Nenda kwa yaliyomo

Ethiopia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Waethiopia)
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia
የኢትዮጵያ ፌዴራላዊ ዴሞክራሲያዊ ሪፐብሊክ (Kiamhara)
Wimbo wa taifa: ወደፊት ገስግሺ ፣ ውድ እናት ኢትዮጵያ
"Mbele Tembea, Mama Mpendwa Ethiopia"
Mahali pa Ethiopia
Mahali pa Ethiopia
Ramani ya Ethiopia
Ramani ya Ethiopia
Mji mkuu
na mkubwa nchini
Addis Ababa
9°1′ N 38°45′ E
Lugha rasmiKiafar
Kiamhara
Kioromo
Kisomali
Kitigrinya
SerikaliJamhuri ya shirikisho
 • Rais
 • Waziri Mkuu
Sahle-Work Zewde
Abiy Ahmed
Eneo
 • Eneo la jumlakm2 1 104 300 [1]
Idadi ya watu
 • Kadirio la 2023116 462 712[1]
Pato la taifaKadirio la 2024
 • JumlaOngezeko USD bilioni 192.013[2]
 • Kwa kila mtuOngezeko USD 1 787.176[2]
Pato halisi la taifaKadirio la 2024
 • JumlaOngezeko USD bilioni 393.297[2]
 • Kwa kila mtuOngezeko USD 3 719[2]
Maendeleo (2021)Ongezeko 0.498[3] - duni
SarafuBirr ya Ethiopia
Majira ya saaUTC+3
(Afrika Mashariki)
Msimbo wa simu+251
Msimbo wa ISO 3166ET
Jina la kikoa.et


Ethiopia au Uhabeshi (Kiamhara: ኢትዮጵያ Ityopp'ya) ni nchi ya Afrika ya Mashariki iliyoko kwenye Pembe ya Afrika.

Nchi zinazopakana na Ethiopia ni Sudan na Sudan Kusini upande wa magharibi, Eritrea na Jibuti kaskazini, Somalia mashariki na Kenya upande wa kusini.

Ni nchi ambayo ina historia ya pekee Afrika na hata duniani kwa ujumla.

Ethiopia ni moja ya nchi mbili za Afrika ambazo hazikutawaliwa na wakoloni wakati walipong’ang’ania Afrika. Nchi nyingine ni Liberia. Kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia Ethiopia ilivamiwa na Waitalia (1936) lakini ilipata uhuru wake tena baada ya miaka michache.

Jina

Asili ya jina "Ethiopia" haijulikani. Kuna maelezo mbalimbali lakini yote yanakosa uhakika. Hilo ni sawa pia kwa jina la pili la kihistoria ambalo ni "Habasha" ilikuwa "Uhabeshi".

Ethiopia mara nyingi linaelezwa kuwa neno la Kigiriki cha Kale Αἰθιοπία Aithiopia lililotokana na Αἰθίοψ "Aithiops" ; maana yake "uso" (ὄψ) "kuwaka" (αιθw) hivyo labda "uso uliochomwa" ama sura nyeusi. Lakini jina hili halikumaanisha hasa nchi ya Ethiopia ya leo lakini nchi zote zenye watu wenye rangi nyeusinyeusi. Kwa muda mrefu watu wa Ulaya waliita Afrika yote kwa jina "Ethiopia". Pia si wazi kama neno la Kiafrika lenye maana tofauti limechukuliwa na Wagiriki kwa maana ya neno lao la "aithiops".

Nchi yenyewe ilijulikana kwa muda mrefu wa historia yake kwa jina la Habasha. Habasha ilikuwa jina la Kiarabu kwa ajili ya nchi ikaingia kama "Uhabeshi" katika Kiswahili au "Abisinia" katika lugha za Ulaya. Asili ya jina hilo haliko wazi; wengine husema ni katika lugha ya kale ya nchi yenyewe kumaanisha "nchi kwenye nyanda za juu"; tena wengine wanadai kwamba jina limetoka Uarabuni wa kusini lilipokuwa jina la kabila moja lililohamia na watu walioleta lugha za kisemiti Ethiopia.

Jiografia

Tazama pia: Orodha ya mito ya Ethiopia

Ethiopia ina eneo la kilometa mraba 1,127,127 (maili mraba 435,071). Nchi yenyewe ni mojawapo ya nchi za Pembe ya Afrika upande wa mashariki.

