Nenda kwa yaliyomo

Kisiwa cha Mafia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Visiwa vikubwa vya Tanzania (Zanzibar, Pemba, Mafia).

Mafia ni funguvisiwa la Tanzania, pamoja na jina la kisiwa kikubwa ndani yake, linalotazama mwambao wa Afrika ya Mashariki km 130 kusini kwa Dar es Salaam karibu na mdomo wa Mto Rufiji.

Umbali wake na bara ni km 16.

Kisiwa kikuu kiko katika Bahari ya Hindi, kikiwa na urefu wa km 49 na upana wa km 16; eneo lake ni takriban km² 400. Inajulikana pia kwa jina "Chole shamba" kutokana na mji wa kale wa Chole uliokuwepo kwenye kisiwa kidogo cha Chole kilichopo karibu na kisiwa kikuu kwa umbali wa mita 900.

Wilaya ya Mafia ni kati ya wilaya 6 za mkoa wa Pwani ikiwa na wakazi 40,801 (2002). Mji mkubwa na makao makuu ya wilaya ni Kilindoni.

Ina tarafa mbili ambazo ni:

  1. Tarafa ya kusini
  2. Tarafa ya kaskazini

Kata za wilaya ya Mafia ni kama zifuatazo:

Ina jumla ya vijiji 23.

Wakazi walio wengi ni wavuvi wanaolima pia mashamba madogo. Bidhaa za sokoni ni pamoja na nazi, chokaa na samaki.

Kuna utalii unaosifiwa sana lakini idadi ya wageni bado ni ndogo. Hasa Waitalia wamependa kutembelea Mafia pia kwa sababu ya jina la kisiwa ambalo kwa Kiitalia linamaanisha shirika la kigaidi lenye historia ndefu katika Italia ya kusini hadi siku ya leo.

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Mafia ilikuwa mahali pa miji ya kale ya utamaduni wa Waswahili kama vile miji ya Chole na Kua. Baada ya kuondoka kwa Wareno ilikuwa chini ya Sultani wa Omani (baadaye wa Zanzibar).

Mwaka 1892 Wajerumani walinunua Mafia kutoka kwa Sultani wa Zanzibar ikawa sehemu ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani[1].

Mwaka 1915, wakati wa Vita Kuu ya Kwanza, Waingereza waliteka kisiwa wakishambulia kutoka hapa manowari ya Kijerumani ya SMS Königsberg mdomoni mwa mto Rufiji kutoka Mafia.[2]

Mnamo 1922, baada ya mwisho wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Mafia imekuwa sehemu ya Tanganyika, si tena Zanzibar.

Viboko visiwani

[hariri | hariri chanzo]

Kisiwa kikuu, kinachokadiriwa kuwa na ukubwa wa karibu nusu ya Unguja, kina sifa ya pekee ya kuwa na wanyama aina ya viboko, ambao kwa kawaida huishi katika maji ya mito, maziwa, na maeneo yenye unyevunyevu. Viboko, wanaojulikana kisayansi kama "Hippopotamus amphibius", ni wanyama wa tatu kwa ukubwa duniani kati ya wale wa nchi kavu, wakifuatia tembo na faru weupe; dume la kiboko linaweza kufikia uzito wa tani 4.5.

Viboko wanaweza kupatikana katika maeneo mbalimbali kusini mwa Jangwa la Sahara mwaka mzima, na kwa Tanzania, wanapatikana hasa katika mito na mabwawa kama Mto Rufiji na Mto Wami, pamoja na maeneo ya hifadhi kama Serengeti na Katavi. Uwepo wao kisiwani Mafia unakipa kisiwa hicho umaarufu na kutofautisha na maeneo mengine katika Bahari ya Hindi.[3]

Wanasayansi na watafiti wametafakari kuhusu jinsi viboko walivyofika Mafia, na wengi hudhani walitokea Mto Rufiji au waliletwa na mafuriko yaliyotokea miaka mingi iliyopita. Hata hivyo, swali la jinsi walivyoweza kuvuka maji ya chumvi umbali wa zaidi ya kilometa 20 bado linabaki kuwa la kushangaza.

Uchunguzi unaonyesha kwamba Mafia, kama visiwa vya Pemba na Zanzibar, ilijitenga kutoka bara kufuatia mchakato wa maelfu ya miaka, ambapo sehemu za nchi kavu zilizungukwa na bahari na kuwa visiwa. Kwa mantiki hiyo, viboko walio Mafia wanaweza kuwa walitenganishwa na bara la Afrika wakati huo, wakabaki kisiwani hapo tangu kipindi hicho.

Hata hivyo, viboko wa Mafia wako hatarini kutoweka kutokana na uwindaji, migongano na binadamu, na mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri makazi yao. Takwimu zisizo rasmi zinaonyesha idadi yao inaweza kuwa chini kiasi cha viboko 10 hadi 20, hali inayohitaji hatua za haraka za ulinzi na uhifadhi mkubwa kutoka kwa serikali, wananchi wa Mafia, na wadau wa uhifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  1. Biashara hiyo iliwahi kukubaliwa mwaka 1890 katika Mkataba wa Helgoland-Zanzibar kati ya Uingereza na Ujerumani
  2. Mafia Island, German East Africa, January 1915, kuhusu uvamizi wa Mafia na Waingereza mwaka 1915, tovuti ya http://www.trenchfighter.homepage.t-online.de
  3. https://www.jamhurimedia.co.tz/maajabu-ya-viboko-kisiwani-mafia/

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Pwani bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Kisiwa cha Mafia kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.