Nenda kwa yaliyomo

Thomas Sankara

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Thomas Sankara.

Noël Isidore Thomas Sankara (* 21 Desemba 1949 mjini Yako, Volta ya Juu; † 15 Oktoba 1987 mjini Ouagadougou, Burkina Faso) alikuwa mwanajeshi na mwanasiasa nchini Burkina Faso. Kuanzia 4 Agosti 1983 hadi kuuawa kwake tarehe 15 Oktoba 1987, Sankara alikuwa rais wa tano wa Volta ya Juu aliyoibadilishia jina kuwa Burkina Faso.

Maisha ya Awali

Wikipedia Alizaliwa Desemba 21, 1949, siku ya Jumapili, kijiji cha Yako, nchini Volta ya Juu. Jina lake la kuzaliwa ilikuwa Thomas Noel Isidore Ouedraogo. Babake, Joseph Sankara, alikuwa Msilmi-Mossi. Alijipa jina Ouedraogo alipojiunga na jeshi la Ufaransa wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Joseph alikuwa Muislamu, lakini baada ya kujiunga na jeshi, alibadili dini na akawa Mkatoliki. Mamake Sankara alikuwa anaitwa Marguerite Kinda, na alikuwa Mmossi. Baada ya Thomas Sankara kufika ujana, babake aliibadilisha jina ya familia yao tena na wakarudi kuitwa "Sankara".

Alikuwa mtoto wa tatu na kijana wa kwanza katika familia ya watoto kumi na mmoja. Mmoja wa dada zake waliomfuata alifariki akiwa bado mchanga.

Alipokuwa mdogo, familia yake iliishi mji wa Gaoua, kwani hapo ndipo baba yake alipoajiriwa na jeshi. Shuleni, alifuzu katika masomo ya hisabati, Kifaransa na dini. Kwa kuwa alikuwa mchamungu, makasisi wake walimshauri aende shule ya seminari baada ya kumaliza shule ya msingi. Alikubali, lakini pia alifanya mtihani wa kuingia kidato cha sita na kuipita. Babake alipowajulisha makasisi kwamba Sankara hangekuwa anaenda seminari, bali angejiunga na shule ya upili, walimjibu kwa kusema hakumwombea mwanake kwa kina.

Sankara alijiunga na Shule ya Upili ya Ouezzin Coulibaly iliyokuwa kule Bobo-Dioulasso. Huko, alifanya urafiki na vijana wengi ambao baadaye wangekuwa wandani wake alipokuwa serikalini, kama vile Fidele Toe, ambaye akawa waziri, Soumane Toure, nk. Shuleni, aliendelea kuyapenda masomo ya Hesabu na Kifaransa, pamoja na kuanza kuigiza kwenye michezo.

Mwaka wa 1966, rais wa kwanza wa Volta ya Juu, Maurice Yameogo, aliondolewa kupitia mapinduzi na kamanda wa jeshi, Sangoulee Lamizana, alichukua uongozi. Lamizana akaanzisha chuo cha wanajeshi mjini Ouagadougou, ambacho kilikuwa cha kwanza nchini. Sankara alisikia kwenye redio tangazo kwamba wanafunzi wa kwanza wa chuo hicho watachaguliwa kutoka waliohitimu shule ya upili. Alipohitimu, alikuwa mmoja wa waliochaguliwa. Wakati huo, alikuwa na umri wa miaka 17.

Baada ya miaka mitatu, alimaliza masomo yake kwenye chuo hicho cha uanajeshi, na kutumwa Antsirabe, nchini Madagascar, kusomea cheo cha uafisaa. Huko, alifundishwa na kujifundisha zaidi ya masomo ya kawaida ya uanajeshi. Masomo ya kilimo, unyunyuzi, na maisha ya raia wa kawaida. Aliyapenda sana masomo yake huko hadi akaomba ruhusa ya kukaa huko kwa mwaka mmoja zaidi.

Mwanajeshi na mwanasiasa

Sankara alipanda ngazi ya kijeshi hadi cheo cha kapteni. Pamoja na mwanajeshi mwenzake Blaise Compaore alishiriki katika chama cha siri cha "maafisa Wakomunisti" waliolenga kupambana na ufisadi.

Mwaka 1981 alikuwa waziri wa mambo ya ndani katika serikali ya kijeshi ya rais Jean-Baptiste Ouédraogo na kupandishwa cheo kuwa waziri mkuu kwa miezi michache kuanzia Februari 1983. Mwezi Mei alikamtawa na kutiwa mbaroni. Mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Blaise Compaore yalimfanya kuwa mwenyekiti wa kamati ya mapinduzi na rais wa tano wa Volta ya Juu.

Rais

Sankara alibadilisha jina la nchi kuwa Burkina Faso. Alijulikana hasa kwa amri yake ya kuwa mawaziri na maafisa wote wa serikali yake wasitumie magari makubwa bali gari dogo aina ya Renault 5 ambayo ilikuwa gari la bei ya chini iliyopatikana nchini.

Pamoja na hayo, alishirikisha wanawake wengi katika serikali yake akapiga marufuku tohara kwa wanawake.

Mwisho

Mwaka 1987 alipinduliwa na wanajeshi wenzake na kuuawa. Blaise Compaore akawa rais badala yake.

Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Thomas Sankara kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.