Nchini Ethiopia kuna milima mirefu; sehemu kubwa ya nchi inaundwa na Nyanda za juu za Ethiopia zilizotenganishwa na Bonde la Ufa la Afrika Mashariki, ambalo limepasua kutoka kusini - magharibi kwenda kaskazini – mashariki na kuzungukwa na mbuga maeneo yaliyo chini. Mabonde na milima hasa nchini Ethiopia yanaathiri hali ya hewa, udongo, mimea, na makazi ya watu.

Ukweo wa milima na eneo la kijiografia vinasababisha aina mbili za hali ya hewa: eneo lililopoa liko zaidi ya ukweo wa mita 2,400 (futi 7,900) ambapo vipimo vya joto ni kati ya kuganda na 16°C (32°–61°F); vipimo vya joto kwa ukweo wa mita 1,500 na 2,400 (futi 4,900—7,900) joto ni 16°C hadi 30°C (61°–86°F); joto zaidi liko chini ya mita 1,500 (futi 4,900) ni hali ya hewa ya tropiki na hali ya hewa ya ukame na joto saa za mchana ni 27°C mpaka 50°C (81°–122°F).

Mvua ya kawaida ni kuanzia kati ya Juni mpaka kati ya Septemba lakini eneo la milima ya kusini mvua hunyesha zaidi ikianzia na mvua kidogo ya Februari ama Machi.

Ethiopia ni nchi ambayo ina ikolojia tambakazi. Ziwa Tana, ambalo liko kaskazini mwa nchi, ndilo chanzo cha Mto Naili ya Buluu (kwa Kiarabu: Bahr al Zraq). Eneo la mto huo lina aina za wanyama za pekee kama Gelada - nyani, Walia ibeka na pia Mbwa mwitu.

Historia

Historia ya awali

Historia ya binadamu katika Ethiopia ilianza mapema kabisa. Mifupa ya kale kabisa ya viumbe jamii ya watu imepatikana katika nchi hii kwa sababu zilihifadhiwa katika mazingira yabisi ya nchi.

Wataalamu wengi huamini ya kwamba Ethiopia (pamoja na Kenya na Tanzania) inaweza kuwa mahali ambako watu wa aina ya Homo Sapiens walianza kupatikana duniani.

Kuna mabaki mbalimbali ya kiutamaduni yanayochunguzwa na akiolojia, lakini sehemu kubwa ya nchi haijaangaliwa bado kitaalamu. Inaonekana kwamba katika karne za K.K. kulikuwa na uhusiano wa karibu na Uarabuni kwa sababu lugha za Kiethiopia ni karibu na lugha za upande mwingine wa Bahari ya Shamu. Inaaminiwa kwamba watu kutoka Uarabuni Kusini walihamia Ethiopia na kuleta lugha yao huko.

Biblia ina taarifa juu ya ziara ya malkia wa Sheba aliyemtembelea mfalme Suleimani wa Yerusalemu. Milki ya Sheba imedaiwa kuwepo ama Ethiopia au Yemen na wengine huamini ya kwamba ilikuwa dola la pande zote mbili za mlangobahari wa Bab el Mandeb unaotenganisha Eritrea ya leo na Uarabuni Kusini.

Historia ya kale

Milki ya kwanza ya Ethiopia inayoweza kutajwa kutokana na mabaki ya majengo na maandishi ilikuwa milki ya D'mt (pia: Da'amot) katika Ethiopia ya kaskazini pamoja na Eritrea ya leo. Kuna mabaki ya hekalu la Yeha pamoja na makaburi ambako majina ya wafalme kadhaa yamehifadhiwa kwa maandishi kwenye mawe. Lugha ilikuwa karibu sana na lugha za kale za Uarabuni. Ilikuwa na athira juu ya sehemu za kaskazini ya Ethiopia kwa kipindi kikubwa cha milenia ya 1 KK.

Ilifuata milki kubwa ya Aksum, iliyoanzishwa wakati wa kuzaliwa Yesu. Ufalme wa Aksum ulikuwa milki ya kwanza kutawala maeneo makubwa ya Ethiopia. Nabii Mwajemi Mani aliuweka Ufalme wa Aksum kwa utukufu sawa na Roma, Uajemi na Uchina kama nchi zilizokuwa na nguvu duniani karne ya 3 BK, wakati yeye alipoishi.

Ilikuwa karne ya 4 BK ambapo Frumentius, mtu Msiro-Mgiriki aliyekuwa amepotelea baharini kutokana na kuzama kwa jahazi, alishikwa na Wahabeshi na kupelekwa kortini na baadaye kumuongoa mfalme Ezana kuingia Ukristo. Kwa hiyo Wahabeshi wakampa jina Abba Selama. Kwa muda mfupi dini hiyo mpya ilienea kote[4].

