Taarab

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Taarab (pia: tarabu, taarabu) ni aina ya muziki ya Afrika ya Mashariki yenye asili yake katika utamaduni wa Waswahili. Neno lenyewe linaaminiwa limetokana na Kiarabu "tarab" (طرب) linalomaanisha "uimbaji, wimbo".

Tabia za taarab

Taarab ni muziki ya Waafrika wa pwani iliyopokea athira kutoka tamaduni nyingi hasa muziki ya Waarabu na Wahindi. Kimsingi ni uimbaji wa mashairi unaofuata muziki wa bendi. Bendi hizi hutofautiana kieneo; katika taarab wa Unguja vinanda vya kulingana na tarab za Kiarabu hupendelewa; katika taarabu wa Mombasa aina za ngoma ni muhimu; katika taarab wa Tanga gitaa inapendwa. Siku hizi vyombo vya kisasa vimetumiwa pia.

Historia

Neno "taarab" laaminiwa lina asili katika Unguja ambako mnamo 1870 Sultani Sayyid Bargash alialika kundi la wanamuziki kutoka Misri kuja Zanzibar walioleta uimbaji wao aina ya "tarab". Alipopenda muziki hii sultani alimtuma Mzanzibari Mohammed bin Ibrahim kwenda Misri ajifunzi vyiombo vya huku. Mohammed aliporudi alikuwa mwanashairi wa Sultani akaendelea kuwafundisha marafiki vinanda vyake. Pamoja waliunda kundi la Nadi Ikhwani Safaa inayosemekana ni bendi ya kwanza iliyotumia jina la "taarab".[1]. Kundi limeendelea hadi leo na kujulikana sasa kwa jina la "Malindi Taarab"[2].

Hata hivyo muziki ya Waswahili inayojulikana leo kwa jina la taarab lina asili ya kale kushinda jina hili ambalo ni kawaida siku hizi. Kuna kumbukumbu kutoka Lamu ya muziki iliyoitwa "kinanda" iliyounganisha uimbaji pamoja na chombo cha kibangala na ngoma ndogo na waimbaji wake walihamia Zanzibar wakaitwa "taarabu" huko.

Taarab katika utamaduni wa Uswahilini

Katika utamaduni wa Waswahili taarab ilikuwa utamaaduni wa pekee kwa sababu ilikuwa mahali pa pekee ambapo wanawake walifika kwenye jukwaa pamoja na wanaume na kuimba. Kwa sababu hii taarab imepingwa mara kwa mara na viongozi wa kidini walioona aina kadhaa za taarab ni haramu hazilingana na masharti ya dini hasa wakati wa mwezi wa Ramadhani na kama watu wanaanza kucheza.[3]

Miaka ya nyuma muziki ya taarab imesambaa hata barani nje ya utamaduni wa Waswahili inavuta wasikilizaji katika miji mikubwa kote Afrika ya Mashariki hadi Burundi na Rwanda. Bendi mbalimbali zimeingiza vyombo vya kisasa vya muziki katika mtindo wao kama vile keyboard na gitaa ya umeme.

Viungo vya Nje

Bendi na waimbaji wa Taarab

Jahazi Modern Taarab‎

Maelezo

  1. tazama Ntarangwi, Mwenda uk. 11
  2. Malindi alimaanishi hapa mji wa Kenya bali mtaa ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar
  3. tazama Ntarangwi, Mwenda uk. 14