Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania | |
---|---|
Kaulimbiu ya taifa: "Uhuru na Umoja" | |
Wimbo wa taifa: "Mungu ibariki Afrika" | |
Mahali pa Tanzania katika Afrika ya Mashariki | |
Ramani ya Tanzania | |
Mji mkuu | Dodoma |
Mji mkubwa nchini | Dar es Salaam |
Lugha rasmi | |
Lugha za taifa | Kiswahili |
Makabila | Kupita makabila 125 |
Dini (asilimia) | 63.1 Wakristo 34.1 Waislamu 1.5 Wakanamungu 1.2 dini asilia 0.1 wengine |
Serikali | Jamhuri |
• Rais • Makumu wa Rais • Waziri Mkuu • Spika • Jaji Mkuu | Samia Suluhu Hassan Philip Isdor Mpango Kassim Majaliwa Tulia Ackson Ibrahim Hamis Juma |
Uhuru kutoka Ufalme wa Muungano | 9 Desemba 1961 (Tanganyika) 10 Desemba 1963 (Zanzibar) |
Eneo | |
• Eneo la jumla | km2 947 303[1] |
• Maji (asilimia) | 6.4[1] |
Idadi ya watu | |
• Kadirio la 2023 | 65 642 682[1] |
• Sensa ya 2022 | 61 741 120[2] |
Pato la taifa | Kadirio la 2023 |
• Jumla | USD bilioni 84.033[3] |
• Kwa kila mtu | USD 1 326[3] |
Pato halisi la taifa | Kadirio la 2023 |
• Jumla | USD bilioni 227.725[3] |
• Kwa kila mtu | USD 3 595[3] |
Maendeleo (2021) | 0.549[4] - duni |
Sarafu | Shilingi ya Tanzania |
Majira ya saa | UTC+3 (Afrika Mashariki) |
Muundo wa tarehe | siku/mwezi/mwaka |
Upande wa magari | Kushoto |
Msimbo wa simu | +255 |
Msimbo wa ISO 3166 | TZ |
Jina la kikoa | .tz |
Tanzania (jina rasmi: Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) ni nchi iliyoko Afrika ya Mashariki, ndani ya ukanda wa maziwa makuu ya Afrika. Imepakana na Uganda na Kenya upande wa kaskazini, Bahari Hindi upande wa mashariki, Msumbiji, Malawi na Zambia upande wa kusini, Kongo, Burundi na Rwanda upande wa magharibi.
Eneo lina kilometa za mraba 947,303 (nchi ya 31 duniani); maji ya ndani yanachukua asilimia 6.2. Mlima Kilimanjaro, mlima mrefu zaidi barani Afrika, upo kaskazini-mashariki mwa Tanzania.
Idadi ya watu kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 ilikuwa 61,741,120[5], (nchi ya 24 duniani) kutoka 44,928,923 waliohesabiwa katika sensa ya mwaka 2012, likiwa ongezeko la 3.2% kwa mwaka.
Msongamano ni wa watu 47.5 kwa km² (nchi ya 124 duniani).
Mji mkuu ni Dodoma (wenye wakazi 765,179), lakini Dar es Salaam ndilo jiji kubwa zaidi, lenye watu 5,383,728.
Miji mingine ni kama vile Mwanza (1,004,521), Arusha (616,631), Mbeya (541,603), Morogoro (471,409), Kahama (453,654), Tanga (393,429), Geita (361,671), Tabora (308,741) na Sumbawanga (303,986).[6]
Jina
Jina "Tanzania" liliundwa kama mkusanyiko wa majina ya maeneo mawili yaliyoungana kuunda nchi: Tanganyika na Zanzibar.[7] Jina lilipatikana kwa mashindano yaliyotangazwa mwaka 1964 na serikali kutafuta jina fupi zaidi kuliko "Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar".
Mshindi alikuwa mwenyeji wa Dar es Salaam aliyeitwa Mohamed Iqbal Dar[8]. Alipendekeza kuunganisha herufi tatu za kwanza za TANganyika na ZANzibar akafikia "Tanzan". Hakuridhika bado, akaona nchi nyingi za Afrika zina majina yanayoishia na "ia" akaongeza herufi hizi. Mwenyewe alieleza baadaye chaguo lake kwamba aliamua kutumia "I" ya jina lake Iqbal na "A" ya jina la dhehebu lake analolifuata katika Uislamu la Ahmadiyya.[9]
Jina "Tanganyika" linatokana na maneno ya Kiswahili "tanga" na "nyika", yakiunda msemo "tanga nyikani". Wakati fulani inaelezwa kama marejeleo ya Ziwa Tanganyika. [10] Jina la Zanzibar linatokana na "zenji", jina la watu wa eneo hilo (inadaiwa lina maana ya "nyeusi"), na neno la Kiarabu "barr", ambalo linamaanisha pwani au ufukwe.[11]
Historia
(Kuhusu historia ya maeneo ya Tanzania kabla ya 1964 angalia makala za Tanganyika, Zanzibar na Afrika ya Mashariki ya Kijerumani)
Kabla ya uhuru nchi zote mbili, Tanganyika na Zanzibar, zilikuwa chini ya utawala wa Uingereza lakini hazikuwa makoloni ya kawaida.
Zanzibar ilikuwa na hali ya nchi lindwa kutokana na mikataba kati ya masultani wa Zanzibar na Ufalme wa Muungano (Uingereza).
Tanganyika iliwahi kuwa sehemu ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani hadi Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia halafu ikawa chini ya Uingereza kama eneo la kudhaminiwa kutokana na azimio la Shirikisho la Mataifa lililoweka Tanganyika katika ngazi "B" ya maeneo ya kudhaminiwa.
