Shaaban Robert

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Shaaban Robert (1 Januari 1909 - 22 Juni 1962) alikuwa mshairi na mwandishi wa riwaya. Mchango wake katika lugha ya Kiswahili ni mkubwa kwani kazi zake zinaheshimika katika fasihi ya Kiswahili na pia zinatumika mashuleni.

Maisha

Shaaban Robert alizaliwa tarehe 1 Januari 1909 kijiji cha Vibambani jirani na Machui kilomita 10 kusini mwa mji wa Tanga, alipata elimu yake katika shule ya Msimbazi, jijini Dar-es-salaam kati ya miaka 1922 na 1926 alifaulu na kupata cheti.

Akaajiriwa na serikali ya kikoloni akawa karani katika idara ya forodha huko Pangani mwaka 1926 – 1944. Bila shaka kukaa kwake miaka mingi hivi katika mji wa kihistoria uliokuwa mahali pa utamaduni wa Kiswahili tena mahali patulivu kumesaidia maendeleo yake Shaaban kama mwandishi wa Kiswahili.

Tangu 1944 alihamia ofisi nyingine ya Hifadhi ya Wanyama, baadaye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

Mbali na maandio yake alikuwa na athari kubwa katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili akiwa mjumbe wa kamati za East Africa Swahili Committee, East Africa Literature Bureau na Tanganyika Languages Board.

Kwa ujumla Mzee Shaaban Robert aliandika vitabu ishirini na mbili. Baadhi ya vitabu hivi ni: Adili na Nduguze, Kusadikika, Kufikirika, Wasifu wa Siti Binti Saad, Baada ya Miaka Hamsini, na Maisha Yangu. Vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha za Kichina, Kiingereza na Kirusi. Alifariki dunia tarere 22 Juni 1962 na kuzikwa Machui. Aliacha wake watatu na watoto kumi.

Familia na Elimu

Wazazi wake wote wawili walikuwa wa ukoo wa Mganga wa kabila la Kiyao. Hatujui sana habari za wazazi wake, lakini twajua kwamba jina la baba yake halikuwa Robert. Jina hili ama latokana na matamshi mabaya ya jina lake hasa au yawezekana kuwa ni jina alilopewa alipokuwa skuli Msimbazi. Kwa muda mfupi yeye mwenyewe aliandika jina lake ‘Roberts’, lakini baadaye aliacha kuliandika hivyo. Alizaliwa Vibambani, ambacho ni kijiji kilicho kusini ya Machui, yapata maili sita kusini ya Tanga, tarehe mosi Januari mwaka wa 1909. Hakujiita Myao kabisa, bali alikuwa mmojawapo wa wachache ambao daima walijiita Waswahili.

Alielemishwa Dar es Salaam toka mwaka wa 1922 mpaka mwaka wa 1926, akawa mtu wa pili katika wanafunzi kumi na mmoja waliofaulu mitihani yao na kupewa shahada ya kutoka chuoni, yaani School Leaving Certificate. Alioa mara tatu: mke wa kwanza alikuwa Mdigo. Alikuwa na watoto kumi. Alipofariki aliacha watoto watano. Pia aliacha dada yake (wa baba mmoja) Mwana Saumu, na Mama Yake.

Kazi

Kazi alizofanya alipokuwa Karani wa Serikali:

 • Forodhani Pangani na mahali pengine tokea mwaka 1926 mpaka 1944
 • Idara ya Wanyama tokea mwaka 1944 hata 1946
 • Afisi ya Mkuu wa Jimbo Tanga tokea mwaka 1946 hata 1952
 • Afisi ya Kupima Nchi Tanga tokea mwaka 1952 hata 1960.

Alipandishwa cheo kuwa Grade III Higher Division mwaka 1929, na katika mwaka wa 1944 akapandishwa tena kuwa Grade II Local Service Alikuwa mwanachama wa East African Swahili Committee, East African Literature Bureau, Tanganyika Languages, Tanga Township Authority.

Kifo na Kumbukumbu

Marehemu akafariki Tanga tarehe ya 22 Juni 1962, akazikwa Machui.

Alitunza kwa zawadi ya waandishi inayoitwa ‘Margaret Wrong Memorial Prize’; pia alikuwa ametunzwa nishani ya M.B.E.

Vitabu vyake

 • Maisha yangu
 • Kusadikika nchi iliyo angani
 • Kufikirika
 • Adili na nduguze
 • Masomo yenye adili
 • Utenzi wa Vita vya Uhuru
 • Wasifu wa Siti Binti Saad
 • Baada ya Miaka Hamsini

Viungo vya nje

Quill and ink.svg Makala hii kuhusu mwandishi fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Shaaban Robert kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.