Michoro ya Kondoa
Michoro ya Kondoa ni kundi la michoro ya miambani ya kale kwenye kuta za miamba katika wilaya ya Kondoa, mkoa wa Dodoma, katikati mwa Tanzania[1] .
Mapango au nusumapango haya zaidi ya 150 yanapatikana mfululizo kwenye vilima vinavyotazama mtelemko wa Bonde la Ufa la Afrika ya Mashariki. Mfululizo huo una urefu wa kilometa 9 na uko kama kilometa 20 kaskazini kwa Kondoa.
Michoro hii inaonyesha picha za watu, wanyama na uwindaji. Hii inatazamwa kutoa ushuhuda wa namna ya maisha ya wachoraji waliokuwa wawindaji hasa.
Hakuna mapatano kama michoro hii ilikuwa sehemu ya ibada za kuomba mafanikio katika uwindaji au labda ilikuwa namna ya kusimulia habari za maisha haya au labda tu sanaa ya awali bila ya makusudi.
Aina nyingine za michoro zinaonyesha tu milia, duara au alama za kimsingi.
Wataalamu wengine huamini ya kwamba picha hizi zilichorwa tangu miaka 1500 iliyopita na jamii za wawindaji waliokalia eneo hili, lakini wengine husema inaewezekana ni za zamani zaidi, labda hata miaka 10,000.
Michoro inafanana na michoro kwenye mwamba inayopatikana katika Afrika ya Kusini na katika milima ya Sahara.
Kuna dalili ya kwamba sehemu ilichorwa na mababu wa Wasandawe na Wahadzabe wa leo, ambao walihifadhi desturi ya kuchora mwambani hadi miaka ya karibuni na walikuwa wawindaji hadi juzijuzi.
Mwaka 2006 eneo hilo liliingizwa katika orodha ya Urithi wa dunia.[2]
Mahali pazuri pa kuangalia michoro kadhaa kwa urahisi ni kijiji cha Kolo kilichopo kwenye barabara kuu kati ya Babati na Kondoa. Kutoka hapo si mbali hadi sehemu kadhaa penye michoro. Wageni wakatakiwa kujiandikisha kwenye kituo cha hifadhi ya mambo ya kale katika kijiji.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Coulson, David; Borona, Gloria K. (2013). Rock Art of Kondoa Irangi and Other Attractions. TARA (Trust for African Rock Art). ISBN 978-9966-7453-4-7.
- ↑ Netherlands National Commission for UNESCO (2004). World Heritage Papers 13. Paris, France: UNESCO World Heritage Centre. ku. 82–83.
Kujisomea zaidi
[hariri | hariri chanzo]- roughguides.com Archived 28 Juni 2010 at the Wayback Machine.
- The Rock Art of Kondoa and Singida: A Comparative Description (National Museum of Tanzania, 1982, 52 p.)
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]4°43′28″S 35°50′02″E / 4.72444°S 35.83389°E
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Dodoma bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Michoro ya Kondoa kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno. |