Kiyunani

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Kigiriki cha Kale)

Kiyunani ni jina la Kiswahili cha zamani kwa "Kigiriki", ambayo ni lugha ya nchi ya Ugiriki ("Uyunani") au kwa tabia za Wagiriki ("Wayunani").

Neno la Kiswahili cha zamani limetokana na lugha ya Kiarabu ambapo يونان yunan linataja kiasili Wagiriki wa eneo la Ionia au wa kabila la Waioni walioishi kwenye pwani ya mashariki ya Bahari ya Aegeis.

Leo hii si la kawaida sana, lakini linapatikana bado, hasa katika matoleo mbalimbali ya Biblia. Kwa kuwa kitabu hicho kina miaka 2000-3000 hivi, ni wazi kwamba kinasimulia mambo ya zamani, hivyo pengine neno Kiyunani linatafsiriwa kuwa Kigiriki cha zamani, na Uyunani kuwa Ugiriki ya Kale.

Ni kwamba miaka ya nyuma neno "Kigiriki" limezidi kusambaa zaidi kati ya wanaoongea Kiswahili, kutokana na athira ya Kiingereza kinachotumia maneno "Greece, Greek" kutoka Kilatini "Graeci", ambayo ni kawaida katika lugha nyingi za Kiulaya.

Wanaotajwa wenyewe hujiita "Helleni", na lugha yao "Helleniki".