Mara nyingi karne ya 6 Aksum ilitawala eneo la Yemeni ng'ambo ya Bahari ya Shamu.

Aksum ilistawi hasa kutokana na biashara kati ya Mediteranea na Bara Hindi iliyopita kwenye mlangobahari wa Bab el Mandeb ikatumia bandari ya Adulis (karibu na Massawa ya leo nchini Eritrea).

Uenezi wa Uislamu ulivuruga biashara hiyo na Aksum ilipoteza utawala juu ya pwani. Kuporomoka kwa uwezo wa kibiashara kunaonekana katika kusimamishwa kwa uchapaji pesa ya wafalme wa Aksum katika karne ya 7. Nchi ilishambuliwa pia kutoka milki za barani.

Mabaki ya ufalme wa Aksum yaliharibiwa mnamo mwaka 900 wakati na malkia Gudit (au Judith) aliyekuwa ama Myahudi ama kiongozi wa makabila ya Kipagani kutoka nyanda za juu.

Milki ya Ethiopia

Kiongozi wa kabila la Agaw alimwoa binti wa mfalme wa mwisho wa Aksum akaanzisha nasaba ya Zagwe na kuunda upya ufalme wa Kikristo katika nyanda za juu. Kitovu cha ufalme huu kilipelekwa zaidi mbali na pwani.

Nasaba hii ilipinduliwa mnamo 1270 na Yekuno Amlak aliyetumia jina la kifalme Tasfa Iyasus. Alianzisha nasaba iliyojiita "Wa Suleimani" kwa kudai ilikuwa ukoo wa mwana wa mfalme Suleimani na malkia wa Sheba. Tasfa Iyasus alitumia cheo cha Negus Negesti ("Mfalme wa Wafalme").

Enzi ya Mfalme Lebna Dengel, Ethiopia iliweza kuwasiliana na nchi za Ulaya na kudumisha ubalozi na nchi kama Ureno. Lakini, Mfalme Susenyos alipojiunga na Kanisa Katoliki mwaka 1622, chakari na misukosuko ilifuata. Wamisionari Wajesuiti walichukiwa na waamini wa Kanisa la Ethiopia, na katika hiyo karne ya 17 Susenyos mwana wa Mfalme Basil aliwafukuza wanamisheni hao.

Baadaye Waoromo wakaanza kuasi amri ya Kanisa la Ethiopia na kutafuta njia za dini yao, eneo hili la Uhebeshi.

Mambo hayo yote yalifanya Ethiopia itengwe miaka ya 1700. Wafalme wakawa kama wakurugenzi, ambao waliamriwa na masharifu kama Ras Mikael Sehul wa Tigrinya. Ethiopia ilitoka kutoka utengo kwa kufuatia misheni ya Uingereza kufika Ethiopia na kukamilisha muungano kati ya nchi hizi mbili; lakini, hadi milki ya Tewodros II ndipo Ethiopia ilipoanza tena shauri za Duni.

Mashujaa Ethiopia karne ya 1800

Miaka ya 1880 ilikuwa miaka ya Ulaya kung’ang’ania ukoloni Afrika ambapo Waitalia na Waingereza walitafuta kutawala eneo la Assab, bandari iliyoko karibu na mdomo wa bahari ya Shamu. Bedari ya Kusini, karibu na kiingilio cha bahari ya Shamu, ilinunuliwa na Waitalia kutoka sultani mwenyeji Machi 1870 ambayo mwaka 1882 ilizaa koloni la Eritrea.

Haya yalizua magombano kati ya Waethiopia na Waitalia na Vita vya Adowa mwaka 1896, ambapo Waethiopia walishtua dunia kwa kupiga nguvu za wakoloni na kulinda madaraka yao kwa uongozi wa Menelik II. Italia na Ethiopia zilisaini mkataba wa amani tarehe 26 Oktoba 1896.

Karne ya 20 hadi leo

Karne ya 20 miaka ya kwanzakwanza ilimilikiwa na Mfalme Haile Selassie, aliyechukua nafasi ya kuendeleza Ethiopia mpaka uongozi wake ulipokatizwa kwa Vita ya pili ya Uhabeshi na Italia (1936).

Waingereza na wazalendo wa Jeshi la Ethiopia wakakomboa nchi mwaka 1941, na Waingereza kukiri madaraka ya Ethiopia kwa mkataba wa Uingereza na Ethiopia mnamo Desemba 1944.

