Nenda kwa yaliyomo

Mtume Petro

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Petro Mtakatifu)
Mtakatifu Petro katika mavazi ya Kipapa alivyochorwa na Peter Paul Rubens katika karne ya 17.
Mitume wa Yesu
Mfululizo wa kurasa juu ya Yesu
Yesu
Yesu Kristo na Ukristo

Umwilisho  • Utoto wa Yesu  • Ubatizo
Arusi ya Kana • Utume wa Yesu • Mifano ya Yesu  • Miujiza ya Yesu
Kugeuka sura • Karamu ya mwisho • Msalaba wa Yesu  • Maneno saba
Kifo cha Yesu  • Ufufuko wa Yesu
Kupaa mbinguni  • Ujio wa pili
Injili  • Majina ya Yesu katika Agano Jipya  • Yesu kadiri ya historia  • Tarehe za maisha ya Yesu • Kristolojia

Mazingira ya Yesu

Wayahudi • Kiaramu • Bikira Maria • Yosefu (mume wa Maria) • Familia takatifu • Ukoo wa Yesu • Ndugu wa Yesu • Yohane Mbatizaji

Mitazamo juu ya Yesu

Mitazamo katika Agano Jipya · Mitazamo ya Kikristo • Mitazamo ya Kiyahudi • Mitazamo ya Kiislamu • Yesu katika sanaa


Simoni Petro alikuwa Myahudi wa karne ya 1, mfuasi wa Yesu Kristo, tena kati ya wandani wake.

Baada ya Yesu, ndiye mtu anayejulikana zaidi katika Injili zote nne.

Katika orodha zote nne za mitume 12 wa Yesu zinazopatikana katika Biblia ya Kikristo anashika nafasi ya kwanza (tofauti na wenzake wengi ambao wanabadilishana nafasi, na kinyume cha Yuda Iskarioti, msaliti anayepewa daima nafasi ya mwisho); isitoshe Math 10:2 inasisitiza nafasi yake hiyo: "Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro".

Tangu kale Wakristo wengi, hasa Wakatoliki na Waorthodoksi, wanamheshimu kama mtakatifu, tena kama papa wa kwanza wa Roma hadi kifodini chake kati ya miaka 64 na 67, wakati wa dhuluma ya Dola la Roma dhidi ya Ukristo iliyoanzishwa na Kaisari Nero.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila tarehe 29 Juni pamoja na ya Mtume Paulo[1].

Jina lake

[hariri | hariri chanzo]

Mwana wa Yona au Yohana, jina lake asili kwa Kiebrania ni שמעון, Šim‘ôn, Shim'on (kutoka kitenzi shama yaani "kusikiliza").

Kadiri ya Injili ya Mathayo (16:18) na Injili ya Yohane (1:42) ni Yesu Kristo aliyembadilishia jina akamuita Kefa (kwa Kiaramu "mwamba", jina ambalo lilitafsiriwa kwa Kigiriki Petros na kwa Kilatini Petrus).

Mtume Paulo alimtaja kwa kawaida kama Kephas (1Kor 1:12; 3:22; 9:5; 15:5; Gal 1:18; 2:9,11,14) na mara moja kama Petro (Gal 2:7-8).

Maisha yake ya awali

[hariri | hariri chanzo]

Mzaliwa wa Bethsaida, kaskazini kwa Galilaya, alihamia Kapernaumu pamoja na ndugu yake Andrea kwa ajili ya uvuvi kwenye ziwa Galilaya. Kijiji hicho kikawa baadaye makao makuu ya utume wa Yesu katika maeneo ya kaskazini ya Palestina. Hasa Yesu alitumia nyumba na boti la Petro.

Mtu wa ndoa, Petro hakusomea ualimu wa Torati, lakini alimfuata Yohane Mbatizaji. Akiwa kwake, karibu na mto Yordani, aliletwa na Andrea kwa Yesu (Yoh 1:41-42[2]).

Baada ya kukutana na Yesu

[hariri | hariri chanzo]

Aliitwa na Yesu kumfuata wakiwa huko ziwani (Math 4:18-20 [3]; Lk 5:11[4]) akiahidiwa atakuwa "mvuvi wa watu", halafu akafanywa mtume wake wa kwanza.

Pamoja na Mtume Yakobo Mkubwa na Mtume Yohane, wana wa Zebedayo, alishirikishwa matukio kadhaa ya pekee kama mwandani wa Yesu, hasa aliposhuhudiwa na Mungu mlimani huku ameng'aa kiajabu (Mk 9:2-9).

Akiwa na silika ya uchangamfu, alikuwa msemaji mkuu kati ya mitume wa Yesu; hasa walipoulizwa naye wanamuona kuwa nani, akajibu: "Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai" (Math 16:16). Ndipo alipojibiwa na Yesu: "Heri wewe Simoni Bar-Yona, kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia: Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni" (Math 16:17-19).

Ungamo la namna hiyo linaripotiwa na Yoh 6:68 pia: "Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu".

Mara nyingine majibu yake yalimvutia lawama ya Yesu, hata akaitwa "Shetani" kwa sababu ya kumshawishi aende mbali na matakwa ya Mungu ili afuate mbinu za kibinadamu (Mk 8:33).

Kwa kuwa Yesu alitakiwa kutumikia, akawafundisha wafuasi wake kutumikia, Petro aliagizwa kuandaa pamoja na Yohane karamu ya mwisho ya Yesu na mitume wake kwenye Pasaka, ambapo ilimbidi akubali kuoshwa naye miguu (Yoh 13:8-9[5]).