Tanganyika na Zanzibar zilikuwa nchi mbili tofauti hadi 1964, zilipoungana na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hapo kiongozi wa Tanganyika Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipata kuwa Rais wa kwanza na kiongozi wa mapinduzi ya Zanzibar Abedi Amani Karume akawa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Tanzania, chini ya Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi (1985–1995) iliruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa Tanzania na kuanza mpango wa kurekebisha uchumi kuendana na masharti ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani.
Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa (1995–2005) aliendeleza mfumo wa uchumi wa soko huria ambapo mashirika ya umma yalibinafsishwa.
Tarehe 21 Desemba 2005 Jakaya Kikwete aliapishwa kuwa Rais wa nne wa taifa (2005–2015), naye aliendeleza sera za watangulizi wake akitokea chama hichohicho cha CCM.
Tarehe 5 Novemba 2015 aliapishwa Rais wa awamu ya tano, John Magufuli (wa CCM vilevile).
Kufuatana na kifo chake tarehe 17 Machi 2021, makamu wake, Samia Suluhu Hassan, aliapishwa kuwa Rais wa awamu ya sita.
Jiografia
Ikiwa na eneo la kilomita za mraba 947,303 (365,756 sq mi), Tanzania ni nchi ya 13 kwa ukubwa barani Afrika na ya 31 kwa ukubwa duniani.[12] Inapakana na Kenya na Uganda upande wa kaskazini; Rwanda, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo upande wa magharibi; na Zambia, Malawi, na Msumbiji upande wa kusini.
Tanzania iko kwenye pwani ya mashariki ya Afrika na ina ufuo wa Bahari ya Hindi takriban kilomita 424 (885 mi).[13] Pia inajumuisha visiwa kadhaa vya pwani, vikiwemo Unguja (Zanzibar), Pemba, na Mafia. Tanzania ni nchi yenye sehemu za juu na za chini kabisa barani Afrika: Mlima Kilimanjaro, wenye urefu wa mita 5,895 (futi 19,341) juu ya usawa wa bahari, na kina cha Ziwa Tanganyika, katika mita 1,471 (futi 4,826) chini ya usawa wa bahari kwa mtiririko huo.
Tanzania ina milima na misitu minene kaskazini-mashariki, ambako kuna Mlima Kilimanjaro. Nchi iko katika eneo la Maziwa makubwa ya Afrika, hivyo maziwa yanafunika km2 61,500, yaani 6% za eneo lote la nchi. Upande wa kaskazini na magharibi kuna Ziwa Victoria, ziwa kubwa zaidi barani Afrika, na Ziwa Tanganyika, ziwa lenye kina kirefu zaidi barani humo, linalojulikana kwa aina yake ya kipekee ya samaki. Upande wa kusini magharibi kuna Ziwa Nyasa. Eneo la katikati mwa Tanzania ni uwanda mkubwa, wenye tambarare na ardhi ya kilimo. Ukanda wa mashariki una joto na unyevunyevu, huku Visiwa vya Zanzibar vikiwa karibu. Maporomoko ya maji ya Kalambo katika mkoa wa kusini-magharibi mwa Rukwa ni maporomoko ya pili kwa urefu barani Afrika, na yanapatikana karibu na ufuo wa kusini-mashariki wa Ziwa Tanganyika kwenye mpaka na Zambia. [14] Eneo la Hifadhi ya Menai Bay visiwani Zanzibar ndilo eneo kubwa zaidi la bahari lililohifadhiwa.
Hali ya hewa
Hali ya hewa inatofautiana sana ndani ya Tanzania. Katika nyanda za juu, halijoto huanzia 10 hadi 20 °C (50 na 68 °F) wakati wa msimu wa baridi na joto kwa mtiririko huo.
Tanzania hupata majira ya joto katika miezi ya Desemba, Januari na Februari (25–31 °C au 77.0–87.8 °F) huku kipindi cha baridi zaidi kikitokea kati ya Mei na Agosti (15–20 °C au 59–68 °F). Halijoto ya kila mwaka ni 20 °C (68.0 °F).
Hali ya hewa ni baridi katika maeneo ya milima mirefu. Tanzania ina vipindi viwili vikuu vya mvua: mvua za vuli hunyesha katika miezi ya Oktoba, Novemba na Desemba na mvua za masika hunyesha katika miezi ya Machi, Aprili na Mei ingawa zipo tofauti ndogo kati ya sehemu mbalimbali.[15] Kiasi cha mvua na halijoto husababisha tofauti za aina ya uoto wa asili, udongo na aina ya mazao yanayolimwa.
