Tanzania

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mtanzania)
Rukia: urambazaji, tafuta
The United Republic of Tanzania (Kiing.)
Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania
(Kiswahili)
Bendera ya Tanzania Nembo ya Tanzania
Bendera ya Tanzania Nembo ya Tanzania

Wito: Uhuru na Umoja

Lugha rasmi Kiswahili (kwa dhati)
Mji Mkuu Dodoma
Makao ya Serikali Dar es Salaam
Serikali Jamhuri
Rais John Pombe Joseph Magufuli
Waziri Mkuu Majaliwa K. Majaliwa
Eneo km² 945.087
Wakazi 44,928,923[2] (30th) (2012)
Wakazi kwa km² 46.3
Uhuru kutoka Uingereza tar. 9 Desemba 1961
Pesa Shilingi ya Tanzania
Wakati UTC+3
Dini za wakazi Dini za jadi (34.3%), Ukristo (33.5%), Uislamu (31.4%), wengineo (0.8%){{Sensa ya 27 Agosti 1967[1]}}
Wimbo wa Taifa Mungu ibariki Afrika
Tanzania katika Afrika
Ramani ya mikoa ya Tanzania tangu mwaka 2012

Tanzania ni nchi iliyoko Afrika ya Mashariki. Imepakana na Uganda na Kenya upande wa Kaskazini, Bahari Hindi upande wa mashariki, Msumbiji, Malawi na Zambia upande wa kusini, Kongo, Burundi na Rwanda upande wa magharibi.

Eneo lina kilometa za mraba 945,203 (nchi ya 31 duniani); maji ya ndani yanachukua asilimia 6.2.

Idadi ya watu kwa mujibu wa sensa ya (mwaka 2012) ni 44,928,923 (nchi ya 30 duniani) kutoka 34,443,603 waliohesabiwa katika sensa ya mwaka 2002.

Msongamano ni wa watu 46.3 kwa km2 (nchi ya 124 duniani).

Tanzania ni nchi kubwa zaidi kati ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Mji mkuu ni Dodoma, lakini makao makuu ya serikali bado yapo Dar es Salaam, jiji kubwa zaidi, lenye watu zaidi ya milioni 4,364,541. Majiji mengine ni kama vile Mwanza, Mbeya, Arusha, Tabora na Tanga.

Historia

(Kuhusu historia ya maeneo ya Tanzania kabla ya 1964 angalia makala za Tanganyika, Zanzibar na Afrika ya Mashariki ya Kijerumani)

Jina "Tanzania" limeundwa kutokana na majina ya TANganyika na ZANzibar (pamoja na athira ya jina la kale la "Azania").

Nchi hizo mbili zilikuwa zote chini ya utawala wa Uingereza hadi kupata uhuru lakini hazikuwa makoloni ya kawaida.

Zanzibar ilikuwa na hali ya nchi lindwa kutokana na mikataba kati ya masultani wa Zanzibar na Ufalme wa Muungano (Uingereza).

Tanganyika iliwahi kuwa sehemu ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani hadi Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia halafu ikawa chini ya Uingereza kama eneo la kudhaminiwa kutokana na azimio la Shirikisho la Mataifa iliyoweka Tanganyika katika ngazi "B" ya maeneo ya kudhaminiwa.

Tanganyika na Zanzibar zilikuwa nchi mbili tofauti hadi 1964, zilipoungana na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hapo kiongozi wa Tanganyika Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipata kuwa Rais wa kwanza na kiongozi wa mapinduzi ya Zanzibar Abedi Amani Karume akawa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Tanzania, chini ya Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi (1985-1995) iliruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa Tanzania na kuanza mpango wa kurekebisha uchumi kuendana na masharti ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani.

Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa (1995-2005) aliendeleza mfumo wa uchumi wa soko huria ambapo mashirika ya umma yanabinafsishwa.

Tarehe 21 Desemba 2005 Jakaya Kikwete aliapishwa kuwa Rais wa nne wa taifa (2005-2015), naye aliendeleza sera za watangulizi wake akitokea chama hichohicho cha CCM.

Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar

Tangu muungano wa Tanganyika na Zanzibar kufanyika mwaka 1964 Tanzania imekuwa na miundo ifuatayo:

Mambo yafuatayo yamekubalika kuwa shughuli za muungano:

 • Mambo ya nje
 • Jeshi
 • Polisi
 • Mamlaka ya dharura
 • Uraia
 • Uhamiaji
 • Biashara ya nje
 • Utumishi wa umma
 • Kodi ya mapato, forodha
 • Bandari, Usafiri wa anga, Posta na Simu

Demografia

tazama Orodha ya makabila ya Tanzania

Watu wa Tanzania hawaenei sawasawa. Katika maeneo makavu sana, kuna mtu mmoja tu kwenye kilomita moja ya mraba (1/km²), lakini sehemu zenye rutuba za bara, kuna watu 51 kwa kila kilomita ya mraba. Hatimaye huku Unguja kuna watu 134 kwa kilomita ya mraba.