Milki ya Haile Selassie ilikoma mwaka 1974, ambapo Wakomunisti wa "Derg" walimpindua na kuanzisha serikali ya kikomunisti chini ya Mengistu Haile Mariam.

Mapinduzi hayo yalifuatwa na msukosuko wa vita na migogoro pamoja na ukame na shida za wakimbizi.

Mwaka 1977 Somalia ilivamia eneo la Ogaden (Vita vya Ogaden), lakini Ethiopia iliweza kuwafukuza Wasomali kwa msaada wa vifaa vya kijeshi vya Urusi, na majeshi ya Kuba, Ujerumani Mashariki na Yemeni. Usaidizi mwingi kutoka Nchi za Kikomunisti uliwezesha Ethiopia kudumisha mojawapo ya majeshi kubwa Afrika.

Lakini hii haikuzuia ukereketwa wa jimbo la Eritrea na Tigray, ambapo ukame wa mwaka 1985 na mapinduzi ya siasa hasa kwa Kambi za Ujamaa, zilileta uongozi wa Derg 1991 kukoma. Chama cha kukomboa Eritrea (EPLF) na Chama cha Mapinduzi cha Kidemokrasi Ethiopia (EPRDF), ziliungana kukomboa Ethiopia, wengi wa wanamgambo wakiwa wanaharakati wa Eritrea.

Mwaka 1993 jimbo la Eritrea likawa huru kutoka Ethiopia, kufuatia kura ya maoni iliyofanywa ili kumaliza vita hivyo vilivyodumu miaka 20, mmojawapo kati ya migogoro ya muda mrefu zaidi Afrika.

Mwaka 1994 Ethiopia kaiweka Katiba mpya ambayo ilileta uchaguzi wa kidemokrasia.

Mwaka 1998 magombano ya mipaka na Eritrea yalileta Vita vya Eritrea na Ethiopia ambayo vilidumu hadi Juni 2000. Vita hivyo vilileta uvivu wa uchumi na nguvu ya muungano unaongoza nchi.

Siasa

Uchaguzi wa Ethiopia ulipitisha wanabaraza 547 Bungeni. Baraza hilo la bunge lilijumuika Juni 1994 na kupitisha katiba mpya ya Jimbo la Demokrasia ya Jamhuri ya Ethiopia mnamo Desemba 1994. Uchaguzi huu ulikuwa wa kwanza kuchagua wanabaraza wa kitaifa kwa sifa bungeni na wanabaraza wa majimbo mnamo Mei na Juni 1995. Vyama vingi vya upinzani viligoma kushiriki uchaguzi. Ushindi ulichukuliwa na Chama cha Mapinduzi cha Kidemokrasi cha Watu wa Ethiopia (EPRDF). Umoja wa Mataifa ukasema vyama vya upinzani vingeweza kushiriki uchaguzi kama zingetaka.

Serikali ya Majimbo ya Demokrasia ya Jamhuri ya Ethiopia ilichukua mamlaka mnamo Agosti 1995. Rais wa kwanza Negasso Gidada. EPRDF ikaongoza serikali na Waziri Mkuu Meles Zenawi ambaye aliunga mkono majimbo ya kikabila, na kuwapa madaraka viongozi wa kikabila. Ethiopia sasa ina majimbo 9 ambayo yana serikali ya madaraka ya shirika, na hata majimbo haya yanakubaliwa kutoza ushuru na kutumia akiba ya ushuru. Hata hivyo, uhuru wa habari na kisiasa bado umefinywa.

Serikali ya Zenawi ilichaguliwa tena mwaka 2000 kwa uchaguzi wa kwanza wa Kidemokrasia, Rais akiwa Girma Wolde-Giorgis.

Kutoka 1991, Ethiopia imetafuta urafiki zaidi na Marekani na Umoja wa Ulaya, ili kuweza kukopa fedha za kusaidia uchumi wake na pia kutoka Benki ya Dunia.

Mwaka 2004, serikali ilianza kuhamisha watu kutoka maeneo ya ukame wakisema hii itazuia njaa. [1].