Yesu alipokamatwa, Petro alijaribu kumtetea kwa upanga, halafu akamfuata kwa mbali pamoja na Yohane mpaka ndani ya ua wa nyumba ya kuhani mkuu. Ndipo woga ulipomfanya amkane Yesu mara tatu kwa kiapo kama alivyotabiriwa naye.

Hata hivyo, Yesu alikuwa amemuahidia atamuombea aongoke akaimarishe wenzake: "Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako" (Lk 22:31-32). Basi, alipotazamwa na Yesu akajuta kwa machozi mengi.

Baada ya ufufuko wa Yesu

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kifo cha Yesu, akawa wa kwanza kuingia kaburi lake tupu[6], tena wa kwanza kati ya mitume kutokewa na Yesu mfufuka[7] Jambo hilo ni kati ya kweli zilizotakiwa kuungamwa na Wakristo wa kwanza: [8].

Katika tokeo lingine katika ziwa Galilaya Yesu alimthibitisha katika uongozi wa kundi lake lote, kondoo na wanakondoo. Alifanya hivyo baada ya Petro kukiri mara tatu kwamba anampenda (Yoh 21:17): "Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda"[9].

Kadiri ya Matendo ya Mitume, kabla ya ujio wa Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste ya mwaka huo (30 au 33 B.K.) aliongoza wafuasi wake kuziba pengo la Yuda, mtume msaliti, kwa kumweka Mathia mahali pake [10].

Halafu akawa mhubiri shujaa [11][12] akachukua maamuzi muhimu sana kwa uenezi wa Kanisa, kama vile kubatiza akida Korneli na Wapagani wengine bila kudai watahiriwe kwanza [13].

Jambo hilo lilimvutia lawama kubwa, lakini zikaja kwisha hasa kwa mtaguso wa Yerusalemu (mwaka 49)[14].

Petro alikuwa maarufu kwa miujiza pia, kiasi cha kuponya wengi kwa kivuli chake tu [15].

Mfalme Herode Agripa I alipomuua Yakobo na kumfunga Petro ili kumuua pia, alitolewa gerezani kimuujiza [16]akahama Yerusalemu (mwaka 44 hivi)[17].

Katika Waraka kwa Wagalatia Paulo aliandika jinsi alivyomlaumu Petro wakiwa Antiokia kwa sababu ya kuficha msimamo wake wa kweli juu ya mahusiano na Wakristo wenye asili ya mataifa ili kuridhisha wale wenye asili ya Uyahudi.

Pia Paulo alimtaja katika Waraka wa kwanza kwa Wakorintho kama mtu mwenye wafuasi kati yao. Hivyo inaonekana alihubiri huko.

Waraka wa kwanza wa Petro unasema aliuandika akiwa Babuloni, jina la fumbo lililotumiwa na Wakristo kudokezea Roma. Kwa kuwa uliandikwa kwa Wakristo wachanga wa nyanda za juu za nchi inayoitwa leo Uturuki, inaonekana alikuwa amewahubiria kwanza.

Kifo chake

[hariri | hariri chanzo]

Yoh 21:18-19 inaeleza kifumbo kifodini ambacho Petro alimtukuza Mungu [18] mjini Roma, katika mtaa wa Vatikano. Ndipo linapoheshimiwa kaburi lake chini ya altare kuu ya kanisa kubwa kuliko yote duniani.

Kifo hicho, inasemekana kwa kusulubiwa kichwa chini, miguu juu, kinashuhudiwa hasa na waandishi mbalimbali wa karne za kwanza, kama vile Papa Klementi I kati ya miaka 95 na 97, Ignasi wa Antiokia, Dionisi wa Korintho, Irenei wa Lyons, Klementi wa Aleksandria, Tertuliani, Jeromu n.k.

Vitabu vinavyomhusu

[hariri | hariri chanzo]

Mbali ya Barua ya kwanza, ambayo aliiandika mwenyewe kwa msaada wa Sila na kukubaliwa mapema kama kitabu kitakatifu, vitabu vingine viliandikwa kwa jina la Petro kuanzia mwisho wa karne ya 1.