Zaidi ya asilimia themanini huishi vijijini.

Kuna makabila zaidi ya 120. Makabila yenye watu zaidi ya milioni moja ni Wasukuma, Wanyamwezi, Wachaga, Waha, Wagogo, Wahaya, Wajaluo na Wamakonde.

Tanzania ni nchi pekee ya Afrika ambamo wakazi asili wanawakilisha makundi makuu yote ya makabila ya Kusini kwa Sahara.

Idadi kubwa sana ya Watanzania ni jamii ya Wabantu.

Nje ya hao, kuna Waniloti, kwa mfano Wamasai na Wajaluo ambao wengi wao zaidi wanaishi Kenya.

Kundi lingine ni makabila ya Wakushi wanaoishi kaskazini mwa Tanzania; hao ni makabila ya Wairaqw, Wafiome na Wasi.

Kuna vikundi viwili vya Wakhoisan wanaofanana na makabila ya Botswana na Namibia; majina yao ni Wasandawe na Waburunge.

Hatimaye kuna Wahadzabe wachache ambao utafiti wa DNA umeonyesha hivi karibuni wana uhusiano wa asili na Watwa wa nchi za Afrika ya Kati.

Pia kuna asilimia ndogo ya watu wenye asili ya nje ya bara la Afrika, kwa mfano Wahindi, Waarabu, Waindochina, Wafarsi, Wachina na Waingereza. Hii ilisababishwa na karne za mchanganyiko wa mahitaji ya biashara yaliofanywa na mabara ya Ulaya na Asia hapo Afrika.

Lugha

Nchini Tanzania kuna lugha za kikabila zaidi ya mia moja na ishirini. Hakuna lugha rasmi kisheria, lakini Kiswahili ndiyo lugha ya taifa.

Ingawa kila kabila lina lugha yake, lugha ya taifa ya Tanzania ni Kiswahili ambacho ni mojawapo kati ya lugha za Kibantu. Hali hii imesaidia sana kukubaliwa kwa Kiswahili nchini kwa sababu idadi kubwa ya Watanzania ni wasemaji wa lugha za Kibantu.

Kiswahili kinatumika kama lugha baina ya watu wa makabila mbalimbali na kwa mambo ya rasmi; kwa hiyo ni lugha rasmi ya dhati. Baada ya uhuru, Kiingereza (iliyokuwa lugha ya kikoloni kabla ya uhuru) iliendelea kutumika kwa mambo kadhaa rasmi na kwa elimu kuanzia sekondari, na kwa hiyo ilichukuliwa kama lugha rasmi ya dhati pamoja na Kiswahili. Lakini utumizi wa rasmi wa Kiingereza imepungua katika milongo iliyopita, na sasa utumizi huu karibu umekwisha. Kwa hiyo siku hizi ni kawaida zaidi kuchukulia Kiswahili kama lugha rasmi ya dhati pekee.

Utawala

Mgawanyo wa kiutawala wa Tanzania unafuata Katiba ya nchi I 2.2. Tanzania imegawiwa kwa mikoa 30. Kila mkoa huwa na wilaya ndani yake.

Ndani ya wilaya kuna ngazi za tarafa (division) na kata (ward).

Chini ya kata kuna vijiji na wakati mwingine ngazi ya chini tena ambayo ni vitongoji.

Mkoa Makao Makuu Mkoa Makao Makuu
Arusha Arusha Mwanza Mwanza
Dar es Salaam Dar es Salaam Njombe Njombe
Dodoma Dodoma Pemba Kaskazini Wete
Geita Geita Pemba Kusini Chake Chake
Iringa Iringa Pwani Kibaha
Kagera Bukoba Rukwa Sumbawanga
Katavi Mpanda Ruvuma Songea
Kigoma Kigoma Shinyanga Shinyanga
Kilimanjaro Moshi Simiyu Bariadi
Lindi Lindi Singida Singida
Manyara Babati Tabora Tabora
Mara Musoma Tanga Tanga
Mbeya Mbeya Zanzibar Kati/Kusini Koani
Morogoro Morogoro Unguja Kaskazini Mkokotoni
Mtwara Mtwara Unguja Magharibi Zanzibar

Dini

Nchi haina dini rasmi na katiba ya Tanzania inatangaza uhuru wa dini kwa wote. Mara nyingi idadi ya wafuasi wa dini hutajwa kuwa theluthi moja Waislamu, theluthi moja Wakristo na theluthi moja wafuasi wa dini za jadi. Lakini tangu uhuru swali la dini ya wananchi halijaulizwa tena katika sensa, kwa hiyo kadirio la theluthi-theluthi inawezekana ni zaidi azimio la kisiasa.