Uchaguzi mwingine wa Ethiopia ulikuwa tarehe 15 Mei 2005, ambao ulivutia wapigakura kiasi cha juu zaidi, asilimia 90% ya wananchi waliojiandikisha. Watazamaji wa Umoja wa Ulaya walidai uchaguzi haujafikia kiwango cha kimataifa, lakini Umoja wa Afrika ulitoa ripoti tarehe 14 Septemba kwamba Waethiopia walionyesha kujitokeza na kuheshimu demokrasia, halafu tarehe 15 Septemba, Carter Center, ikasema matokeo ya uchaguzi yaaminika na kuonyesha ushindani wa kisiasa. Uangalizi na ushuhuda wote ulimalizia kuranki Uchaguzi wa Ethiopia na kesi nyingine waipa, asilimia 64% ya matokeo mazuri, na vizuri zaidi kulingana na kesi nyingine 24%.

Arat Kilo monument
Commercial Bank of Ethiopia
Meskel Square
Kanisa kuu la Mt. George (Addis Ababa)
Thieta Hager Fikir (April 2006)
Kituo cha TV ya Ethiopia
Makao makuu ya Polisi

Katika Uchaguzi wa Ethiopia, 2005 EPRDF ilitokea iking’ang’ania uongozi. Tarehe za kwanza za Juni na tena Novemba, polisi kwa amri ya EPRDF wakafyatua risasi na kuua watu kwa maandamano yaliyokuwa yakipinga matokeo ya kura.

Ni kwamba vyama vya upinzani vililalamika kwamba EPRDF iliiba kura na kuwazisha wananchi na kusema baraza 299, wapata hitilafu ya wizi wa kura. Hayo yote yalichunguzwa na Watazamaji wa Uchaguzi wa kimataifa na pia Kamisheni ya Uchaguzi Ethiopia.

Matokeo ya uchunguzi huo kama haijatokea mnamo Juni 2005, wanafunzi wa chuo kikuu walianza maandamano wakisaidiwa na wanamgambo wa Muungano wa Vyama vya Upinzani. Lakini serikali kwa kutoa amri ya kukomesha maaandamano, mnamo 8 Juni, watu 26 waliuliwa mjini Addis Ababa kwa msukosuko wa maandamano na wengine wengi kushikwa.

Mnamo 5 Septemba 2005, Kamisheni ya Uchaguzi Ethiopia, ilitoa matokeo na kusema kwamba (EPRDF) kashinda uchaguzi na kwa hiyo iongoze serikali. Lakini vyama vya upinzani viliongezea viti bungeni kutoka 12 mpaka 176. Muungano wa umoja na demokrasia ulishinda viti vyote vya Addis Ababa, kwa Bunge la Taifa na Baraza la mtaala.

Maandamano yalizuka tena mitaani 1 Novemba, ambapo vyama vya upinzani viliitisha mgomo kwa jumla na pia kwa Bunge mpya, wakatae matokeo ya uchaguzi. Polisi tena walijaribu kuzuia maandamano hayo na watu 42 wakafa kwa misukosuko mjini Addis Ababa. Polisi saba pia wakafa na mwingine pia kafa kutokana na majeruhi ya mlipuko wa bomu. Tope la watu walishikwa na kufungwa jela. Februari 2006 watu elfu sita bado walikuwa jela wakingoja hukumu Machi.

Mnamo 14 Novemba, Bunge la Ethiopia lilipitisha mkataba kuimarisha Kamisheni huru na kuchunguza visa vya 8 Juni na tarehe 1 na tarehe 2 Novemba. Februari 2006 Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair, alitamka kwamba, EPRDF kashinda kura, lakini angetaka kuona Ethipia ikitatua shida zake yenyewe na iendelee katika njia ya demokrasia. [2].

Majimbo ya Kujitawala

Ethiopia imegawiwa katika majimbo 9 ya mamlaka ya kikabila (kililoch; umoja: kilil), na maeneo 68.

Zaidi ya hayo kuna maeneo ya miji miwili (astedader akababiwoch; umoja: astedader akababi): Addis Ababa na Dire Dawa.

Watu

Gari huko Adama (Nazareth), Ethiopia.

Idadi ya wakazi ilikadiriwa kuwa 113,656,596 (2022) ambao wanaongezeka kwa asilimia 2.88 kwa mwaka.

Ethiopia ina makabila zaidi ya 80 yenye utamaduni tofautitofauti. Watu wengi huongea lugha za Kisemiti na lugha za Kikushi.

Waoromo (34.49%), Waamhara (26.89%), Wasomali (6.20%) na Watigrinya (6.07%) ni zaidi ya 73% ya wananchi wote. Kumbe kuna makabila mengine yenye watu wachache kiasi kama 10,000.