Mabadiliko ya hali ya hewa nchini Tanzania yanasababisha kuongezeka kwa joto na uwezekano mkubwa wa matukio ya mvua kubwa (kusababisha mafuriko) na vipindi vya ukame.[16][17] Mabadiliko ya hali ya hewa tayari yanaathiri sekta za kilimo, rasilimali za maji, afya na nishati nchini Tanzania. Kupanda kwa kina cha bahari na mabadiliko ya ubora wa maji kunatarajiwa kuathiri uvuvi na ufugaji wa samaki.[18]
Tanzania ilitoa Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NAPAs) mwaka 2007 kama ilivyoagizwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi. Mwaka 2012, Tanzania ilitoa Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi ili kukabiliana na wasiwasi unaoongezeka wa athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi katika mazingira ya kijamii na kiuchumi.[19]
Wanyamapori na Hifadhi
Tanzania ina takriban 20% ya spishi za wanyama wengi wa Afrika wenye damu moto, wanapatikana kwenye mbuga zake za Taifa, hifadhi na bahari. Hifadhi za Taifa na mbuga za wanyama zimeenea katika eneo la zaidi ya kilomita za mraba 42,000 (sq. mi 16,000) na kuunda karibu 38% ya eneo la nchi.[20][21] Tanzania ina mbuga 21 za taifa, pamoja na hifadhi mbalimbali za wanyamapori na misitu, ikijumuisha Hifadhi ya Ngorongoro. Magharibi mwa Tanzania, Hifadhi ya Taifa ya Gombe ni kitovu ya uchunguzi unaoendelea wa Jane Goodall wa tabia ya sokwe, ambao ulianza mwaka wa 1960.[22][23]
Tanzania ina bioanuwai nyingi na ina aina mbalimbali za makazi ya wanyama.[24] Katika uwanda wa Serengeti nchini Tanzania, nyumbu (Connochaetes taurinus mearnsi), "bovids" wengine na pundamilia[25] hushiriki katika uhamaji mkubwa wa kila mwaka. Tanzania ni nyumbani kwa takriban spishi 130 za amfibia na zaidi ya spishi 275 za wanyama watambaao, wengi wao wanapatikana Tanzania tu na wamejumuishwa katika orodha ya International Union for Conservation of Nature.[26] Tanzania ina idadi kubwa ya simba duniani.[27]
Tanzania ilikuwa na alama 7.13/10 kwenye Forest Landscape Integrity Index mwaka 2019, ilishika nafasi ya 54 duniani kati ya nchi 172.[28]
Miundo ya muungano
Tangu muungano wa Tanganyika na Zanzibar kufanyika mwaka 1964 Tanzania imekuwa na miundo ifuatayo:
- Nchi inatawaliwa na serikali ya muungano ikitekeleza sheria zinazotolewa na bunge la Tanzania.
- Tanganyika au Tanzania bara haina serikali wala bunge la pekee.
- Zanzibar (visiwa vya Unguja na Pemba) ina serikali na bunge lake vinavyoratibu mambo yasiyo ya muungano.
Mambo yafuatayo yamekubalika kuwa shughuli za muungano:
- Mambo ya nje
- Jeshi
- Polisi
- Mamlaka ya dharura
- Uraia
- Uhamiaji
- Biashara ya nje
- Utumishi wa umma
- Kodi ya mapato, forodha
- Bandari, Usafiri wa anga, Posta na Simu
Utawala
- Muundo wa uongozi na utawala katika kipindi cha ukoloni ulizingatia mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mitatu ya dola yaani serikali, bunge na mahakama.
Tangu uhuru, mgawanyo wa madaraka na uhusiano miongoni mwa mihimili hiyo uliimarishwa kwa kuzingatia wakati, mahitaji ya demokrasia na misingi ya utawala bora na umeainishwa pia katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 4 (1).
Kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi pia kulikuwa hatua ya kuendelea kuimarisha utawala wa ushiriki wa wananchi kadiri mahitaji ya upanuzi wa maono na falsafa duniani.
Ugatuzi, yaani mgawanyo wa kiutawala, unafuata Katiba ya nchi I 2.2. Tanzania imegawiwa kwa mikoa 31. Kila mkoa huwa na wilaya ndani yake. Jumla ya wilaya ni 169, ambazo kati yake 34 ni miji.
Ndani ya wilaya kuna ngazi za tarafa na kata.
Chini ya kata kuna vijiji na wakati mwingine ngazi ya chini tena ambayo ni vitongoji.
Watu
Watu wa Tanzania hawaenei sawasawa. Katika maeneo makavu sana, kwa wastani kuna mtu mmoja tu kwa kilomita ya mraba (1/km²), lakini sehemu zenye rutuba za bara, kuna watu 51 kwa kila kilomita ya mraba. Hatimaye huku Unguja kuna watu 134 kwa kilomita ya mraba na katika Mkoa wa Dar es Salaam ni 3,133 kwa kilomita ya mraba.
Asilimia 70 hivi huishi vijijini, ingawa uhamiaji mijini unakwenda kasi.[29]
Makabila
Jamii nyingi za watu zimeishi na kushirikiana katika eneo la Tanzania bara kwa milenia nyingi.
Kati ya jamii hizo, nyingi zilikuja kutoka maeneo mengine ya Afrika.
Nyingi katika jamii zilizohamia sehemu hii ziliingia katika makundi madogomadogo kwa amani, ingawa ziko zilizoingia kwa njia ya uvamizi na vita. Baadhi ya jamii zilizovamiwa zilijihami na kuwazuia wahamiaji wasiendelee kuteka maeneo mengine.
Kufikia mwaka 1884, wakati Wajerumani walipoanza harakati za kufanya sehemu hii ya Afrika kuwa koloni lao, kulikuwa na makabila zaidi ya 120 katika eneo la Tanzania bara.
Kuna makabila 125 hivi. Makabila yenye watu zaidi ya milioni moja ni Wasukuma, Wanyamwezi, Wachaga, Waha, Wagogo, Wahaya, Wajaluo na Wamakonde.
Jambo la pekee kuhusu jamii zilizoishi na zinazoendelea kuishi Tanzania ni kwamba wakazi asili wanawakilisha makundi yote makuu manne ya lugha barani Afrika.[30]
1. Idadi kubwa sana ya Watanzania ni wa jamii ya Wabantu (k.m. Wazaramo, Wapare na Wapogoro).
2. Nje ya hao, kuna Waniloti, kwa mfano Wamasai na Wajaluo ambao wengi wao zaidi wanaishi Kenya.
3. Kundi lingine ni makabila ya Wakushi wanaoishi kaskazini mwa Tanzania; hao ni makabila ya Wairaqw, Wafiome, Wasi na Waburunge.