Kati yake kimoja kimeingia katika Agano Jipya kama Waraka wa pili wa Petro, wakati vingine vyote vilikataliwa na Kanisa, kama vile Injili ya Petro, Matendo ya Petro na Ufunuo wa Petro.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  1. Martyrologium Romanum: ex Decreto Sacrosancti oecumenici Concilii Vaticani II instauratum auctoritate Ioannis Pauli P.P. II promulgatum, Romae 2001, ISBN 8820972107
  2. 35 Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili. 36 Alipomwona Yesu akipita akasema, "Tazameni! Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu." 37 Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu. 38 Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, "Mnatafuta nini?" Nao wakamjibu, "Rabi (yaani Mwalimu), unakaa wapi?" 39 Yesu akawaambia, "Njoni, nanyi mtaona." Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata saa kumi jioni. 40 Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu. 41 Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, "Tumemwona Masiha" (maana yake Kristo). 42 Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, "Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa." (maana yake ni Petro, yaani, "Mwamba.")
  3. 18 Yesu alipokuwa anatembea kando ya ziwa Galilaya, aliwaona ndugu wawili wavuvi; Simoni (aitwae Petro) na Andrea, ndugu yake; walikuwa wakivua samaki kwa nyavu ziwani. 19 Basi, akawaambia, "Nifuateni, nami nitawafanya ninyi wavuvi wa watu." 20 Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.
  4. 1 Siku moja Yesu alikuwa amesimama kando ya ziwa Genesareti, na watu wengi walikuwa wamemzunguka wakisongana wanalisikiliza neno la Mungu. 2 Akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa; wavuvi wenyewe walikuwa wametoka, wanaosha nyavu zao. 3 Baada ya Yesu kuingia katika mashua moja, iliyokuwa ya Simoni, alimtaka Simoni aisogeze majini, mbali kidogo na ukingo wa ziwa. Akaketi, akafundisha umati wa watu akiwa ndani ya mashua. 4 Alipomaliza kufundisha, akamwambia Simoni, "Peleka mashua mpaka kilindini, mkatupe nyavu zenu mpate kuvua samaki." 5 Simoni akamjibu, "Bwana, tumejitahidi kuvua samaki usiku kucha bila kupata kitu, lakini kwa kuwa umesema, nitatupa nyavu." 6 Baada ya kufanya hivyo, wakavua samaki wengi, hata nyavu zao zikaanza kukatika. 7 Wakawaita wenzao waliokuwa katika mashua nyingine waje kuwasaidia. Wakaja, wakazijaza mashua zote mbili samaki, hata karibu zingezama. 8 Simoni Petro alipoona hayo, akapiga magoti mbele ya Yesu akisema, "Ondoka mbele yangu, ee Bwana, kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi!"Simoni pamoja na wenzake wote walishangaa kwa kupata samaki wengi vile. 10 Hali kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa wavuvi wenzake Simoni. Yesu akamwambia Simoni, "Usiogope; tangu sasa utakuwa ukivua watu." 11 Basi, baada ya kuzileta zile mashua ukingoni mwa ziwa, wakaacha yote, wakamfuata.
  5. 1 Ilikuwa kabla ya sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua kwamba saa yake ya kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ilikuwa imefika. Alikuwa amewapenda daima watu wake walioko duniani; naam, aliwapenda mpaka mwisho! 2 Basi, Yesu na wanafunzi wake walikuwa mezani kwa chakula cha jioni. Ibilisi alikwisha mtia Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti, nia ya kumsaliti Yesu. 3 Yesu alijua kwamba Baba alikuwa amemkabidhi kila kitu, na kwamba alikuwa ametoka kwa Mungu na anarudi kwa Mungu. 4 Basi, Yesu aliondoka mezani, akaweka kando vazi lake, akachukua kitambaa na kujifunga kiunoni. 5 Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuipangusa kwa kile kitambaa alichojifungia. 6 Basi, akamfikia Simoni Petro; naye Petro akasema, "Bwana, wewe utaniosha miguu mimi?" 7 Yesu akamjibu, "Huelewi sasa ninachofanya lakini utaelewa baadaye." 8 Petro akamwambia, "Wewe hutaniosha miguu kamwe!" Yesu akamjibu, "Nisipokuosha hutakuwa na uhusiano nami tena." 9 Simoni Petro akamwambia, "Bwana, nioshe, si miguu tu, bali na mikono yangu na kichwa pia." 10 Yesu akamwambia, "Aliyekwisha oga hana lazima ya kunawa isipokuwa miguu, maana amekwisha takata mwili wote. Ninyi mmetakata, lakini si nyote." 11 Yesu alimjua yule ambaye atamsaliti, ndiyo maana alisema: "Ninyi mmetakata, lakini si nyote.") 12 Alipokwisha waosha miguu na kuvaa tena vazi lake, aliketi mezani, akawaambia, "Je, mmeelewa hayo niliyowatendeeni? 13 Ninyi mwaniita Mwalimu na Bwana, nanyi mwasema vyema, kwa kuwa ndimi. 14 Basi, ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu, nimewaosha ninyi miguu, nanyi pia mnapaswa kuoshana miguu. 15 Nimewapeni mfano, ili nanyi pia mfanye kama nilivyowafanyieni. 16 Kweli nawaambieni, mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake, wala mtume si mkuu zaidi kuliko yule aliyemtuma. 17 Basi, ikiwa mwayajua hayo, mtakuwa na heri mkiyatekeleza.
