Yohane Hus

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jan Hus.
Kuchomwa kwa Hus akiwa hai; kutoka kitabu cha Tarihi ya Spiez, mnamo 1485.jpg

Yohane Hus (Husinec (Bohemia) 1371 hivi - Konstanz (Ujerumani) 6 Julai 1415) alikuwa padri na mwanateolojia wa Ukristo ambaye alilenga urekebisho wa Kanisa Katoliki kwa kufuata mafundisho ya John Wyclif.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Padri Yohane Hus alikuwa mwalimu wa teolojia kwenye Chuo Kikuu. Mwaka 1412 alihubiri kwa nguvu sana kule Praha (leo mji mkuu wa Ucheki), akafundisha ya kwamba mamlaka kuu Kanisani ni katika Biblia si katika maamuzi ya maaskofu au Papa.

Mwaka 1411 maaskofu wakamtangaza kuwa mzushi akatengwa na Kanisa. Alishtakiwa mbele ya mfalme lakini wengi walimfuata. Akahifadhiwa na kufichwa na kabaila katika boma lake.

Miaka 1414-1418 kulikuwa na Mtaguso mkuu wa Kanisa Katoliki kule Konstanz, Ujerumani. Hus akaitwa kujitetea mbele ya mkutano huo, akaahidiwa ulinzi wa mfalme, yaani kwamba ataweza kurudi tena hata akionekana kuwa mzushi. Lakini kinyume cha ahadi alikamatwa akahukumiwa kuwa mwasi na mzushi, akachomwa moto akiwa hai.

Urithi[hariri | hariri chanzo]

Wafuasi wake katika mikoa ya Bohemia na Moravia (leo Ucheki) wakasikitika mno. Wengine wakachukua silaha wakataka kutenga nchi yao kutoka uongozi wa Kanisa.

Vita vya miaka mingi vilianza kati ya Wahus na askari wa mfalme na maaskofu. Alama ya Wahus ilikuwa kikombe cha Ekaristi kwani Hus alifundisha ya kwamba Wakristo wote wanapaswa kupokea kikombe kanisani (katika karne XII Kanisa Katoliki lilianza desturi ya kutoa kikombe kwa mapadri tu).

Mwishoni Ukristo wa Bohemia na Moravia uligawanyika. Wahus wakali waliojaribu kuunda utaratibu wa kisiasa juu ya mahubiri ya Yesu na kuwalazimisha wote kuufuata kwa silaha wakashindwa. Wengine wakafuata Wahus wasio wakali waliopatana na wakubwa wa nchi. Wengine wakabaki ndani ya Kanisa Katoliki, wakaruhusiwa kuwa na ibada ya Misa (chakula cha Bwana) wakipokea sakramenti katika maumbo ya mkate na divai.

Mwaka 1457 kikundi kidogo cha wafuasi wa Hus waliochoka uuaji na vita vya kidini walianzisha jumuiya ya Kikristo iliyoitwa "Umoja wa Ndugu", wakajaribu kuishi kama ndugu wakikaa pamoja, kufanya kazi na kusali pamoja. Mwanzoni hawakupokea matajiri waliotaka kujiunga nao.

Mbinu hii ilifanana na watawa aina ya Wafransisko lakini walikuwa jumuiya ya watu wenye ndoa na watoto. Waliona muhimu wasiwe na taratibu za utawala katika Kanisa, lakini viongozi wawe kama ndugu na watumishi wa wengine. Hawakutaka kumlazimisha yeyote katika mambo ya imani kama ilivyokuwa katika maeneo ya Wakatoliki na ya Wahus wengine.

Mwanzoni walihudumiwa kiroho na mapadri wa Kanisa Katoliki, lakini mwaka 1467 waliamua kuchagua watumishi wao wenyewe, wakiwemo mpaka leo mashemasi, makasisi na maaskofu. Umoja huo ulienea Bohemia na Moravia ukawa chanzo cha madhehebu ambayo yalistawi upya kuanzia mwaka 1722 na yanaitwa ya "Wamoravia" (leo wengi wao wanaishi nchini Tanzania).

Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.