Tani GT

Tani GT (kifupi cha tani ya aina ya "gross tonnage") ni kipimo cha ukubwa wa meli kilichokuwa kawaida kimataifa tangu mwaka 1982 kufuatana na mapatano ya kimataifa kuhusu upimaji wa ukubwa wa meli (The International Convention on Tonnage Measurement of Ships) ya mwaka 1969. Tani GT zilichukua nafasi ya vipimo vya awali vilivyoitwa pia tani lakini kwa mjao tofauti iliyokadiria mjao wa nafasi za shehena (mzigo) pekee.
Umuhimu wa tani GT ni ya kwamba kodi na malipo kwa ajili ya meli hufuata kipimo hiki kama vile kodi za kutumia mifereji (Suez, Panama) au kukaa bandarini.
Tani GT zinataja mjao wa nafasi yote ya ndani ya meli, yaani ya kila sehemu ambayo imefungwa kwa kuta za pembeni, sitaha na majengo juu ya sitaha ("the moulded volume of all enclosed spaces of the ship").
Lakini si mjao huu pekee yake. Idadi ya mita za mjao inazidishwa kwa namba inayotegemea ukubwa wa meli iko kati ya 0,22 na 0,32; yaani hali halisi asilimia 22 hadi 32 ya mjao inahesabiwa kuwa tani GT. Meli ndogo zinapata makadirio nafuu yaani ya asilimia 22 au karibu nayo halafu meli kubwakubwa hukadiriwa kwa namba inayolingana zaidi na 32.
Meli yenye mjao wa mita za ujazo 10,000 inazidishwa na namba 0,28 hivyo kukadiriwa kuwa na tani GT 2,800.