  6. Yoh 20:1 Alfajiri na mapema Jumapili, kukiwa bado na giza, Maria Magdalene alikwenda kaburini, akaliona lile jiwe limeondolewa mlangoni pa kaburi. 2 Basi, akaenda mbio hadi kwa Petro na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, "Wamemwondoa Bwana kaburini, na wala hatujui walikomweka." 3 Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine wakaenda kaburini. 4 Wote wawili walikimbia lakini yule mwanafunzi mwingine alikimbia mbio zaidi kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini. 5 Alipoinama na kuchungulia ndani, aliona sanda, lakini hakuingia ndani. 6 Simoni Petro naye akaja akimfuata, akaingia kaburini; humo akaona sanda, 7 na kile kitambaa alichofungwa Yesu kichwani. Hicho kitambaa hakikuwekwa pamoja na hiyo sanda, bali kilikuwa kimekunjwa na kuwekwa mahali peke yake. 8 Kisha yule mwanafunzi mwingine aliyemtangulia kufika kaburini, akaingia pia ndani, akaona, akaaamini. 9 Walikuwa bado hawajaelewa Maandiko Matakatifu yaliyosema kwamba ilikuwa lazima afufuke kutoka wafu). 10 Basi, hao wanafunzi wakarudi nyumbani.
  7. 33 Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu: wakawakuta wale mitume kumi na mmoja na wale wengine waliokuwa pamoja nao, wamekusanyika 34 wakisema, "Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simoni." 35 Basi, hao wafuasi wawili wakawajulisha yale yaliyowapata njiani, na jinsi walivyomtambua katika kumega mkate. 36 Wanafunzi wote wawili walipokuwa wakiwaambia hayo, Yesu mwenyewe akasimama kati yao, akawaambia "Amani kwenu."
  8. 1Kor 15:1 Sasa ndugu, napenda kuwakumbusha ile Habari Njema niliyowahubirieni nanyi mkaipokea na kusimama imara ndani yake. 2 Kwa njia yake mnaokolewa, ikiwa mnayazingatia maneno niliyowahubirieni, na kama kuamini kwenu hakukuwa bure. 3 Mimi niliwakabidhi ninyi mambo muhimu sana ambayo mimi niliyapokea: kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na Maandiko Matakatifu; 4 kwamba alizikwa, akafufuka siku ya tatu kama ilivyoandikwa; 5 kwamba alimtokea Kefa, na baadaye aliwatokea wale kumi na wawili. 6 Kisha aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano kwa mara moja; wengi wao wanaishi bado, lakini baadhi yao wamekwisha kufa. 7 Baadaye alimtokea Yakobo kisha akawatokea mitume wote. 8 Baada ya wote, akanitokea hata mimi, mimi niliyekuwa kama mtu aliyezaliwa kabla ya wakati.
  9. Yoh 21:14 Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka kutoka wafu. 15 Walipokwisha kula, Yesu alimwuliza Simoni Petro, "Simoni, mwana wa Yohane! Je, wanipenda mimi zaidi kuliko hawa?" Naye akajibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba mimi nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza wana kondoo wangu." 16 Kisha akamwambia mara ya pili, "Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?" Petro akamjibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza kondoo wangu." 17 Akamwuliza mara ya tatu, "Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?" Hapo Petro akahuzunika kwa sababu alimwuliza mara ya tatu: "Wanipenda?" akamwambia, "Bwana, wewe wajua yote; wewe wajua kwamba mimi nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza kondoo wangu!
  10. Mdo 1:12 Kisha mitume wakarudi Yerusalemu kutoka mlima wa Mizeituni ulioko karibu kilomita moja kutoka mjini. 13 Walipofika mjini waliingia katika chumba ghorofani ambamo walikuwa wanakaa; nao walikuwa Petro, Yohane, Yakobo, Andrea, Filipo na Thoma, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo. 14 Hawa wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria mama yake Yesu, na ndugu zake. 15 Siku chache baadaye, kulikuwa na mkutano wa waumini, karibu watu mia moja na ishirini. Petro alisimama mbele yao, 16 akasema, "Ndugu zangu, ilikuwa lazima ile sehemu ya Maandiko Matakatifu itimie, sehemu ambayo Roho Mtakatifu, kwa maneno ya Daudi, alibashiri habari za Yuda ambaye aliwaongoza wale waliomtia Yesu nguvuni. 17 Yuda alikuwa mmoja wa kikundi chetu maana alichaguliwa ashiriki huduma yetu. 18 "Mnajua kwamba yeye alinunua shamba kwa zile fedha alizopata kutokana na kitendo chake kiovu. Akaanguka chini, akapasuka na matumbo yake yakamwagika nje. 19 Kila mtu katika Yerusalemu alisikia habari za tukio hilo na hivyo, kwa lugha yao, wakaliita lile shamba `Hekeli Dama`, maana yake, `Shamba la Damu.`) 20 Basi, imeandikwa katika kitabu cha Zaburi: `Nyumba yake ibaki mahame; mtu yeyote asiishi ndani yake.` Tena imeandikwa: `Mtu mwingine achukue nafasi yake katika huduma hiyo.`21 Kwa hiyo, ni lazima mtu mwingine ajiunge nasi kama shahidi wa ufufuo wake Bwana Yesu. Anapaswa kuwa mmoja wa wale waliokuwa katika kundi letu wakati wote Bwana alipokuwa anasafiri pamoja nasi, tangu wakati Yohane alipokuwa anabatiza mpaka siku ile Yesu alipochukuliwa kutoka kwetu kwenda mbinguni." 22 [] 23 Basi, wakataja majina ya watu wawili; wa kwanza Yosefu aliyeitwa Barsaba (au pia Yusto), na wa pili Mathia. 24 Kisha wakasali: "Bwana, wewe unajua mioyo ya watu wote. Hivyo, utuonyeshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua 25 ili achukue nafasi hii ya huduma ya kitume aliyoacha Yuda akaenda mahali pake mwenyewe." 26 Hapo, wakapiga kura; kura ikampata Mathia, naye akaongezwa katika idadi ya wale mitume wengine kumi na mmoja.