Lugha

Ethiopia ina lugha 84 za kienyeji (angalia Orodha ya Lugha za Ethiopia). Mifano fulani ni kama ifuatavyo:

Kiingereza ndiyo lugha ya kigeni inayoongelewa zaidi na kufunzwa katika shule ya upili.

Kiamhara ilikuwa lugha ya ufundishaji katika shule ya msingi lakini sasa sehemu nyingi nafasi yake imeshikwa na Kioromo na Kitigrinya.

Dini

Wakristo, ambao ndio wengi (67.3%, kati yao Waorthodoksi wa mashariki 43.8%), wanaishi hasa kwenye milima, na Waislamu (31.3%) na Wapagani (0.6%) wengi wanaishi kwenye mabonde.

Ukristo

Picha katika ngozi inayomuonyesha padri wa Kanisa Orthodoksi la Ethiopia Tewahedo akichezea ala za muziki za kienyeji.

Ufalme wa Aksum ulikuwa milki na nchi ya kwanza kukubali Ukristo, ambapo askofu Frumentius wa Taya, aliyetumwa na Atanasi wa Aleksandria kuiinjilisha nchi, alimuongoa Ezana wa Aksum katika karne ya 4. Kwa hiyo Wahabeshi wakampa jina Abba Selama. Kwa muda mfupi dini hiyo mpya ilienea kote[5].

Labda Frumentius alifika tayari na wamonaki kama wamisionari. Lakini umonaki hasa ulianza mnamo mwaka 500 walipofika wamonaki tisa wenye asili ya Siria waliotokea Misri katika monasteri za Pakomi.

Hivyo mpaka leo mtindo huo ndio unaotawala kati ya umati wa wamonaki wa Ethiopia, wakati wakaapweke ni wachache, ingawa hawajawahi kukosekana. Athari za Siria na Misri zinajitokeza katika mambo mengi.

Wamonaki wanaishi katika vibanda vya binafsi wakikutana kwa sala tu. Wamonaki wanawake (kawaida ni wajane) wanaishi jirani na monasteri ya kiume wakiitegemea kiroho na kiuchumi.

Uislamu

Uislamu nchini Ethiopia unapatikana kutoka mwanzo wa dini hiyo; ambapo nabii Muhammad aliwaambia Waislamu waepuke kuuliwa Maka kwa kukimbilia Uhabeshi, ambayo ilitawaliwa na Mfalme Mkristu.

Hata utamaduni wa Kiislamu wasema Bilal, mfuasi wa Nabii Muhammad, alikuwa ametokea Ethiopia.

Uyahudi

Wayahudi, ambao wanaitwa Beta Israeli a Wafalasha, walioishi Ethiopia tangu karne nyingi, wengi wao wamehamia Israeli hasa katika karne ya 20.

Dini za jadi

Mbali na dini hizo za kimataifa, kuna wafuasi wa dini za jadi za Kiafrika.

Utamaduni

Mnamo Aprili 2005, Mnara wa Aksum, mojawapo ya dafina za kidini Ethiopia, ulirudishwa na Waitalia [6] ambao waliunyakua mwaka 1937 na kuupeleka Roma. Italia ikakubali kuurudisha mnamo 1947 kulingana na mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Ethiopia ndiyo Nyumba ya kiroho ya Mwendo wa Rastafari, ambao wanaamini Ethiopia ni Zion. Warastafari wamuona mfalme Haile Selassie I kama Yesu.

Sikukuu

Ona pia: Kalenda ya Waethiopia

Tarehe Jina za Kiswahili Jina za waenyeji Maelezo
7 Januari Waminina Siku ya Krismasi Genna  
10 Januari Siku kuu ya sadaka 'Id al-Adha ya kutegemea; tarehe ya 2006
19 Januari Siku kuu ya Epifania Timket  
2 Machi Siku ya Adwa Ye'adowa B'al  
11 Aprili Kuzaliwa kwa nabii Muhammad Mawlid an-Nabi ya kutegemea; tarehe ya 2006
21 Aprili Waminina Ijumaa ya Pasaka Siqlet (kusulubiwa) ya kutegemea; tarehe ya 2006
23 Aprili Waminina Pasaka Fasika ya kutegemea; tarehe ya 2006
24 Aprili Jumatatu ya Pasaka (sikukuu)   ya kutegemea; tarehe ya 2006
Mei 1 Siku ya Wafanyakazi Kimataifa    
Mei 5 Siku ya wazalendo Arbegnoch Qen  
Mei 28 Siku ya Taifa   Kuanguka kwa Derg
18 Agosti   Buhe  
11 Septemba Mwaka mpya wa Ethiopia Inqut'at'ash  
27 Septemba Kutafuta Msalaba Halisi Meskel  
24 Oktoba Mwisho wa Mwezi wa Ramadhani 'Id al-Fitr ya kutegemea; tarehe ya 2006

Uchumi

Mwanamke mkulima wa mbuni na kapu la mbegu za kahawa huko Ethiopia

Ethiopia imebaki nchi fukara mojawapo: Waethiopia wengi wanapewa chakula cha msaada kutoka ng’ambo.

