SMS Königsberg

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
SMS Königsberg huko Daressalaam 1914

SMS Königsberg [1] (tamka ke-niks-barg) ilikuwa manowari ya Kijerumani iliyoshiriki katika mapigano ya vita kuu ya kwanza ya dunia katika Afrika ya Mashariki. Bodi yake inakaa hadi leo chini ya maji kwenye mdomo wa mto Rufiji ilipozamishwa.

Ujenzi wa Königsberg ulimalizika mwaka 1906 mjini Hamburg. Jina lilitolewa kwa heshima ya mji wa Königsberg katika Ujerumani jimbo la Prussia Mashariki. Ilisukumwa na injini ya mvuke iliyoendeshwa kwa makaa. Ukubwa wake ilikuwa tani GT 3390 t.

Kiasili ilifanya kazi katika Bahari ya Kaskazini na Bahari ya Baltiki hasa iliongozana mara kadhaa na meli ya kifalme ya Kaisari Wilhelm II.

Kufika Afrika ya Mashariki[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1914 ilitumwa itembelee koloni ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani chini ya amri ya nahodha Max Loof. Ilipofika ilikuwa manowari ya kwanza ya kisasa ya wakati wake iliyofika Daressalaam ikaitwa na wenyeji "manowari ya bomba tatu" kutokana na dohani zake tatu.

SMS Königsberg ilifika tareke 6 Juni 1914 na mwezi uleule katika Ulaya mfalme mteule wa Austria-Hungaria aliuawa na mgaidi Mserbia katika mji wa Sarayevo. Kwa hiyo hali ya siasa ya kimataifa ikawa mbaya ilikuwa wakati wa maandalizi ya vita kuu ya kwanza. Mwisho wa Julai ilipoonekana ya kwamba vita kati ya Austria-Hungaria na Serbia italeta pia mapigano kati ya Ujerumani na mataifa mengine SMS Königsberg ilifuata amri zilizoandaliwa ikaondoka katika bandari ya Daressalaam na kusubiri baharini habari kama Uingereza itaingia vitani dhidi ya Ujerumani na Austria-Hungaria. Königsberg ilikuwa manowari kubwa ya pekee ya Ujerumani katika Bahari Hindi wakati Waingereza walikuwa na manowari mengi huko Afrika Kusini na hasa Uhindi.

Manowari tatu za Waingereza kutoka Afrika Kusini zilipelekwa Afrika ya MAshariki zikasubiri nje ya Daressalaam walikuwa na amri ya kuzuia Königsberg ndani ya bandari au kuifuata kila mahali kwa sababu nao Waingereza walitegemea vita inaweza kuanza kila siku wakaona Köniberg ingekuwa hatari kwa meli za Kiingereza katika Bahari Hindi. Lakini katika usiku wa 1 Agosti SMS Königsberg ilifaulu kupita kwenye manowari za Kiingereza ma kwa kutumia mbio mkuu ikakimbia hadi Waingereza walishindwa kuiona tena.

Vita ya bahari Hindi[hariri | hariri chanzo]

Tarehe 5 Agosti SMS Königsberg ilipokea kwa njia ya simu hewa habari za hali ya vita iliyoanzishwa siku ileile. Wakati ule ilikuwa mbele ya rasi Gardafui ya Somalia. Akiba yake ya makaa mawe ilikuwa imepungua mno kutokana na mbio mkubwa katika mashindano na Waingereza mbele ya Daressalaam. Tar 5 Agosti ilikutana na meli ya Kiingereza City of Winchester iliyobeba majani ya chai kutoka Uhindi ikaikamata ikachukua makaa mawe yake na kuizamisha.

Matatizo ya makaa yaliendelea lakini meli kadhaa za Kijerumani ziliweza kukutana na manowari na kuipatia kiasi cha makaa yao. Ikaona manowari za kiingereza kwa mbali ikaamua kuelekea kusini tena. Tar. 30 Agosti ilivamia bandari ndogo ya Majunga kwenye koloni ya Kifaransa ya Madagaska. Lakini haikukuta meli yoyote ikaondoka tena bila mapigano na Wafaransa walifikiri ilikuwa manowari ya Kiingereza.

Kimbilio katika delta yya Rufiji[hariri | hariri chanzo]

Kapteni Loof aliamua kutafuta kimbilio katika delta ya mto Rufiji; Wajerumani pekee walijua ya kwamba mkono mmoja wa delta hii ulikuwa na kimo cha kutosha kwa manowari yake lakini hii ilikuwa siri alitegemea ya kwamba Waingereza wasingemtafuta hapa. Kwa hiyo tar. 3 Septemba Königsberg pamoja na meli moja ya Kijerumani iliyobeba makaa zikaingia mdomo wa Rufiji. Hapa waliweza kufungua injini na kufanya matengenezo kadhaa za lazima pia kuwasiliana na serikali ya koloni ya Kijerumani iliyofikiri ya kwamba Königsberg ilizamishwa tayari.