  11. Mdo 2:1 Siku ya Pentekoste ilipofika, waumini wote walikuwa wamekusanyika pamoja. 2 Ghafla, sauti ikasikika kutoka angani; sauti iliyokuwa kama ya upepo mkali, ikajaza ile nyumba yote walimokuwa wamekaa. 3 Kisha, vikatokea vitu vilivyoonekana kama ndimi za moto, vikagawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao. 4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali kadiri Roho alivyowawezesha. 5 Na huko Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu, waliotoka katika kila nchi duniani. 6 Waliposikia sauti hiyo, kundi kubwa la watu lilikusanyika. Wote walishtuka sana kwani kila mmoja wao aliwasikia hao waumini wakisema kwa lugha yake mwenyewe. 7 Walistaajabu na kushangaa, wakisema, "Je, hawa wote tunaowasikia wakisema hivi, si wenyeji wa Galilaya? 8 Imekuwaje, basi, kwamba kila mmoja wetu anawasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe? 9 Baadhi yetu ni Waparthi, Wamedi na Waelami; wengine ni wenyeji wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na Asia, 10 Frugia na Pamfulia, Misri na sehemu za Libya karibu na Kurene; wengine wetu ni wageni kutoka Roma, 11 Wayahudi na watu walioongokea dini ya Kiyahudi; wengine wametoka Krete na Arabia. Sisi sote tunasikia wakisema kwa lugha zetu wenyewe mambo makuu ya Mungu." 12 Wote walishangaa na kufadhaika huku wakiulizana, "Hii ina maana gani?" 13 Lakini wengine wakawadhihaki wakisema, "Watu hawa wamelewa divai mpya!" 14 Lakini Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza kuwahutubia watu kwa sauti kubwa: "Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa makini maneno yangu. 15 Watu hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu asubuhi? 16 Ukweli ni kwamba jambo hili ni lile alilosema nabii Yoeli: 17 `Katika siku zile za mwisho, asema Bwana, nitawamiminia binadamu wote Roho wangu. Watoto wenu, wanaume kwa wanawake, watautangaza ujumbe wangu; vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto. 18 Naam, hata watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, nitawamiminia Roho wangu, siku zile, nao watautangaza ujumbe wangu. 19 Nitatenda miujiza juu angani, na ishara chini duniani; kutakuwa na damu, moto na moshi mzito; 20 jua litatiwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kutokea ile siku kuu na tukufu ya Bwana. 21 Hapo, yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.` 22 "Wananchi wa Israeli, sikilizeni maneno haya! Yesu wa Nazareti alikuwa mtu ambaye mamlaka yake ya kimungu yalithibitishwa kwenu kwa miujiza, maajabu na ishara Mungu alizofanya kati yenu kwa njia yake, kama mnavyojua. 23 Kufuatana na mpango wake mwenyewe Mungu alikwisha amua kwamba Yesu angetiwa mikononi mwenu; nanyi mkamuua kwa kuwaachia watu wabaya wamsulubishe. 24 Lakini Mungu alimfufua kutoka wafu akamwokoa katika maumivu ya kifo kwa maana haingewezekana kabisa kifo kimfunge. 25 Maana Daudi alisema juu yake hivi: `Nilimwona Bwana mbele yangu daima; yuko nami upande wangu wa kulia, na hivyo sitatikisika. 26 Kwa hiyo, moyo wangu ulifurahi; tena nilipiga vigelegele vya furaha. Mwili wangu utakaa katika tumaini; 27 kwa kuwa hutaiacha roho yangu katika kuzimu, wala kumruhusu mtakatifu wako aoze. 28 Umenionyesha njia za kuufikia uzima, kuwako kwako kwanijaza furaha!` 29 "Ndugu zangu, napenda kuwaambieni waziwazi juu ya mambo yaliyompata Daudi, babu yetu. Yeye alikufa, akazikwa, tena kaburi lake liko papa hapa petu mpaka leo. 30 Lakini kwa vile Daudi alikuwa nabii, alijua kuwa Mungu alimwapia kiapo kwamba atamtawaza mmoja wa uzawa wake kuwa mfalme mahali pake. 31 Daudi aliona kabla mambo yatakayofanywa na Mungu na hivyo akasema juu ya ufufuo wa Kristo wakati aliposema: `Hakuachwa kuzimu, mwili wake haukuoza.` 32 Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu na sisi sote ni mashahidi wa tukio hilo. 33 Yesu aliinuliwa juu mpaka upande wa kulia wa Mungu, akapokea kutoka kwa Baba ile zawadi aliyoahidi yaani Roho Mtakatifu; na mnachoona sasa na kusikia ni mmiminiko wa huyo Roho. 34 Maana Daudi mwenyewe, hakupanda mpaka mbinguni; ila yeye alisema: `Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia, 35 hadi nitakapowafanya adui zako kibao cha kukanyagia miguu yako.` 36 "Watu wote wa Israeli wanapaswa kufahamu kwa hakika kwamba huyo Yesu mliyemsulubisha ninyi, ndiye huyo ambaye Mungu amemfanya kuwa Bwana na Kristo." 37 Basi, watu waliposikia hayo, walichomwa moyo, wakawauliza Petro na wale mitume wenzake: "Ndugu zetu, tufanye nini?" 38 Petro akajibu, "Tubuni na kila mmoja wenu abatizwe kwa jina la Yesu Kristo ili mpate kuondolewa dhambi zenu na kupokea ile zawadi ya Roho Mtakatifu. 39 Maana, ahadi ile ilikuwa kwa ajili yenu, kwa ajili ya watoto wenu, kwa ajili ya wote wanaokaa mbali; na kwa ajili ya kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita kwake." 40 Kwa maneno mengine mengi, Petro alisisitiza na kuwahimiza watu akisema, "Jiokoeni katika kizazi hiki kiovu." 41 Wengi waliyakubali maneno yake, wakabatizwa. Watu wapatao elfu tatu wakaongezeka katika kile kikundi siku hiyo.
