na kueneza Ukristo wa Kiselti katika nchi mbalimbali za Ulaya bara, ukiwa pamoja na kanuni kali ya kitawa, malipizi, na maungamo ya binafsi kwa padri.

Tangu kale anaheshimiwa na Wakatoliki na Waorthodoksi kama mtakatifu, hasa siku ya kifo chake, tarehe 23 Novemba[1].

Sala zake

[hariri | hariri chanzo]

Ee Kristo Bwana, utujalie daima maji haya yawe ndani mwetu pia chemchemi ya maji hai yanayobubujikia uzima wa milele!

Kwa hakika naomba jambo kubwa; nani asiyejua?

Lakini wewe, mfalme wa utukufu, unajua kuzawadisha makuu, tena umeahidi makuu.

Hakuna kilicho kikuu kuliko wewe: lakini umejizawadisha kwetu na kujitoa kafara kwa ajili yetu.

Kwa hiyo tunakuomba utujulishe tunachopenda, kwa kuwa hatutafuti chochote nje yako.

Kwetu wewe ni yote: uhai wetu, mwanga wetu, wokovu wetu, chakula chetu, kinywaji chetu, Mungu wetu.

Ee Yesu wetu, nakuomba uivuvie mioyo yetu kwa mvumo wa Roho wako na kuzichoma roho zetu kwa upendo wako ili kila mmojawetu aweze kusema kwa ukweli wote: Unijulishe mpenzi wa roho yangu; kwa kuwa nimejeruhiwa na upendo wako.

Ee Bwana, natamani madonda hayo yatiwe ndani mwangu.

Heri yake roho iliyochomwa na upendo! Yenyewe itatafuta chemchemi na kuinywea.

Kwa kuinywea ataionea kiu daima.

Kwa kutuliza kiu yake atatamani kwa ari yule anayemuonea kiu daima, ingawa anamnywa mfululizo.

Hivyo kwa roho upendo ni kiu inayotafuta kwa hamu, ni jeraha linaloponya.


Ee Kristo, Mwokozi wetu mwema sana, tafadhali uwashe taa zetu: ziangaze mfululizo katika hekalu lako na kudumishwa daima na wewe, mwanga wa milele; pembe zenye giza za roho zetu ziangazwe, na giza lolote la ulimwengu lifukuzwe mbali nasi.

Basi, Yesu wangu, uijalie taa yangu mwanga wako, ili kwa uangavu wake nifunguliwe patakatifu pa mbinguni, patakatifu pa patakatifu ambapo chini ya makuba yake makuu panakuwa na wewe, kuhani wa milele wa sadaka ya kudumu.

Unijalie nikutazame, nikukazie macho na kukutamani wewe tu; nikupende wewe tu na kukungojea wewe tu kwa hamu motomoto kabisa.

Katika kutazama kwa upendo hamu yangu izimike ndani mwako na mbele yako taa yangu iangaze na kuwaka mfululizo.

Tafadhali, Mwokozi wetu mpendwa, ujionyeshe kwetu tunaopiga hodi, ili, kwa kukufahamu, tukupende wewe tu, tukutamani wewe tu, tukufikirie mfululizo wewe tu, na kutafakari usiku na mchana maneno yako.

Tafadhali utumiminie upendo mkubwa ambao unakufaa wewe uliye Mungu na unastahili kupewa, ili upendo wako uenee katika nafsi yetu yote na kutufanya wako kabisa.

Hivyo hatutaweza kupenda chochote nje ya wewe uliye wa milele, na upendo wetu hautaweza kuzimwa na maji mengi ya uwingu huu, ya dunia hii na ya bahari hii, kama ilivyoandikwa, Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo.

Hayo yatimie hata kwetu kwa neema yako, Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye upewe utukufu milele na milele. Amina.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]

Maandishi yake

[hariri | hariri chanzo]
  • San Colombano abate, Istruzioni e regola dei monaci, Abbazia San Benedetto, Milano 1997.
  • San Colombano, Lettere e poesie, Abbazia San Benedetto, Milano 1998. ISBN 9788887796360
  • San Colombano. Le opere, a cura di Inos Biffi e Aldo Granata, Jaca Book, Milano 2001.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.