4. Kuna kundi la Wakhoisan wanaofanana na makabila ya Botswana na Namibia; wanaitwa Wasandawe .
Hatimaye kuna Wahadzabe wachache ambao utafiti wa DNA umeonyesha hivi karibuni wana uhusiano wa asili na Watwa wa nchi za Afrika ya Kati.
Pia kuna asilimia ndogo ya watu wenye asili ya nje ya bara la Afrika, kwa mfano Wahindi, Waarabu, Waindochina, Wafarsi, Wachina, Wagiriki na Waingereza. Hii ilisababishwa na karne za mchanganyiko wa mahitaji ya biashara yaliyofanywa na mabara ya Ulaya na Asia hapo Afrika.
Lugha
Nchini Tanzania kuna lugha za kikabila zaidi ya mia moja na ishirini, kwa kuwa kila kabila lina lugha yake.
Kiswahili ndiyo lugha ya taifa na inazidi kuwa lugha mama[31] kwa watoto wengi, hasa mijini.[32] Walau asilimia 90 za wakazi wanakitumia walau kama lugha ya pili. Kiswahili ni mojawapo kati ya lugha za Kibantu: hii imesaidia sana kukubaliwa kwa Kiswahili nchini, kwa sababu idadi kubwa ya Watanzania ni wasemaji wa lugha za Kibantu. Kiswahili kinatumika kama lugha baina ya watu wa makabila mbalimbali na kwa mambo rasmi; kwa hiyo ni lugha rasmi ya dhati.
Baada ya uhuru, Kiingereza (iliyokuwa lugha ya kikoloni kabla ya uhuru) iliendelea kutumika kwa mambo kadhaa rasmi na kwa elimu kuanzia sekondari ingawa sera mpya inataka Kiswahili kishike nafasi yake hadi chuo kikuu;[33] kwa hiyo ilichukuliwa kama lugha rasmi ya dhati pamoja na Kiswahili. Lakini utumizi rasmi wa Kiingereza umepungua katika milongo iliyopita, na sasa utumizi huu karibu umekwisha. Kwa hiyo siku hizi ni kawaida zaidi kuchukulia Kiswahili kama lugha rasmi ya dhati pekee.
Sera mpya ya elimu inakusudia kufanya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika ngazi zote kufikia mwaka 2024.
Dini
Nchi haina dini rasmi na katiba ya Tanzania inatangaza uhuru wa dini kwa wote. Mara nyingi idadi ya wafuasi wa dini hutajwa kuwa theluthi moja Waislamu, theluthi moja Wakristo na theluthi moja wafuasi wa dini za jadi. Lakini tangu uhuru swali la dini ya wananchi halijaulizwa tena katika sensa, kwa hiyo kadirio la theluthi-theluthi inawezekana ni zaidi azimio la kisiasa.
Kwenye funguvisiwa la Zanzibar idadi ya Waislamu huaminiwa kuwa takriban 97%.
Usafiri
Usafiri nchini Tanzania ni hasa kwa njia ya barabara. Nyingine ni reli na ndege. Kwenye maziwa makubwa na pwani ya Bahari Hindi kuna pia usafiri wa meli.
Hadi sasa idadi ya barabara za lami si kubwa. Kuna hasa njia nzuri kati ya Dar es Salaam, Mbeya katika kusini-magharibi, Dodoma katika kitovu cha nchi, Arusha / Tanga katika kaskazini-mashariki. Kusini-Mashariki na Magharibi ya nchi kwa jumla haina barabara nzuri na mawasiliano ni magumu.
Mashirika mawili ya reli yanayohudumia Tanzania: ni TRC (Shirika ya Reli Tanzania - Tanzania Railways Corporation) na TAZARA (Tanzania-Zambia Railways Corporation). TRC imetawala reli ya kati kuanzia Dar es Salaam hadi Kigoma halafu reli ya Tanga kati ya Tanga na Arusha. Tazara imeunganisha Dar es Salaam na kusini ya nchi hadi Zambia. Zote hazikutunzwa vizuri na usafiri unakumbwa na huduma mbaya pamoja na ajali.
Huduma kwa ndege zinatumia hasa viwanja vya ndege 11 vyenye barabara ya lami kwa ajili ya ndege, hasa Julius Nyerere/Dar es Salaam, Kilimanjaro/Arusha-Moshi na Zanzibar-Kisauni. Pia kuna viwanja vingine vya ndege kama vile uwanja wa ndege wa Mwanza, Bukoba na Kigoma.
Usafiri wa majini pia unafanyika hasa katika bahari ya Hindi, ingawa hakuna meli ya serikali hapo na mashirika binafsi hutoa huduma. Usafiri wa majini hufanyika pia katika maziwa ya Viktoria, Tanganyika na Nyasa. Miongoni mwa meli ni MV Bukoba iliyozama tarehe 21 Mei 1996 pamoja na abiria karibu 1,000 na MV Nyerere iliyozama tarehe 20 Septemba 2018 pamoja na abiria zaidi ya 200.
Katika ziwa Tanganyika ipo meli ya Mv Liemba ambayo ilianza kutumika tangia kipindi cha ukoloni wa Wajerumani: inatoa huduma kati ya miji ya mwambao wa ziwa Tanganyika na nchi jirani.
Mwaka 2017 ulianza ujenzi wa awamu ya kwanza ya njia ya geji sanifu nchini Tanzania inayolenga kuunganisha Dar es Salaam na Morogoro.[34] Njia hii inatarajiwa kuendelea hadi Mwanza na hatimaye hadi Burundi.