  12. Mdo 3:1 Siku moja, saa tisa alasiri, Petro na Yohane walikuwa wanakwenda Hekaluni, wakati wa sala. 2 Na pale karibu na mlango wa Hekalu uitwao "Mlango Mzuri", palikuwa na mtu mmoja, kiwete tangu kuzaliwa. Watu walimbeba huyo mtu kila siku na kumweka hapo ili aombe chochote kwa wale waliokuwa wakiingia Hekaluni. 3 Alipowaona Petro na Yohane wakiingia Hekaluni, aliwaomba wampe chochote. 4 Petro na Yohane walimkodolea macho, naye Petro akamwambia, "Tutazame!" 5 Naye akawageukia, akitazamia kupata kitu kutoka kwao. 6 Kisha Petro akamwambia, "Sina fedha wala dhahabu lakini kile nilicho nacho nitakupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!" 7 Halafu, akamshika mkono wa kulia, akamwinua. Papo hapo miguu na magoti yake yakapata nguvu. 8 Akaruka, akasimama na kuanza kutembea. Halafu akaingia pamoja nao Hekaluni, akitembea na kurukaruka huku akimtukuza Mungu. 9 Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu Mungu. 10 Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba karibu na ule "Mlango Mzuri" wa Hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze kuelewa yaliyompata. 11 Watu wote, wakiwa na mshangao mkubwa wakaanza kukimbilia mahali palipoitwa "Ukumbi wa Solomoni," ambapo yule mtu alikuwa bado anaandamana na Petro na Yohane. 12 Basi, Petro alipowaona watu hao akawaambia, "Wananchi wa Israeli, kwa nini mnashangazwa na jambo hili? Mbona mnatukodolea macho kana kwamba ni kwa nguvu zetu au utakatifu wetu sisi wenyewe tumemfanya mtu huyu aweze kutembea? 13 Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza Yesu mtumishi wake. Yeye ndiye yuleyule mliyemtia mikononi mwa wakuu na kumkataa mbele ya Pilato hata baada ya Pilato kuamua kumwacha huru. 14 Alikuwa mtakatifu na mwema; lakini ninyi mlimkataa, mkataka mtu mwingine aliyekuwa muuaji afunguliwe. 15 Basi, mlimuua yule ambaye ni chanzo cha uzima. Lakini Mungu alimfufua, na sisi ni mashahidi wa tukio hilo. 16 Jina la Yesu na imani katika jina hilo ndivyo vilivyompa nguvu mtu huyu mnayemwona na kumfahamu. Imani kwa Yesu ndiyo iliyomponya kabisa mtu huyu kama mnavyoona nyote. 17 "Sasa ndugu zangu, nafahamu kwamba ninyi na wakuu wenu mlitenda hayo kwa sababu ya kutojua kwenu. 18 Lakini ndivyo Mungu alivyotimiza yale aliyotangaza zamani kwa njia ya manabii wote, kwamba ilikuwa lazima Kristo wake ateseke. 19 Basi, tubuni mkamrudie Mungu ili afute dhambi zenu. 20 Fanyeni hivyo ili Bwana awape nyakati za kuburudika rohoni na kuwaletea yule Kristo aliyemteua ambaye ndiye Yesu. 21 Ni lazima yeye abaki huko mbinguni mpaka utakapofika wakati wa kurekebishwa vitu vyote, kama Mungu alivyosema kwa njia ya manabii wake watakatifu wa tangu zamani. 22 Kwa maana Mose alisema, `Bwana Mungu wenu atawapelekeeni nabii kama mimi kutoka kati yenu ninyi wenyewe. 23 Yeyote yule ambaye hatamsikiliza nabii huyo atatengwa mbali na watu wa Mungu na kuangamizwa.` 24 Manabii wote, kuanzia Samweli na wale waliomfuata, walitangaza habari za mambo haya ambayo yamekuwa yakitendeka siku hizi. 25 Ahadi zile Mungu alizotoa kwa njia ya manabii ni kwa ajili yenu; na mnashiriki lile agano Mungu alilofanya na babu zenu, kama alivyomwambia Abrahamu: `Kwa njia ya wazawa wako, jamaa zote za dunia zitabarikiwa.` 26 Basi, ilikuwa kwa ajili yenu kwanza kwamba Mungu alimfufua mtumishi wake, alimtuma awabariki kwa kumfanya kila mmoja wenu aachane kabisa na maovu yake."
  13. Mdo 10:1 Kulikuwa na mtu mmoja huko Kaisarea aitwaye Kornelio, Jemadari wa kikosi kimoja kiitwacho "Kikosi cha Italia." 2 Alikuwa mtu mwema; naye pamoja na jamaa yake yote walimcha Mungu; alikuwa anafanya mengi kusaidia maskini wa Kiyahudi na alikuwa anasali daima. 3 Yapata saa tisa mchana, aliona dhahiri katika maono malaika wa Mungu akiingia ndani na kumwambia, "Kornelio!" 4 Kornelio alimkodolea macho huyo malaika kwa hofu, akamwambia, "Kuna nini Mheshimiwa?" Huyo malaika akamwambia, "Mungu amezipokea sala na sadaka zako kwa maskini. 5 Sasa, watume watu Yopa wakamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro. 6 Yeye yumo nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko karibu na bahari." 7 Huyo malaika aliyesema hayo alipokwisha kwenda zake, Kornelio aliwaita watumishi wawili wa nyumbani na mmoja wa askari zake ambaye alikuwa mcha Mungu, 8 akawaeleza yote yaliyotukia, akawatuma Yopa. 9 Kesho yake, hao watu watatu wakiwa bado safarini, lakini karibu kufika Yopa, Petro alipanda juu ya paa la nyumba yapata saa sita mchana ili kusali. 