Kuzamisha HMS Pegasus[hariri | hariri chanzo]

Tarehe 19 Septemba 1914 Kapteni Loof alipokea taarifa ya kwamba manowari kubwa ya Kiingereza ilifika bandari ya Zanzibar. Loof aliamua kushambulia manowari hii iliokuwa peke yake. Kwa msaada wa nahodha Mjerumani aliyejua pande zote za pwani vizuri alifika mbele ya Zanzibar wakati wa usiku na saa ya alfajiri iliona manowari ya Kiingereza SMS Pegasus kwenye bandari ya Zanzibar. Mara moja Königsberg ilianza kufyatulia risasi kwa bunduki zake ikazamisha Pegasus katika muda wa dakika 20. Pegasus ilishindwa kujitetea ipasavyo kwa sababu ilikuwa Zanzibar kwa matengenezo ya injini yake ilishindwa kukimbia hata kidogo. Königsberg ikaendelea kufyatulia risasi kadhaa kwa mnara wa kituo cha redio ya hewani ya Zanzibar ikarudi Rufiji. Kwa bahati mbaya ikapata tena tatizo la injini kwa sababu pistoni moja ilivunjika na Loof alipaswa kusubiri hadi karahana za Daressalam ziliweza kutengeneza spea.

SMS Königsberg baada ya vita katika maji ya Rufiji
Mtalii na bunduki ya Königsberg mbele ya Boma la Yesu, Mombasa

Mwisho katika Rufiji[hariri | hariri chanzo]

Waingereza walituma mara moja kikosi cha manowari kutoka Uhindi wakatafuta Königsberg. Walibahatishwa kukamata meli moja ya Kijerumani wakakuta risiti ya mzigo wa makaa uliowahi kupokelewa na SMS Königsberg kwenye kituo cha Salale iliyoko katika eneo la delta ya Rufiji. Waingereza walipeleka kikosi cha wanamaji kwa pwani waliopanda miti wakafaulu kuona milingoti ya Königsberg kwa mbali. Sasa manowari wa Waingereza walikusanyika mbele ya delta ya Rufiji na kusubiri lakini walishindwa kuona Königsberg hivyo waliendelea kufyatulia risasi bila kuwa uhakika. Wakaendelea kuzamisha meli moja katika mkono wa mto ulipokaa SMS Königsberg kwa shabaha ya kuziba njia hii. Hata hivyo SMS Königsberg haikuwa na uwezo wa kutoka kutokana na uhaba wa makaa.

Hali hii iliendela kwa miezi tisa hadi Julai 1915. 10 Januari 1915 Waingereza walivamia kisiwa cha Mafia iliyokuwa na wanajeshi Wajerumani na Waafrika 23 pekee. Walijenga kiwanja cha ndege wakaleta ndege kadhaa zilizoendelea kupeleleza delta kutoka angani. Wajerumani walipeleka wanajeshi katika delta kwa lengo la kuzuia wanamaji kuikaribia Königsberg kwa miguu.

Mwezi wa Juni 1915 manowari mbili ndogo aina ya monitor yenye bunduki kubwa zilifika mbele ya Rufiji zilizovutwa hapa kutoka Uingereza. Hizi monitor ziliweza kuingia katika mkono moja wa Rufiji zikaanza kufyatulia Königsberg zikipokea taarifa kutoka ndege zilizotazama jinsi gani risasi zililengwa vema au la. Katika mashambulio mawili tarehe 6 na 11 Julai Königsberg ilipigwa vibaya mara kadhaa. Wakati wa 11 Julai Wajerumani walikosa risasi za kutosha na mapigo ya Waingereza zilisababisha hasara kubwa.

Katika hali hii kapteni Loof aliamua kuondoa bunduki na vifaa vyote vilivyoweza kutumiwa kwenye nchi kavu kutoka manowari yake na kuizamisha mtoni. Baada ya kuzamisha meli sitaha yake bado ilikuwa juu ya maji kutokana na kimo kidogo cha maji na Wajeruamni walirudi kwa muda wa siku nyingu na kuchukua vitu vingi.

Habari za baadaye[hariri | hariri chanzo]

Bunduki kubwa 10 zilibadilishwa kuwa bunduki za nchi kavu kwa kuzifunga juu ya magurudumu zikawa bunduki kubwa katika vita iliyofuata. Mara kadhaa zilipigana na bunduki kutoka HMS Pegasus zilizookolewa kutoka manowari ile iliyozamishwa na Königsberg huko Zanzibar na kutumiwa pia kwa vita ya nchi kavu.

Wanamaji 350 ziliingizwa katika jeshi la kutetea koloni ya Kijerumani chini ya kamanda Paul von Lettow-Vorbeck. Kati ya hao wote ni 32 pekee waliorudi Ujerumani baada ya vita wengine walikufa.

Bunduki kadhaa zilikamatwa baadaye na Waingereza. Moja iko kama maonyesho na kumbukumbu ya kihistoria mbele ya Boma la Yesu huko Mombasa pamoja na bunduki kutoka HMS Pegasus. Nyingine iko Pretoria (Afrika Kusini) mbele ya ikulu.

Sehemu za juu za SMS Königsberg zilionekana kwenye Rufiji wakati wa maji ya kupwa hadi miaka ya 1970 lakini bodi yake iliendelea kuzama chini katika matope ya mto na sasa haionekani tena.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. SMS ni kifupi cha Kijerumani "Seiner Majestät Schiff" sawa na Kiingereza "HMS - His/Her Majesty's Ship" yaani manowari ya mfalme maana yake manowari ya jeshi la wanamaji

Marejeo ya Nje[hariri | hariri chanzo]