Urithi wa Dunia
Mahali pafuatapo katika Tanzania pamepokewa katika orodha ya UNESCO ya "Urithi wa Dunia" (mwaka wa kukubaliwa – jina la mahali)
- 1979 – Hifadhi ya Taifa Ngorongoro.
- 1981 – Hifadhi ya Serengeti.
- 1981 – Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.
- 1982 – Hifadhi ya Taifa Selous.
- 1987 – Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro.
- 2000 – Mji Mkongwe wa Jiji la Zanzibar / Unguja.
- 2006 – Michoro ya Kondoa.
Utamaduni na Sanaa
Muziki
Kuna aina zaidi ya tano za muziki nchini Tanzania, kama zilivyofafanuliwa na BASATA ni pamoja na ngoma (ngoma za asili), dansi, kwaya (muziki wa injili), taarab, na bongo flava (pop/hip hop).[35][36] Ngoma ni muziki wa dansi wa kitamaduni, ngoma hutofautiana kati ya kabila na kabila.[37][38] Dansi ni muziki wa bendi unatokana na muziki wa soukous kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (au "rumba ya kikongo").[39][40] Taarab ni muziki wa Waafrika wa pwani uliopokea athira kutoka tamaduni nyingi, hasa muziki wa Waarabu na Wahindi. Kimsingi ni uimbaji wa mashairi unaofuata muziki wa bendi.[41] Kwaya ni muziki ambao asili yake ni kanisani. Bongo flava ni muziki wa pop wa Tanzania uliozaliwa na muziki wa kizazi kipya, unajumuisha reggae, RnB, na hip hop, uliochanganywa na vionjo vya asili (flava) lakini tangu wakati huo umekua na kuwa muziki wa kipekee wa maeneo ya Maziwa Makuu.[42] Asili mbalimbali za ushawishi zimesaidia kufanya bongo flava kuwa muziki maarufu zaidi Afrika Mashariki, na muziki mmojawapo kati ya ile maarufu zaidi katika bara la Afrika.[43][44]
Tangu kuundwa kwa Tanzania hadi 1993, kurekodi na usambazaji wote wa muziki ulisimamiwa kikamilifu na BASATA, hasa kupitia Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD).[45] Ni aina 4 tu za muziki za Kitanzania zilizoruhusiwa kurekodiwa au kutangazwa, ambazo wakati huo zilikuwa ngoma, taarab, kwaya na dansi. Sheria ya Huduma za Utangazaji ya 1993 iliruhusu mitandao ya kibinafsi ya matangazo na studio za kurekodi.[46] Haya ni mojawapo ya mabadiliko muhimu zaidi katika tasnia ya muziki ya Tanzania tangu kuanzishwa kwa nchi miaka 30 kabla.[47] Miaka michache kabla ya Act ya 1993, muziki wa hip hop ulikuwa umeanza kuimarika katika miji ya Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na Mwanza. Ilikuwa ikianza mageuzi kutoka kwenye hip hop ya Kiingereza huko Uzunguni, maeneo tajiri kama Oysterbay na Masaki pamoja na shule za kimataifa, hadi kizazi kipya Uswahilini, vitongoji maskini na kutumia Kiswahili.[48] Mara tu baada ya kufunguliwa kwa mawimbi ya redio, bongo flava ilizaliwa ikienea kwa haraka kote nchini, na katika Maziwa Makuu.[49]
Fasihi
Utamaduni wa kifasihi wa Tanzania kimsingi ni wa simulizi.[50]: 68 Tanzu na vipera maaarufu vya fasihi simulizi ni pamoja na ngano, mashairi, mafumbo, methali na nyimbo.[50]: 69 Sehemu kubwa zaidi ya fasihi simulizi iliyorekodiwa Tanzania ni ya Kiswahili, ingawa lugha za makabila ya Tanzania zina mapokeo yake ya simulizi. Fasihi simulizi ya nchi imekuwa ikipungua kwa sababu ya mabadiliko ya muundo wa jamii, na kufanya uwasilishaji wa fasihi simulizi kuwa mgumu zaidi, pia teknolojia za kisasa zinachangia kushushwa kwa thamani ya fasihi simulizi.[50]: 68–9
Utamaduni wa kuandika na kusoma vitabu umeenea nchini Tanzania. Fasihi andishi nyingi za Kitanzania ni za Kiswahili au Kiingereza.[50] : 75 Watu mashuhuri katika fasihi andishi ya Tanzania ni pamoja na Shaaban Robert (anatambulika kama baba wa fasihi ya Kiswahili), Muhammed Saley Farsy, Faraji Katalambulla, Adam Shafi Adam, Muhammed Said Abdalla, Said Ahmed Mohammed Khamis, Mohamed Suleiman Mohamed, Euphrase Kezilahabi, Gabriel Ruhumbika, Ebrahim Hussein, May Materru Balisidya, Fadhy Mtanga, Abdulrazak Gurnah, na Penina O. Mlama.[50]: 76–8
Uchoraji na Uchongaji
Mitindo miwili ya sanaa ya Tanzania imepata kutambuliwa kimataifa.[51] Uchoraji wa Tingatinga umejulikana tangu miaka ya 1970. Mtindo huo umepewa jina la mwanzilishi wake, mchoraji wa Kitanzania Edward Said Tingatinga. Kwa ujumla michoro ya Tingatinga inayoonyesha watu, wanyama, au maisha ya kila siku.[50]: 13 [51]
Baada ya kifo cha Tingatinga mwaka wa 1972, wasanii wengine walikubali na kuendeleza mtindo wake, na aina hiyo sasa ndiyo mtindo muhimu zaidi unaolenga utalii katika maeneo ya Afrika Mashariki.[50]: 113 [51]
Uchongaji wa mabombwe ya Kimakonde yamesifiwa tangu mwanzo wa karne ya 20. Wamakonde wengi wamehamia Dar es salaam au Arusha wanapohudumia soko la watalii na soko la nje.