10 Aliona njaa, akatamani kupata chakula. Chakula kilipokuwa kinatayarishwa, alipatwa na usingizi mzito akaona maono. 11 Aliona mbingu zimefunguliwa na kitu kama shuka kubwa inateremshwa chini ikiwa imeshikwa pembe zake nne. 12 Ndani ya shuka hiyo kulikuwa na kila aina ya wanyama: wanyama wenye miguu minne, wanyama watambaao na ndege wa angani. 13 Akasikia sauti ikimwambia: "Petro, amka uchinje, ule!" 14 Petro akajibu, "La, Bwana; mimi sijaonja kamwe chochote ambacho ni najisi au kichafu." 15 Ile sauti ikasikika tena ikimwambia: "Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa!" 16 Jambo hili lilifanyika mara tatu, kisha ile shuka ikarudishwa juu mbinguni. 17 Petro alipokuwa bado anashangaa juu ya maana ya hilo maono alilokuwa ameliona, wale watu waliotumwa na Kornelio, baada ya kuigundua nyumba ya Simoni, walifika mlangoni, 18 Wakaita kwa sauti: "Je, kuna mgeni humu aitwaye Simoni Petro?" 19 Petro alikuwa bado anajaribu kuelewa lile maono, na hapo Roho akamwambia, "Sikiliza! kuna watu watatu hapa, wanakutafuta. 20 Shuka upesi na wala usisite kwenda pamoja nao kwa maana ni mimi niliyewatuma." 21 Basi, Petro akateremka chini, akawaambia hao watu, "Mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja?" 22 Wao wakamjibu, "Jemadari Kornelio ambaye ni mtu mwema, mcha Mungu na mwenye kuheshimika mbele ya Wayahudi wote ametutuma. Aliambiwa na malaika mtakatifu akualike nyumbani kwake ili asikilize chochote ulicho nacho cha kusema." 23 Petro akawaalika ndani, akawapa mahali pa kulala usiku ule. Kesho yake, Petro alianza safari pamoja nao, na baadhi ya ndugu wa huko Yopa walifuatana naye. 24 Siku ya pili yake, walifika Kaisarea na huko Kornelio alikuwa anawangojea pamoja na jamaa na marafiki aliokuwa amewaalika. 25 Petro alipokuwa anaingia, Kornelio alitoka nje kumlaki, akapiga magoti mbele yake na kuinama chini kabisa. 26 Lakini Petro alimwinua, akamwambia, "Simama, kwa maana mimi ni binadamu tu." 27 Petro aliendelea kuongea na Kornelio wakiwa wanaingia nyumbani ambamo aliwakuta watu wengi wamekusanyika. 28 Petro akawaambia, "Ninyi wenyewe mnajua kwamba Myahudi yeyote amekatazwa na Sheria yake ya dini kushirikiana na watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amenijulisha nisimfikirie mtu yeyote kuwa najisi au mchafu. 29 Kwa sababu hiyo, mliponiita nimekuja bila kusita. Basi, nawaulizeni: kwa nini mmeniita?" 30 Kornelio akasema, "Siku tatu zilizopita saa kama hii, saa tisa alasiri, nilikuwa nikisali chumbani mwangu. Ghafla, mtu aliyekuwa amevaa mavazi yenye kun`gaa alisimama mbele yangu, 31 akasema: `Kornelio! Sala yako na sadaka zako kwa maskini vimekubaliwa na Mungu. 32 Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petroi; yuko nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi karibu na bahari.` 33 Kwa hiyo nilikutumia ujumbe bila kuchelewa, nawe umefanya vyema kuja. Sasa, sisi tuko mbele ya Mungu, kusikiliza chochote ambacho bwana amekuamuru kusema." 34 Hapo Petro akaanza kusema: "Sasa nimetambua kwamba hakika Mungu hana ubaguzi. 35 Mtu wa taifa lolote anayemcha Mungu na kutenda haki anapokelewa naye. 36 Huu ndio ule ujumbe Mungu alioupeleka kwa watu wa Israeli, akitangaza Habari Njema iletayo amani kwa njia ya Yesu Kristo ambaye ni Bwana wa wote. 37 Ninyi mnajua jambo lililotukia katika nchi yote ya Wayahudi kuanzia Galilaya baada ya ule ubatizo aliohubiri Yohane. 38 Mnajua Yesu wa Nazareti na jinsi Mungu alivyomteua kwa kummiminia Roho Mtakatifu na nguvu. Mungu alikuwa pamoja naye; yeye alikwenda huko na huko akitenda mema na kuwaponya wote waliokuwa wamevamiwa na Ibilisi. 39 Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyotenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu. Walimuua kwa kumtundika msalabani; 40 lakini Mungu alimfufua siku ya tatu, akamfanya aonekane 41 si kwa watu wote ila kwa wale Mungu aliokwisha wachagua wawe mashahidi wake, yaani sisi tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka wafu. 42 Alituamuru kuihubiri Habari Njema kwa watu wote na kushuhudia kwamba yeye ndiye aliyeteuliwa na Mungu awe Mwamuzi wa wazima na wafu. 43 Manabii wote waliongea juu yake kwamba kila mtu atakayemwamini atasamehewa dhambi zake zote kwa jina lake." 44 Wakati Petro alipokuwa bado anasema maneno hayo, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wanasikiliza ujumbe huo. 45 Wale Wayahudi waumini waliokuja pamoja na Petro kutoka Yopa walishangaa kuona kuwa Mungu aliwamiminia zawadi ya Roho Mtakatifu watu wa mataifa mengine pia; 46 maana waliwasikia wakiongea kwa lugha mbalimbali wakimtukuza Mungu. Hapo Petro akasema, 47 "Watu hawa wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi wenyewe tulivyompokea. Je, kuna yeyote atakayeweza kuwazuia wasibatizwe kwa maji?" 48 Basi, akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Kisha wakamwomba akae nao kwa siku chache.