Baada ya mapinduzi ya mwaka 1974, uchumi wa Ethiopia ulikuwa uchumi wa kijamaa: amri ya uchumi iliwekwa na jimbo, na upande mkubwa wa uchumi uliwekwa kwa jamii, kutoka viwanda vyote vya kisasa, kilimo cha biashara, taasisi za kukopesha na mashamba yote na mali yote ya kukomboa.

Kutoka kati ya 1991, uchumi ulianza kutolewa katika ujamaa na kuendekeza uchumi wa soko huria, serikali inasisitiza uchumi wa rasilimali ili kuzuia uvivu wa uchumi uliojitokeza wakati wa amri ya ujamaa. Mwaka 1993, Ubinafsishaji wa kampuni kaanza, viwanda, mabenki, ukulima, biashara za ndani na biashara za kimataifa.

Kilimo ni karibu asilimia 41% ya mapato ya uchumi (GDP), ambayo ni asilimia 80 ya biashara ya kimataifa, na asilimia 80 ya wananchi wanategemea kilimo.

Mambo mengi ya biashara hutegemea ukulima, wauzaji, viwanda vya kufunganya na kuuza nje mavuno ya ukulima. Mavuno yanayouzwa nje mengi yanatolewa na wakulima wa kiasi binafsi. Wanazalisha kahawa, nafaka (hasa maharagwe), mbegu za mafuta, viazi, miwa, na mboga.

Biashara ya nje hasa ni ya kuuza mazao, kahawa ikiwa ndiyo inayoleta pesa nyingi za kigeni.

Mifugo ya Ethiopia inaaminika kuwa ndiyo wengi zaidi Afrika. Mnamo 1987 ilihesabika kuwa asilimia 15 ya mapato ya uchumi yanatokana na mifugo.

Michezo

Ethiopia ni nchi mojawapo inayotoa wanariadha wazuri zaidi duniani, hasa kama wa mbio wa masafa ya kati na masafa marefu. Kenya na Morocco ni wapinzani wa Ethiopia kwa Michezo ya mabingwa wa Dunia na Olimpiki kwa masafa ya kati na marefu.

Machi 2006, Waethiopia wawili walitamalaki mbio za masafa marefu, kwa jina wakiwa: Haile Gebreselassie (Bingwa wa Dunia na Olimpiki) aliyevunja rekodi ya kilometa 10 na sasa pia kilomita 20, NusuMarathoni, na rekodi ya kilomita 25, na kijana Kenenisa Bekele (bingwa wa dunia, mbio za majira (bara), na pia bingwa wa olimpiki), anayeshikilia Rekodi za Dunia za mita 5,000 na 10,000.

Huko nyuma Ethiopia ilitoa mwanariadha maarufu katika historia ya mchezo huu duniani, Abebe Bikila.