Michezo
Mchezo maarufu nchini Tanzania ni mpira wa miguu. Ingawa mpira wa miguu (kandanda) unaongoza kwa ufuasi mkubwa miongoni mwa vijana, michezo mingine kama vile mpira wa kikapu, mchezo wa ngumi na riadha inazidi kuwa maarufu miongoni mwa watu.[52][53] Baraza la Michezo la Taifa ndicho chombo kinachosimamia michezo nchini chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni.[54]
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni chombo kinachosimamia mpira wa miguu nchini.[55] Vilabu maarufu vya soka la kulipwa jijini Dar es Salaam ni Young Africans F.C. na Simba S.C. Wachezaji wa kandanda ambao wamechezea klabu kubwa za kigeni ni pamoja na Mbwana Samatta, Kelvin John, na Morice Abraham. Tanzania iliandaa Kombe la Mataifa ya Afrika U-17 2019.[56]
Soka la wanawake ni mchezo unaokuwa kwa kasi zaidi Tanzania. Utamaduni wa wanawake kucheza mpira wa miguu umeanza kueleweka kwa wengie. Timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania, Taifa Queens ni bingwa wa Michuano ya CECAFA kwa Wanawake kwa mwaka 2016 na mwaka 2018.[57][58] Michuano hii huandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA). Timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 17 'Serengeti Girls' ilifuzu kucheza Michuano ya Kombe la Dunia la Wanawake nchini India mwaka 2022.[59]
Hasheem Thabeet ni Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA).[60]Mwanariadha wa zamani wa Tanzania wa mbio za kati, Filbert Bayi Sanka[61] mwaka 1974 aliboresha rekodi ya mbio ya mita 1500, na mwaka wa 1975 aliboresha rekodi ya mbio ya maili moja.[62][63] Bado anashikilia rekodi ya Michezo ya Jumuiya ya Madola ya mita 1500.
Filamu
Tanzania ina tasnia maarufu ya filamu inayojulikana kwa jina la "Bongo Movie".[64] Studio nyingi za utayarishaji filamu za Kitanzania ziko Dar es Salaam.
Kabla ya uhuru wa Tanzania mwaka 1961, baadhi ya sinema za kigeni zilirekodiwa Tanganyika na Zanzibar. Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar huandaa maonyesho ya filamu, warsha, muziki pamoja na sanaa zingine za maigizo.[65]
Tazama pia
- Orodha ya Mawaziri Wakuu wa Tanzania
- Orodha ya Mawaziri Wakuu wa Zanzibar
- Orodha ya Magavana Wakuu wa Tanganyika
- Orodha ya Masultan wa Zanzibar
- Orodha ya watu maarufu wa Tanzania
- Orodha ya mikoa ya Tanzania kwa eneo
- Orodha ya mikoa ya Tanzania na Pato la Taifa
- Orodha ya mikoa ya Tanzania na Maendeleo
- Utawala wa Kijiji - Tanzania
- Orodha ya nchi kufuatana na wakazi
- Orodha ya nchi za Afrika kulingana na idadi ya watu
- Orodha ya nchi za Afrika kulingana na msongamano wa watu
- Orodha ya nchi za Afrika kulingana na pato la taifa
- Demografia ya Afrika
Marejeo
- ↑ 1.0 1.1 1.2 "Tanzania". The World Factbook (kwa Kiingereza) (tol. la 2024). Shirika la Ujasusi la Marekani. Iliwekwa mnamo 30 Machi 2024.
- ↑ "Idadi ya watu nchini Tanzania". Tanzania National Bureau of Statistics. Iliwekwa mnamo 1 Aprili 2024.
- ↑ 3.0 3.1 3.2 3.3 "World Economic Outlook Database, October 2023 Edition. (Tanzania)". IMF.org. International Monetary Fund. 10 Octoba 2023. Iliwekwa mnamo 14 Octoba 2023.
{{cite web}}
: Check date values in:|access-date=
na|date=
(help) - ↑ "Human Development Report 2023/24" (kwa Kiingereza). Mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa. 13 Machi 2024. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 19 Machi 2024. Iliwekwa mnamo 22 Machi 2023.
- ↑ https://assengaonline.com/2022/11/05/matokeo-ya-sensa-2022-tanzania/
- ↑ Administrative Units Population Distribution Report - National Bureau of Statistics: https://www.nbs.go.tz
- ↑ "tanzania | Etymology, origin and meaning of the name tanzania by etymonline". www.etymonline.com (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
- ↑ Gordon Kalulunga (2011-06-17). "KALULUNGA BLOG: Mfahamu aliyebuni Jina la Tanzania". KALULUNGA BLOG. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2019-04-28. Iliwekwa mnamo 2019-04-28.
- ↑ "Mohammed Iqbal Dar: Mbunifu wa jina la Tanzania". Global Publishers. 2016-03-07. Iliwekwa mnamo 2019-04-28.
- ↑ "Loading..." home.frognet.net. Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
- ↑ "zanzibar | Etymology, origin and meaning of the name zanzibar by etymonline". www.etymonline.com (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
- ↑ "The World Factbook". web.archive.org. 2014-02-09. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2014-02-09. Iliwekwa mnamo 2022-06-15.
- ↑ "Review of the state of world marine capture fisheries management: Indian Ocean". www.fao.org. Iliwekwa mnamo 2022-06-15.