Kwenye visiwa vya Zanzibar idadi ya Waislamu huaminiwa kuwa takriban 97%.

Usafiri

(habari za undani zaidi katika makala ya Usafiri wa Tanzania)

Usafiri nchini Tanzania ni hasa kwa njia ya barabara. Mengine ni reli na ndege. Kwenye maziwa makubwa na pwani la Bahari Hindi kuna pia usafiri kwa meli.

Hadi sasa idadi ya barabara za lami si kubwa. Kuna hasa njia nzuri kati ya Dar es Salaam, Mbeya katika kusini-magharibi, Dodoma katika kitovu cha nchi, Arusha / Tanga katika kaskazini-mashariki. Kusini-Mashariki na Magharibi ya nchi kwa jumla haina barabara nzuri na mawasiliano ni magumu.

Shirika mbili za reli zahudumia Tanzania ni TRC (Shirika ya Reli Tanzania - Tanzania Railways Corporation) na TAZARA (Tanzania-Zambia Railways Corporation). TRC imetawala reli ya kati kuanzia Dar es Salaam hadi Kigoma halafu reli ya Tanga kati ya Tanga na Arusha. Tazara imeunganisha Dar es Salaam na kusini ya nchi hadi Zambia. Zote hazikutunzwa vizuri na usafiri unakumbwa na huduma mbaya pamoja na ajali.

Huduma kwa ndege zatumia hasa nyanja za ndege 11 penye barabara ya lami kwa ajili ya ndege hasa Julius Nyerere/Dar es Salaam, Kilimanjaro /Arusha-Moshi na Zanzibar-Kisauni.

Utamaduni na sanaa

Bombwe la Kimakonde: Tembo

Kati ya wasanii wa Tanzania ni hasa wajume wa ubao na wachoraji waliojulikana kimataifa.

Uchongaji wa mabombwe ya Kimakonde yamesifiwa tangu mwanzo wa karne ya 20. Wamakonde wengi wamehamia Daressalaam au Arusha wanapohudumia soko la watalii na soko la nje.

Tangu miaka ya 1970 uchoraji wa "tingatinga" umejulikana: ulipata jina hilo kutoka kwa Edward Tingatinga naye mtu wa Umakonde.

Utamaduni wa Watanzania ni pamoja na utaraab. Muziki ana nyimbo za kitaraab ndizo muhimu sana kwa nchi nzima, hasa visiwani na pwani. Pia kuna miziki ya Kinyarwanda, dansi kama intore n.k.

Urithi wa Dunia

Mahali pafuatapo katika Tanzania pamepokewa katika orodha ya UNESCO ya "Urithi wa Dunia".

(mwaka wa kukubaliwa - jina la mahali)

Tanbihi

 1. International Religious Freedom Report 2007: Tanzania. United States Bureau of Democracy, Human Rights and Labor (14 Septemba 2007). This article incorporates text from this source, which is in the public domain.


Soma pia

Viungo vya nje

WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu: 
Mikoa ya Tanzania
Bandera Tanzania
Arusha | Dar es Salaam | Dodoma | Geita | Iringa | Kagera | Katavi | Kigoma | Kilimanjaro | Lindi | Manyara | Mara | Mbeya | Morogoro | Mtwara | Mwanza | Njombe | Pemba Kaskazini | Pemba Kusini | Pwani | Rukwa | Ruvuma | Shinyanga | Simiyu | Singida | Tabora | Tanga | Unguja Kaskazini | Unguja Kusini | Unguja Mjini Magharibi


Nchi za Afrika Bara la Afrika
Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesotho | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Uhabeshi | Uswazi | Zambia | Zimbabwe
Maeneo ya kiafrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika
Ufaransa: Mayotte · Réunion | Hispania: Visiwa vya Kanari · Ceuta · Melilla | Ureno: Visiwa vya Madeira | Uingereza: · Kisiwa cha St. Helena · Kisiwa cha Diego Garcia
Africa satellite plane.jpg Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Tanzania kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.