Jeromu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Mt. Jeromu alivyochorwa na Caravaggio.

Jeromu au Yeronimo (Strido, leo nchini Korasya 347 - Bethlehemu, Israeli, 420) alikuwa padri, mmonaki na mtaalamu wa Biblia, aliyemudu vizuri lugha zote za kitabu hicho pamoja na Kilatini hata akawa mwandishi bora wa lugha hiyo kati ya mababu wa Kanisa.

Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Mwaka 1298 Papa Bonifasi VIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa tarehe 30 Septemba.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa mwaka 347 huko Strido, sehemu za Dalmazia .

Alisomea Roma miaka ya 360 - 367, akijipatia elimu ya hali ya juu, aliyoiendeleza maisha yake yote, hata kwa safari nyingi magharibi na mashariki zilizomwezesha kufahamiana na watu wengi maarufu.

Alibatizwa huko Roma akiwa na umri wa miaka 25, akaendelea moja kwa moja kupambana kiume na tabia yake ngumu iliyochanganya ukali na wepesi wa kulia machozi, unyofu na elekeo la kinyongo, maisha magumu na hisia kali, uadilifu na hamaki, hisani na uchungu wa maneno.

Akishika kazi, saumu, sala na makesha, alivuta wengi kumfuata Kristo kwa karibu zaidi.

Miaka 375 - 377 katika jangwa la Kalchis alifundishwa Kiebrania na Myahudi aliyeongokea Ukristo.

Mwaka 379 kisha kupewa upadri na askofu Paulino wa Antiokia alikwenda Konstantinopoli alipokamilisha ujuzi wake wa lugha ya Kigiriki chini ya Gregori wa Nazianzo.

Baada ya kuishi kama mmonaki miaka 3 akarudi Roma (382) na kuanza kutafsiri vitabu vya Origene, mpaka alipoteuliwa na Papa Damaso I kuwa karani na mshauri wake.

Wakati huo alikamilisha ujuzi wake wa Kiebrania kwa msaada wa mwalimu wa dini ya Kiyahudi, na baada yake akazidi kutegemea elimu ya Kibiblia ya dini hiyo badala ya mbinu za Origene. Ndiyo sababu alikataa vitabu vya Deuterokanoni.

Baada ya papa huyo kufa (385), upinzani dhidi yake ulizidi, akahamia Mashariki ya Kati, alipoanzisha na kuongoza monasteri kadhaa za kike na za kiume zenye elimu ya hali ya juu, akaishi katika mojawapo huko Bethlehemu, akitafsiri na kufafanua Biblia hadi dakika yake ya mwisho (420).

'Vulgata'[hariri | hariri chanzo]

Vulgata, tafsiri ya kwanza ya Biblia ya Kikristo nzima katika Kilatini ndiyo kazi yake muhimu zaidi. Aliianza kwa agizo la papa Damaso I mwaka 382, akaimaliza baada ya miaka 23. Tafsiri hiyo ilitumika kama msingi wa tafsiri nyingine nyingi hadi karne XX. Hata hivyo tangu wakati wake ilikosolewa sana kwa kufuata mno msimamo wa Uyahudi.

Pia alitafsiri vitabu vingine, alitunga hotuba, barua pamoja na vitabu juu ya maisha ya watu maarufu (yeye akiwa mmojawao) na vya kupinga mafundisho ya wengine.

Sala yake[hariri | hariri chanzo]

Ee Bwana, umetupatia Neno lako kama nuru ambayo iangazie njia yetu; utujalie tulitafakari Neno lako na kufuata mafundisho yake hivi kwamba tuone hiyo nuru inazidi kuangaza hadi adhuhuri, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

Vyanzo[hariri | hariri chanzo]

  • J.N.D. Kelly, "Jerome: His Life, Writings, and Controversies" (Peabody, MA 1998)
  • S. Rebenich, "Jerome" (London and New York, 2002)

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Maandishi kwa Kilatini[hariri | hariri chanzo]

Google Books' Facsimiles[hariri | hariri chanzo]

Tafsiri za Kiingereza[hariri | hariri chanzo]