Pakomi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mt. Pakomi.

Pakomi (Thebe, Luxor, 292 - Pbow 9 Mei 348) alikuwa askari, halafu mmonaki wa Misri, maarufu kwa kuanzisha abasia ya kwanza (320 hivi) na kwa kutunga kanuni ya kwanza ya maisha ya utawa.

Mpaka leo maisha hayo yanafuatwa hasa Ethiopia, lakini athari zake zinaonekana katika umonaki na mashirika mbalimbali ya kitawa, hata katika Kanisa la magharibi.

Anaheshimiwa na Kanisa Katoliki na madhehebu mengine mbalimbali ya Ukristo kama mtakatifu.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe ya kufa kwake[1] au tarehe 15 Mei.

Maisha na karama[hariri | hariri chanzo]

Muda mfupi baada ya maisha ya upwekeni ya Antoni abati, katika nchi ileile, yalianza maisha ya pamoja ambamo mali na vilevile mang’amuzi ya Kiroho yashirikishwe, hata kwa waamini wa ulimwenguni.

Wa kwanza kutunga kanuni kwa watawa ni Pakomi, askari aliyeongokea imani kwa kuona Wakristo waliotumikia wafungwa kwa upendo. Mang’amuzi hayo ya awali yalimuangazia kuwa Mungu ni upendo yakaathiri maisha na mafundisho yake yote.

Hivyo, baada ya kushika kwa miaka 7 umonaki huko Misri Kusini, chini ya Palemon, akajisikia wito wa kuishi na wengine kwa upendo akaanzisha maisha ya pamoja upwekeni. Tena, kwa ombi la dada yake, karibu na monasteri za kiume kulikuwa na nyingine ya kike.

Muundo huo mpya wa umonaki ulitegemea matatu: upweke, mwanzilishi na kanuni. Ndani ya ile aliyoandika jina “ndugu” linashika nafasi ya “mmonaki”.

Mbali ya mafungo na sala ndefu, Pakomi alisisitiza kujikana kwa ajili ya wengine, yaani kuwa na utiifu, huruma na misaada ya kila aina: ndiyo njia ya upendo ambayo iliagizwa na Bwana na kufanya maisha ya pamoja yawe bora kuliko upweke kamili.

Sawa na sala na ibada, milo yote ilikuwa ya pamoja, kama vile mapato ya kazi, zilizopangwa na kiongozi kila asubuhi, yalivyotakiwa kuingia katika mfuko wa jumuia.

Kwa busara yake, Pakomi alipanga hatua za malezi ya awali, akisisitiza kukariri sehemu ndefu ya Biblia pamoja na kufanya kazi kwa mikono.

Kanuni hiyo ikaja kuathiri moja kwa moja maisha ya watawa na kanuni zao mashariki na magharibi vilevile, na ndiyo inayoongoza umati wa wamonaki wa Ethiopia tangu mwaka 500 hivi hadi leo.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Martyrologium Romanum: ex Decreto Sacrosancti oecumenici Concilii Vaticani II instauratum auctoritate Ioannis Pauli P.P. II promulgatum, Romae 2001, ISBN 8820972107

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.