- ↑ "Kalambo Falls | waterfall, East Africa | Britannica". www.britannica.com (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2022-06-15.
- ↑ Verfasser, Zorita, Eduardo (2002). Rainfall variability in Northern Tanzania in the March-May season (long rains) and its links to large-scale climate forcing. OCLC 1075513535.
{{cite book}}
:|last=
has generic name (help)CS1 maint: multiple names: authors list (link) - ↑ "Tanzania". www.climatelinks.org (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
- ↑ Future Climate for Africa (2017). "Future Climate Projections for Tanzania" (PDF). Future Climate for Africa.
- ↑ "Tanzania | UNDP Climate Change Adaptation". www.adaptation-undp.org (kwa Kiingereza). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2022-04-16. Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
- ↑ "Tanzania: National climate change strategy - National Policy, Plans & Statements - PreventionWeb.net". web.archive.org. 2021-04-17. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2021-04-17. Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
- ↑ "Tanzania travel guide | Tanzania | Zepisa African safaris". web.archive.org. 2020-12-01. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2020-12-01. Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
- ↑ Ridwan, Laher; Korir, SingíOei (2014-05-05). Indigenous People in Africa: Contestations, Empowerment and Group Rights (kwa Kiingereza). Africa Institute of South Africa. ISBN 978-0-7983-0464-1.
- ↑ "The official site of the Tanzania National Parks - Gombe Stream National Park". web.archive.org. 2014-10-04. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2014-10-04. Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
- ↑ Riley, Laura (2005). Nature's strongholds : the world's greatest wildlife reserves. unknown library. Princeton, N.J. : Princeton University Press. ISBN 978-0-691-12219-9.
- ↑ Stuart, S. N. (1990). Biodiversity in sub-Saharan Africa and its islands : conservation, management, and sustainable use. Internet Archive. Gland, Switzerland : IUCN. ISBN 978-2-8317-0021-2.
- ↑ "Serengeti wildebeest migration explained with moving map". www.expertafrica.com. Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
- ↑ Edoarado Razzetti and Charles Andekia Msuya (2002) "Introduction" Archived 16 Julai 2020 at the Wayback Machine, Field Guide to Amphibians and Reptiles of Arusha National Park. Tanzania National Parks. p. 11
- ↑ Arusha, Edward Qorro in (12 Agosti 2019). "Africa: Tanzania Has Largest Number of Lions in Africa, New Report Says". allAfrica.com (kwa Kiingereza).
- ↑ Grantham, H. S.; na wenz. (2020). "Anthropogenic modification of forests means only 40% of remaining forests have high ecosystem integrity – Supplementary Material". Nature Communications. 11 (1): 5978. doi:10.1038/s41467-020-19493-3. ISSN 2041-1723.
- ↑ Athuman Mtulya (26 September 2013) "Report reveals rapid rural -urban migration". thecitizen.co.tz.
- ↑ Ulrich Ammon; Norbert Dittmar; Klaus J. Mattheier (2006). Sociolinguistics: An International Handbook of the Science of Language and Society. Walter de Gruyter. pp. 1967–. ISBN 978-3-11-018418-1.
- ↑ Kadiri ya Ulrich Ammon; Norbert Dittmar; Klaus J. Mattheier (2006). Sociolinguistics: An International Handbook of the Science of Language and Society. Walter de Gruyter. p. 1967. ISBN 978-3-11-018418-1 tayari Kiswahili ni lugha ya kwanza kwa asilimia 10 za wananchi
- ↑ Concise Encyclopedia of Languages of the World. Elsevier. 2010. pp. 1026–. ISBN 978-0-08-087775-4.
- ↑ "Tanzania Ditches English In Education Overhaul Plan". AFK Insider. 17 February 2015. Retrieved 23 February 2015.
- ↑ Turkish, Portuguese firms win bid to construct Tanzania’s SGR, tovuti ya theeastafrican.co.ke ya 6 Februari 2017, iliangaliwa Mei 2017
- ↑ Askew, Kelly; Askew, Professor Kelly (2002-07-28). Performing the Nation: Swahili Music and Cultural Politics in Tanzania (kwa Kiingereza). University of Chicago Press. ISBN 978-0-226-02981-8.
- ↑ Ivaska, Andrew (2011-01-25). Cultured States: Youth, Gender, and Modern Style in 1960s Dar Es Salaam (kwa Kiingereza). Duke University Press. ISBN 978-0-8223-4770-5.
- ↑ Stone, Ruth M. (2010-04-02). The Garland Handbook of African Music (kwa Kiingereza). Routledge. ISBN 978-1-135-90001-4.
- ↑ Edmondson, Laura (2007-07-20). Performance and Politics in Tanzania: The Nation on Stage (kwa Kiingereza). Indiana University Press. ISBN 978-0-253-11705-2.
- ↑ Njogu, Kimani; Maupeu, Herv (2007-10-15). Songs and Politics in Eastern Africa (kwa Kiingereza). African Books Collective. ISBN 978-9987-08-108-0.
- ↑ Mahenge, Elizabeth (2022-04-16). "Matumizi ya Mbinu ya Usimulizi katika Kuibua Dhamira ya Ukombozi wa Kisiasa Kusini mwa Afrika: Uchunguzi wa Nyimbo Teule za Muziki wa Dansi nchini Tanzania 1940-1990". Mulika Journal. 40 (2).
- ↑ Njogu, Kimani; Maupeu, Herv (2007-10-15). Songs and Politics in Eastern Africa (kwa Kiingereza). African Books Collective. ISBN 978-9987-08-108-0.