Tazama pia

Marejeo

  1. 1.0 1.1 "Ethiopia". The World Factbook (kwa Kiingereza) (tol. la 2024). Shirika la Ujasusi la Marekani. Iliwekwa mnamo 23 Machi 2024.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  2. 2.0 2.1 2.2 2.3 "World Economic Outlook Database, October 2023 Edition. (Ethiopia)". IMF.org. International Monetary Fund. 10 Oktoba 2023. Iliwekwa mnamo 12 Oktoba 2023.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  3. "Human Development Report 2021/2022" (PDF) (kwa Kiingereza). Mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa. Septemba 8, 2022. Iliwekwa mnamo Septemba 8, 2022.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  4. https://www.avvenire.it/agora/pagine/ritrovate-le-chiese-piu-antiche-dell-africa-subsahariana
  5. https://www.avvenire.it/agora/pagine/ritrovate-le-chiese-piu-antiche-dell-africa-subsahariana
  6. http://news.bbc.co.uk/1/hi/world/africa/4458105.stm
  • Zewde, Bahru (2001). A History of Modern Ethiopia, 1855–1991 (tol. la 2nd). Athens, OH: Ohio University Press. ISBN 0-8214-1440-2.
  • Selassie I., Haile (1999). My Life and Ethiopia's Progress: The Autobiography of Emperor Haile Selassie I. Translated by Edward Ullendorff. Chicago: Frontline. ISBN 0-948390-40-9.
  • Deguefé, Taffara (2006). Minutes of an Ethiopian Century, Shama Books, Addis Ababa, ISBN 99944-0-003-7.
  • Hugues Fontaine, Un Train en Afrique. African Train, Centre Français des Études Éthiopiennes / Shama Books. Édition bilingue français / anglais. Traduction : Yves-Marie Stranger. Postface : Jean-Christophe Belliard. Avec des photographies de Matthieu Germain Lambert et Pierre Javelot. Addis Abeba, 2012, ISBN 978-99944-867-1-7. English and French. [3]
  • Henze, Paul B. (2004). Layers of Time: A History of Ethiopia. Shama Books. ISBN 1-931253-28-5.
  • Marcus, Harold G. (1975). The Life and Times of Menelik II: Ethiopia, 1844–1913. Oxford, U.K.: Clarendon. Reprint, Trenton, NJ: Red Sea, 1995. ISBN 1-56902-009-4.
  • Marcus, Harold G. (2002). A History of Ethiopia (tol. la updated). Berkeley: University of California Press. ISBN 0-520-22479-5.
  • Mauri, Arnaldo (2010). Monetary developments and decolonization in Ethiopia, Acta Universitatis Danubius Œconomica, VI, n. 1/2010, pp. 5–16. [4] and WP [5]
  • Mockler, Anthony (1984). Haile Selassie's War. New York: Random House. Reprint, New York: Olive Branch, 2003. ISBN 1-902669-53-3.
  • Murphy, Dervla (1968). In Ethiopia with a Mule. London: Century, 1984, cop. 1968. N.B.: An account of the author's travels in Ethiopia. 280 p., ill. with a b&w map. ISBN 0-7126-3044-9
  • Rubenson, Sven (2003). The Survival of Ethiopian Independence (tol. la 4th). Hollywood, CA: Tsehai. ISBN 0-9723172-7-9.
  • Siegbert Uhlig, et al. (eds.) (2003). Encyclopaedia aethiopica, Vol. 1: A-C. Wiesbaden: Harrassowitz Verlag.
  • Siegbert Uhlig, et al. (eds.) (2005). Encyclopaedia aethiopica, Vol. 2: D-Ha. Wiesbaden: Harrassowitz Verlag.
  • Siegbert Uhlig, et al. (eds.) (2007). Encyclopaedia aethiopica, Vol. 3: He-N. Wiesbaden: Harrassowitz Verlag.
  • Siegbert Uhlig & Alessandro Bausi, et al. (eds.) (2010). Encyclopaedia aethiopica, Vol. 4: O-X. Wiesbaden: Harrassowitz Verlag.
  • Alessandro Bausi & S. Uhlig, et al. (eds.) (2014). Encyclopaedia aethiopica, Vol. 5: Y-Z and addenda, corrigenda, overview tables, maps and general index. Wiesbaden: Harrassowitz Verlag.
  • Abir, Mordechai (1968). Ethiopia: The Era of the Princes; The Challenge of Islam and the Re-unification of the Christian Empire (1769–1855). London: Longmans.
  • Beshah, Girma and Aregay, Merid Wolde (1964). The Question of the Union of the Churches in Luso-Ethiopian Relations (1500–1632). Lisbon: Junta de Investigações do Ultramar and Centro de Estudos Históricos Ultramarinos.{{cite book}}: CS1 maint: multiple names: authors list (link)
  • Munro-Hay, Stuart (1991). Aksum: An African Civilization of Late Antiquity (PDF). Edinburgh: University Press. ISBN 0-7486-0106-6. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2013-01-23. Iliwekwa mnamo 2016-03-30.
  • Valdes Vivo, Raul (1977). Ethiopia's Revolution. New York: International Publishers. ISBN 0717805565.

Viungo vya nje

Serikali

Habari

Masomo

Maelekezo

Utalii

Lugha

Mashirika ya msaada

Mengineyo


Nchi za Afrika Bara la Afrika
Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Eswatini | Ethiopia | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesotho | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Zambia | Zimbabwe
Maeneo ya Afrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika
Hispania: Kanari · Ceuta · Melilla | Italia: Pantelleria · Pelagie | Ufaransa: Mayotte · Réunion | Uingereza: · St. Helena · Diego Garcia | Ureno: Madeira
Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Ethiopia kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.