  14. Mdo 15:6 Basi, mitume na wazee walifanya mkutano maalum wa kuchunguza jambo hilo. 7 Baada ya majadiliano marefu, Petro alisimama, akasema, "Ndugu zangu, ninyi mnafahamu kwamba hapo awali Mungu alipenda kunichagua mimi miongoni mwenu niihubiri Habari Njema, ili watu wa mataifa wapate kusikia na kuamini. 8 Naye Mungu anayejua mioyo ya watu, alithibitisha kwamba amewakubali kwa kuwapa nao Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi. 9 Hakufanya ubaguzi wowote kati yetu na wao; aliitakasa mioyo yao kwa imani. 10 Sasa basi, kwa nini kumjaribu Mungu kwa kuwatwika hao waumini mzigo ambao wala babu zetu, wala sisi hatukuweza kuubeba? 11 Isiwe hivyo, ila tunaamini kwamba, sisi kama vile wao, tunaokolewa kwa njia ya neema ya Bwana Yesu."
  15. Mdo 5:12 Mitume walifanya miujiza na maajabu mengi kati ya watu. Waumini walikuwa wakikutana pamoja katika ukumbi wa Solomoni. 13 Mtu yeyote mwingine ambaye hakuwa mwamini hakuthubutu kujiunga nao. Hata hivyo, watu wengine wasiokuwa wa imani hiyo waliwasifu. 14 Idadi ya watu waliomwamini Bwana, wanaume kwa wanawake, iliongezeka zaidi na zaidi. 15 Kwa sababu hiyo, watu walikuwa wakipeleka wagonjwa barabarani na kuwalaza juu ya vitanda na mikeka ili Petro akipita, walau kivuli chake kiwaguse baadhi yao. 16 Watu wengi walifika kutoka katika miji ya kando kando ya Yerusalemu, wakiwaleta wagonjwa wao na wale waliokuwa na pepo wachafu, nao wote wakaponywa.
  16. Mdo 12:1 Karibu wakati huohuo, mfalme Herode alianza kuwatesa baadhi ya Wakristo. 2 Alimwua kwa upanga Yakobo ndugu yake Yohane. 3 Alipoona kuwa kitendo hiki kiliwapendeza Wayahudi, aliendelea, akamkamata Petro. (Hiyo ilifanyika wakati wa sikukuu ya Mikate Isiyotiwa chachu.) 4 Baada ya kutiwa nguvuni, Petro alifungwa gerezani, akawekwa chini ya ulinzi wa vikundi vinne vya askari wannewanne. Herode alikusudia kumtoa hadharani baada ya sikukuu ya Pasaka. 5 Basi, Petro alipokuwa gerezani, kanisa lilikuwa linamwombea kwa Mungu kwa moyo. 6 Usiku, kabla ya siku ile ambayo Herode angemtoa Petro hadharani, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili. Alikuwa amefungwa minyororo miwili, na walinzi walikuwa wanalinda lango la gereza. 7 Ghafla, malaika wa Bwana akasimama karibu naye na mwanga ukaangaza kile chumba cha gereza. Malaika akamgusa akisema, "Amka upesi!" Mara ile minyororo ikaanguka kutoka katika mikono yake. 8 Malaika akamwambia, "Jifunge mshipi wako, vaa viatu vyako." Akafanya hivyo. Kisha huyo malaika akamwambia, "Vaa koti lako, unifuate." 9 Petro akamfuata nje lakini hakujua kama hayo yaliyofanywa na huyo malaika yalikuwa ya kweli; alidhani alikuwa anaota ndoto. 10 Walipita kituo cha kwanza cha ulinzi na cha pili, halafu wakafika kwenye mlango wa chuma wa kuingilia mjini. Huo mlango ukawafungukia wenyewe, nao wakatoka nje. Wakawa wanatembea katika barabara moja na mara yule malaika akamwacha Petro peke yake. 11 Hapo ndipo Petro alipotambua yaliyotukia, akasema, "Sasa najua kwa hakika kwamba Bwana amemtuma malaika wake akaniokoa kutoka katika mkono wa Herode na kutoka katika mambo yale yote watu wa Israeli waliyotazamia."
  17. Mdo 12:12 Alipotambua hivyo alikwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Maria mama yake Yohane aitwaye Marko. Humo watu wengi walikuwa wamekusanyika wakisali. 13 Petro alibisha mlango wa nje na mtumishi mmoja msichana aitwaye Roda, akaenda mlangoni kuitikia. 14 Huyo msichana aliitambua sauti ya Petro akafurahi mno, hata badala ya kuufungua ule mlango, akakimbilia ndani na kuwaambia kwamba Petro alikuwa amesimama nje mlangoni. 15 Wakamwambia yule msichana, "Una wazimu!" Lakini yeye akasisitiza kwamba ilikuwa kweli. Nao wakamwambia, "Huyo ni malaika wake." 16 Wakati huo Petro alikuwa anaendelea kupiga hodi. Mwishowe walifungua mlango, wakamwona, wakashangaa. 17 Petro aliwaashiria kwa mkono wakae kimya, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa gerezani. Kisha akawaambia watoe taarifa ya jambo hilo kwa Yakobo na wale ndugu wengine, halafu akatoka akaenda mahali pengine.
  18. 18 Kweli nakwambia, ulipokuwa kijana ulizoea kujifunga mshipi na kwenda kokote ulikotaka. Lakini utakapokuwa mzee utanyosha mikono yako, na mtu mwingine atakufunga na kukupeleka usikopenda kwenda." 19 (Kwa kusema hivyo, alionyesha jinsi Petro atakavyokufa na kumtukuza Mungu.) Kisha akamwambia, "Nifuate."
  • Thenashara, Mitume Kumi na Wawili – tafsiri ya P. A. Bunju – Toleo la pili – ed. Benedictine Publications Ndanda Peramiho – Ndanda 1984 – ISBN 9976-63-030-1
  • Stefano Kaombe, Mfahamu Mtakatifu Petro anavyosimuliwa na Wainjili - Dar es Salaam 2017 - ISBN 9987-474-20-9

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mtume Petro kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.