Haile Selassie

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Haile Selassie wa Ethiopia.

Haile Selassie (kwa Kige'ez: ቀዳማዊ ኃይለ ሥላሴ, qädamawi haylä səllasé, [ˈhaɪlə sɨlˈlase]; 23 Julai 189227 Agosti 1975) alikuwa Kaisari au Negus Negeste wa Ethiopia. Kabla ya kuwa mfalme aliitwa Ras Tafari Makonnen. Jina lake la kifalme lina maana ya "Utukufu wa Utatu (Mtakatifu)". Pia anafahamika kwa jina la Simba wa Yuda, Mfalme wa wafalme.

Alikuwa Mkristo, tena shemasi wa madhehebu ya Kanisa la Kiorthodoksi la Ethiopia.

Maisha

Maisha ya awali

Alizaliwa katika kijiji kiitwacho Ejersa. Baba yake alikuwa kabaila Mwethiopia aliyeitwa Ras Makonnen akawa gavana wa Harar, familia yake ikiwa na watoto 11.

Gavana wa mikoa

Ras Tafari Makonnen alikuwa bado kijana alipopewa cheo cha gavana wa Sidamo mwaka 1907. Mwaka 1911 akarithi nafasi ya gavana wa Harar.

Wakati wa ugomvi kuhusu Negus Mwislamu Lij Iyasu (1913-1916) alisimama awali upande wa mfalme lakini alifaidika zaidi na uasi uliompindua Negus. Makabaila waliomwondoa Iyasu mwaka 1916 walimteua shangazi yake Zauditu, aliyekuwa binti wa Negus Negesti marehemu Menelik II, kuwa malkia, wakaamua pia Ras Tafari awe mwangalizi wake.

Mtawala na Negus Negeste

Kwa njia hiyo Ras Tafari akawa kiongozi muhimu zaidi nchini. Mwaka 1928 Zauditu akampa cheo cha negus chini yake mwenyewe. Baada ya kifo cha Zauditu (1930) Ras Tafari akapokea taji na cheo cha Negus Negeste (au mfalme wa wafalme) wa Ethiopia akajiita Haile Selassie.

Baada ya kupokea taji akafanya ziara Ulaya.

Mwokozi wa Rastafari

Habari zake zikaenea kote duniani zikasababisha kutokea kwa dini mpya ya Rastafari iliyopokea jina kutoka kwake, ingawa mwenyewe alibaki mwamini wa Kanisa la Orthodoksi, akiwa na daraja ya ushemasi. Watu weusi kisiwani Jamaika, waliokuwa wajukuu wa watumwa wenye asili ya Afrika, walisikia kwa mara ya kwanza ya kwamba Mwafrika anaheshimiwa na wafalme wa Ulaya, wakaona yeye ni mwokozi wa Mungu aliyerudi duniani kwa ajili ya watu weusi.

Haile Selassie alifukuzwa katika Ethiopia mwaka 1936 Italia ilipovamia Ethiopia, akarudi 1941 kwa msaada wa Uingereza iliyoondoa Waiitalia nchini katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Sifa na kasoro za utawala wake

Utawala wa Haile Selassie uliingiza Ethiopia katika Chama cha Mataifa ikiwa nchi ya kwanza ya Afrika kujiunga nacho. Baadaye ulimpa nafasi kubwa katika harakati ya uhuru wa Afrika na makao makuu ya Umoja wa Afrika yalijengwa Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia.

Katika siasa ya ndani alishindwa kuendeleza nchi yake. Alikosa nguvu na nia ya kumaliza utawala wa kikabaila nchini uliosababisha umaskini mkali kati ya wakulima waliopaswa kuwaachia wakabaila sehemu ya mazao.

Hivyo kimataifa Haile Selassie aliheshimiwa sana lakini ndani ya nchi maendeleo yalikwama, wanafunzi na wasomi wakikasirikia na wakulima maskini wakifa njaa mara kwa mara.

Mapinduzi ya 1974 na kifo

Njaa kubwa ya miaka 19721973 katika majimbo ya Wollo na Tigray ikafuatwa na mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1974. Kamati ya kijeshi ya Derg ikamkamata tarehe 12 Septemba 1974.

Kifo chake kikatangazwa tarehe 28 Agosti 1975 na haieleweki kama aliuawa au alikufa kutokana na ugonjwa.

Baada ya kuondolewa kwa Derg mabaki ya maiti ya Kaisari yalipatikana mwaka 1992 chini ya sakafu ya choo cha jumba la kifalme alikokamatwa. Tarehe 5 Novemba 2000 mabaki hayo yalipewa mazishi ya kifalme katika kanisa kuu la Kiorthodoksi la Addis Ababa.


Makala hii kuhusu Kaizari fulani wa Uhabeshi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Haile Selassie kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.