Mengistu Haile Mariam

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Mengistu Haile Mariam (kwa Kiamhara: ሊየተና ኮሎኔል መንግስቱ ኃይለ ማርያም; alizaliwa Addis Ababa, 21 Mei 1937), ni mwanajeshi na mwanasiasa kutoka nchi ya Ethiopia aliyewahi kuwa rais wa Ethiopia hadi kupinduliwa mwaka 1991.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Wazazi wake walitoka [kusini]] mwa Ethiopia (leo: Jimbo la Mataifa ya Kusini).

Baba yake Mengistu, Haile Mariam, alikuwa mtumishi wa kabaila na gavana wa sehemu ya jimbo la Shoa. Mama yake Mengistu alikufa alipokuwa mdogo wa miaka 8 kwa hiyo aliishi kwa bibi yake pamoja na wadogo zake. Baadaye akarudi akaishi pamoja na babake na kuingia jeshini. Alipanda ngazi ya vyeo hadi kuwa meja.

Mwaka 1968 alimwoa Wubanchi Bishaw akazaa naye watoto 3 wanaoitwa Tigist, Andenet na Tilahun.

Mwaka 1991 alikimbia pamoja na familia yake na kuhamia Zimbabwe anapoishi tangu kupewa kimbilio na rais Robert Mugabe.

Mapinduzi ya kijeshi ya 1974[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1974 serikali ya kaisari Haile Selassie ilishindwa kutatua matatizo ya ukame, njaa na mvurugo wa wananchi waliosikitika na serikali. Sehemu za jeshi zilianza kukataa utekelezaji wa amri. Kamati ya maafisa wa ngazi iliundwa Addis Ababa kwa shabaha ya kurudisha utaratibu nchini. Baada ya miezi ya kwanza walipanua kamati yao kwa wawakilishi kutoka kila kikosi cha jeshi na kamati ilijulikana kwa kifupi chake cha "Derg".

Mengistu alitumwa Addis Ababa kama mwakilishi wa kikosi chake. Katika majadiliano ya kamati aliweza kujipatia nafasi muhimu akachaguliwa kuwa makamu wa mwenyekiti. Chini ya uongozi wake mtawala Haile Selassie alikamatwa na kufungwa ndani hadi kifo chake mwaka uliofuata 1975.

Mengistu aliendelea kushika madaraka akahakikisha kuuawa kwa majenerali wa jeshi la Haile Selassie na pia maafisa kadhaa waliompinga ndani ya Derg.

Tangu mwaka 1977 Mengistu aliweza kuua wapinzani wake wote ndani ya jeshi na Derg akatangaziwa kuwa mkuu wa dola.

Kugeukia ukomunisti[hariri | hariri chanzo]

Tangu ziara yake ya Marekani kama meja kabla ya mapinduzi Mengistu alisoma vitabu vya kikomunisti akaendelea kujiona mfuasi wa itikadi ya Marx na Lenin. Hapo alitumia madaraka yake kuelekeza Ethiopia kwenye njia ya kikomunisti.

Kwa kufuata mfano wa Umoja wa Kisovyeti serikali ililenga kusimamia matawi yote ya uchumi na kupanga uzalishaji wa mavuno na bidhaa. Ardhi yote pamoja na makampuni makubwa ya kibiashara yalitaifishwa; wakulima waliwekwa huru na mabwana wao wa awali lakini wakalazimishwa kufanya kazi katika vijiji vya pamoja, hawakupewa ardhi ya binafsi.

Chama cha wafanyakazi wa Ethiopia kilianzishwa mwaka 1984 kikiwa chama pekee kilichoongozwa na kamati kuu. Mengistu alikuwa mwenyekiti wa chama na pia rais wa nchi tangu 10 Septemba 1987. Jina la nchi lilibadilishwa kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Ethiopia.

Matatizo ya utawala[hariri | hariri chanzo]

Katika kipindi cha miaka ya 1980 serikali ya Mengistu iliona matatizo mengi. Sehemu za sababu zilikuwa kimazingira kama ukame; mengine kisiasa kwa sababu mabadiliko ya uchumi yalileta uhaba wa mazao na vifaa. Kutokana na mipango ya uchumi kilimo kilikwama kabisa kwenye mikoa kadhaa. Njaa kubwa ilitokea 1984-1985 iliyokuwa mbaya kuliko ile ya zamani za Kaisari Haile Selassie. Watu walianza kupinga serikali na kuchukua silaha katika sehemu mbalimbali za nchi.

Upinzani wa watu wa Eritrea uliendelea na pia watu wa Tigray walichukua silaha.

Jeshi la Mengistu lilipata misaada mingi kutoka Umoja wa Kisovyeti na nchi nyingine za kikomunisti, hasa Ujerumani ya Mashariki. Hata hivyo, wakati harakati ya ukombozi wa Tigray ilipoungana na vikundi kutoka majimbo mengine na kuunda umoja wa EPRDF, muundo wa ukomunisti ulianza kuporomoka katika nchi za Ulaya na msaada kwa Mengistu kutoka kule ulipungua.

Wapinzani walianza kusogea mbele na mwezi Mei 1991 jeshi lao lilifika mbele ya Addis Ababa. Mengistu aliondoka kwa ndege pamoja na familia yake akapata kimbilio nchini Zimbabwe kama mgeni wa rais Robert Mugabe.

Kuhukumiwa kama mwuaji[hariri | hariri chanzo]

Serikali mpya ya EPRDF ilifungua kesi dhidi ya Mengistu baada ya kuondoka kwake nchini. Alihukumiwa kwa kuhusika katika kifo cha watu 2,000. Mashtaka dhidi yake yalijaza kurasa 8.000. Zilionyesha amri zilizotiwa saini naye mwenyewe kwa kuua watu, pia video ya mateso ya wafungwa na ushuhuda wa mashahidi.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Marejeo mengine[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikiquote ina mkusanyiko wa dondoo kuhusu:
Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mengistu Haile Mariam kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.