- ↑ Kerr, David (2018-01-02). "From the margins to the mainstream: making and remaking an alternative music economy in Dar es Salaam". Journal of African Cultural Studies. 30 (1): 65–80. doi:10.1080/13696815.2015.1125776. ISSN 1369-6815.
- ↑ Suriano, M. (2011). "Hip-Hop and Bongo Flavour Music in Contemporary Tanzania: Youths' Experiences, Agency, Aspirations and Contradictions". Africa Development (kwa Kiingereza). 36 (3–4): 113–126. doi:10.4314/ad.v36i3-4. ISSN 0850-3907.
- ↑ Perullo, Alex (2005). "Hooligans and Heroes: Youth Identity and Hip-Hop in Dar es Salaam, Tanzania". Africa Today. 51 (4): 75–101. ISSN 0001-9887.
- ↑ Brennan, James; Burton, Yus (2007-10-15). Dar es Salaam. Histories from an Emerging African Metropolis (kwa Kiingereza). African Books Collective. ISBN 978-9987-08-107-3.
- ↑ "THE BROADCASTING SERVICES ACT, 1993" (PDF) (Act) (kwa Kiingereza). Juni 11, 1994. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2020-09-27. Iliwekwa mnamo 2022-06-17.
- ↑ Perullo, Alex (2011). Live from Dar es Salaam: Popular Music and Tanzania's Music Economy. United States: Indiana: Indiana University Press. ISBN 978-0-253-00150-4. Iliwekwa mnamo 5 Juni 2022.
- ↑ Nne, Juma (2001-10-01). "Saleh J – Tanzanian Swahili rap pioneer". Africanhiphop.com (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 5 Juni 2022.
- ↑ Kerr, David (2018-01-02). "From the margins to the mainstream: making and remaking an alternative music economy in Dar es Salaam". Journal of African Cultural Studies (kwa Kiingereza). 30 (1). Routledge: 65-80. doi:10.1080/13696815.2015.1125776. ISSN 1369-6815.
- ↑ 50.0 50.1 50.2 50.3 50.4 50.5 50.6 Otiso, Kefa M. (2013-01-24). Culture and Customs of Tanzania (kwa Kiingereza). ABC-CLIO. ISBN 978-0-313-08708-0.
- ↑ 51.0 51.1 51.2 Doling, Tim (1999). Tanzania Arts Directory (kwa Kiingereza). Visiting Arts. uk. 17. ISBN 9781902349114.
- ↑ Wairagala, Wakabi (2004). Tanzania (kwa Kiingereza). Gareth Stevens. ISBN 978-0-8368-3119-1.
- ↑ Pritchett, Bev (2007-12-15). Tanzania in Pictures (kwa Kiingereza). Twenty-First Century Books. ISBN 978-0-8225-8571-8.
- ↑ "NSC should perfect all sports categories". Tanzania Sports (kwa Kiingereza (Uingereza)). 2011-10-01. Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
- ↑ "Member Association - Tanzania - FIFA.com". web.archive.org. 2020-07-04. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2020-08-23. Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
- ↑ CAF-Confedération Africaine du Football. "U17 AFCON - Asante Sana Tanzania!!!". CAFOnline.com (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
- ↑ "Tanzania win Cecafa Women's trophy", BBC Sport (kwa Kiingereza (Uingereza)), iliwekwa mnamo 2022-06-16
- ↑ "Tanzania retain Cecafa Women's Cup", BBC Sport (kwa Kiingereza (Uingereza)), iliwekwa mnamo 2022-06-16
- ↑ PTI / Jun 6, 2022, 15:53 Ist. "Morocco, Nigeria, Tanzania book last 3 spots in FIFA U-17 Women's World Cup in India | Football News - Times of India". The Times of India (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
{{cite web}}
: CS1 maint: multiple names: authors list (link) CS1 maint: numeric names: authors list (link) - ↑ "Hasheem Thabeet Stats". Basketball-Reference.com (kwa Kiingereza). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2020-12-07. Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
- ↑ "Filbert BAYI | Profile | World Athletics". www.worldathletics.org. Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
- ↑ 1975 Miracle Mile: Filbert Bayi runs 3:51.0, iliwekwa mnamo 2022-06-16
- ↑ "Bayi's record may be gone but it should never be forgotten". HeraldScotland (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
- ↑ "Swahiliwood: Researching Tanzania's Film Industry - Media for Development International". mfditanzania.com. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2020-02-06. Iliwekwa mnamo 2022-06-17.
- ↑ "ZIFF 2022 | Zanzibar International Film Festival" (kwa American English). Iliwekwa mnamo 2022-06-17.
Viungo vya nje
- Wikimedia Atlas of Tanzania
- Tanzania katika Open Directory Project
- Tanzania Corruption Profile Archived 12 Agosti 2016 at the Wayback Machine. from the Business Ani-Corruption Portal
Arusha | Dar es Salaam | Dodoma | Geita | Iringa | Kagera | Katavi | Kigoma | Kilimanjaro | Lindi | Manyara | Mara | Mbeya | Morogoro | Mtwara | Mwanza | Njombe | Pemba Kaskazini | Pemba Kusini | Pwani | Rukwa | Ruvuma | Shinyanga | Simiyu | Singida | Songwe | Tabora | Tanga | Unguja Kaskazini | Unguja Kusini | Unguja Mjini Magharibi |
Nchi za Afrika | |
---|---|
Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Eswatini | Ethiopia | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesotho | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Zambia | Zimbabwe | |
Maeneo ya Afrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika | |
Hispania: Kanari · Ceuta · Melilla | Italia: Pantelleria · Pelagie | Ufaransa: Mayotte · Réunion | Uingereza: · St. Helena · Diego Garcia | Ureno: Madeira |
Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Tanzania kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |