Edward Tingatinga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Edward Saidi Tingatinga (1937 - 1972) alikuwa na msanii Mtanzania aliyeanzisha mtindo wa uchoraji wa Tingatinga unaojulikana sana siku hizi na kutafutwa na wapenzi wa sanaa ya Tanzania kote duniani.

Maisha kabla ya sanaa[hariri | hariri chanzo]

Kijiji kilichopo karibu na Namocheli alipozaliwa Edward Tingatinga

Alizaliwa 1937 Umakonde ila haijajulikana kama upande wa Tanzania au upande wa Msumbiji. Vijiji mbalimbali vimetajwa kama mahali pa kuzaliwa kwake kama vile Mindu, Namocheli (leo Nakapanya - vyote katika wilaya ya Tunduru) au Msumbiji. Anasemekana alisoma shule ya msingi ya misioni katoliki Nandembo.

Kati ya miaka 1955 na 1959 - habari zikitofautiana - alihamia Dar es Salaam alipopata kazi kama mtumishi wa nyumbani kwa Waingereza. Hao walipoondoka baada ya uhuru Edward alipaswa kujitafutia maisha kwa biashara ndogondogo mtaani.

Kuchora kwa kujipatia chakula[hariri | hariri chanzo]

Siku zile alianza kuchora ingawa haijulikani ilikuwa kwa njia gani. Katika miaka ya 1960 aliuza picha zake barabarani kwa Shilingi 15 iliyokuwa sawa na bei ya mlo.

Mwaka 1968 baada ya kufunga ndoa na Agata Mataka alikazia uchoraji. Wengine walisema ya kwamba aliendelea na kazi ndogo kwenye hospitali ya Muhimbili ingawa hapa haijulikana alifanya kazi gani kamili na hadi lini.

Mtindo wa Tingatinga[hariri | hariri chanzo]

Wakati ule alianzisha mtindo wake. Badala ya karatasi alichora kwenye ubao aina ya "ceiling board" iliyokuwa rahisi lakini ni imara. Alikata vipande vya mraba vya futi 2x2. Akishirikiana na wadogo zake alianza kuchora picha za wanyama.

Mnamo mwaka 1970 Wazungu kutoka Skandinavia walianza kutafuta picha zake wakimsaidia kuhudhuria maonyesho ya biashara ya kwanza ya Dar es Salaam. Ghafla Tingatinga akawa maarufu, picha zake zilitafutwa na bei zikapanda. Picha zake zilikuwa uso wa sanaa ya Tanzania akawa mchoraji maarufu wa Afrika yote.

Kifo na ushirika wa Tingatinga[hariri | hariri chanzo]

Edward Tingatinga aliaga dunia mnamo mwaka 1972. Alipigwa risasi na polisi kimakosa akidhaniwa ni mhalifu. Alizikwa kwenye makaburi ya Msasani Mikoroshini mjini Dar es Salaam.

Ndugu zake waliendelea na mtindo wake wa uchoraji na wengine wengi walimfuata wakiiga mtindo huo. Mtindo wa uchoraji wa Tingatinga (Tingatinga painting) uliendelea kukua na kuwa kivutio kwa watalii nchini Tanzania, Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Awali walikuwa na matatizo kwa sababu walifukuzwa mara nyingi toka mahali walipofanya kazi. Mwaka 1977 wachoraji Hashimi Mruta, Zaburi Muradi Chimwanda, Amonde, Tedo, Mpata, Amadi Saidi, Mchisa, Abasi, Salum Mussa, Mohamedi Saidi Chilamboni na Fr. J. Linda waliunda ushirika wa "TINGATINGA Partnership" wakaiandikisha serikalini. Mwenyekiti wa kwanza alikuwa Omari Amonde.

Washirika walijenga vibanda karibu na Morogoro Stores ambako picha zao ziliuzwa.

Ushirika ulibadilisha jina mwaka 1990 kuwa "Tingatinga Arts Cooperative Society Limited".

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

People.svg Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Edward Tingatinga kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.