Yohane wa Msalaba
Yohane wa Msalaba ni jina la kitawa la Juan de Yepes Álvarez, padri wa Kanisa Katoliki na mwanzilishi (pamoja na Teresa wa Yesu) wa urekebisho wa shirika la Wakarmeli maarufu kama Wakarmeli Peku.
Anaheshimiwa kama mtakatifu na mwalimu wa Kanisa.
Sikukuu yake ni tarehe 14 Desemba.
Yaliyomo |
[hariri] Maisha
Yohane alizaliwa Fontiveros, kijiji cha Castilia (Hispania, tarehe 24 Juni 1542 akafariki Ubeda tarehe 14 Desemba 1591.
Baba yake, Gonzalo de Yepes, wa ukoo maarufu, alifukuzwa na familia yake na kunyimwa urithi kwa sababu ya kumuoa mfumaji maskini, Catalina Álvarez.
Tangu utotoni alielekea huruma kwa maskini na hasa sala.
Kati ya 1551 na 1559 alipata elimu na ufundi kwenye "Colegio de los doctrinos" huko Medina del Campo (Valladolid), ambapo familia yake ilikuwa imehamia.
Baadaye akawa seremala, mshonaji, mchoraji, mchongaji, nesi msaidizi namtumishi wa altare.
Mwaka 1563 alijiunga na shirika la Wakarmeli, na kati ya 1564 na 1568 akasomea chuo kikuu cha Salamanca.
Mwaka 1567 alipata upadirisho akakutana na Teresa wa Yesu, ambaye alimpata amuunge mkono katika kurekebisha shirika hilo; upande wake Teresa alianza kumheshimu sana akamuita "baba wa roho" yake.
Tarehe 9 Agosti 1568, alikwenda Valladolid ilipoanzishwa monasteri ya kwanza ya Masista Wakarmeli Peku akabaki huko hadi Oktoba ili kujifunza maisha ya urekebisho, halafu akaenda Duruelo (Segovia), akageuza nyumba ya wakulima kuwa konventi ya kwanza ya Wakarmeli Peku (28 novembre).
Kati ya mateso ya kimwili na ya kiroho yaliyompata kutokana na kupigania urekebisho, mojawapo ni lile la kufungwa kwa miezi minane katika gereza la shirika la Toledo (kuanzia tarehe 2 Desemba 1577 hadi alipotoroka tarehe 17 Agosti 1578).
Hata hivyo humo aliangaziwa kutunga baadhi ya mashairi yake bora, yaliyompatia nafasi kati wa washairi mashuhuri wa lugha ya Kihispania.
Miaka ya mwisho ya maisha yake alijikuta ameacha na wafuasi wake walio wengi.
Tarehe 28 Septemba 1591 akiwa mgonjwa alisafiri kwenda Úbeda (Jaén), alipofariki usiku kati ya tarehe 13 na 14 dicembre 1591.
[hariri] Teolojia yake
Pamoja na kuwa mshairi, Yohane alikuwa hasa mwanateolojia, aliyetunga vitabu mbalimbali kuhusu maisha ya Kiroho, yaani sala na safari ya kiroho ya kumuelekea Mungu kwa njia ya mkato kupitia (hatua ya utakaso, hatua ya mwanga na [[hatua ya muungano).
Kufuatana na mapokeo ya Ukristo, alifundisha namna ya kubandukana na wote na vyote ili kuungana na Mungu tu aliye «mwanga wenye giza na giza angavu», kwa kuwa mwanga wake ni mkali mno kwa macho yetu mabovu.
Mojawapo ya semi zake ilikuwa kwamba: «Mungu anamnyenyekesha sana mtu ili kumuinua sana».
[hariri] Maandishi na sifa yake baada ya kifo
- Wimbo wa Kiroho
- Usiku wenye giza wa roho
- Kupanda mlima Karmeli
- Mwali hai wa upendo
- Mawazo juu ya upendo na amani
- Barua
Maandishi yake yalitolewa kwa mara ya kwanza mwaka 1618, akatangazwa mwenye heri mwaka 1675, halafu mtakatifu na papa Benedikto XIII mwaka 1726 na hatimaye mwalimu wa Kanisa na Papa Pius XI mwaka 1926.
[hariri] Kulinganisha maandishi yake na yale ya Teresa wa Yesu
Tangu tusome mara ya kwanza maandishi ya Teresa wa Yesu na Yohane wa Msalaba, ni rahisi tutambue tofauti ambazo zimesisitizwa mara nyingi. Basi, tuone hasa asili yake.
Zinatokana na tofauti za mitazamo yao. Teresa alitegemea mang’amuzi yake binafsi, akidokeza neema za pekee alizojaliwa (njozi n.k.) asiwe makini kuzitofautisha na mambo yaliyo ya lazima katika “makao saba” ya jumba la Kiroho. Hivyo alitia maanani kuliko wengine matukio ya kihisi, ya nje na ya ziada yanayoweza yakaendana na sala ya kumiminiwa; vilevile alisisitiza kuzingatia [[[ubinadamu]] wa Yesu.
Yohane pia alisema kwa mang’amuzi yake binafsi na ya watu aliowaongoza, lakini hakuyataja, akijitahidi kuyachimba kiteolojia, jambo ambalo ni muhimu ili kutofautisha yaliyo ya kawaida na yaliyo ya ziada. Alieleza sababu za hali za sala kwa mafundisho juu ya maadili ya Kimungu na ya vipaji vya Roho Mtakatifu vinavyoendana nayo.
Kwa mtazamo huo alizingatia yaliyo ya lazima katika safari ya kuelekea utakatifu, hasa matakaso ya Kimungu yanayohitajika kwa usafi kamili wa upendo. Hivyo hakuelekea kujali neema za pekee zinazoendana pengine na sala ya kumiminiwa, wala hakusisitiza kuzingatia ubinadamu wa Yesu, akilenga moja kwa moja shabaha kuu ya sala ya kumiminiwa, yaani Mungu aliyemo mwetu, ambaye tunamfikia katika giza la imani kwa njia ya ujuzi ambao anatumiminia na unafanana na mang’amuzi.
Kwa kufanya hivyo amekamilisha maandishi ya Teresa na kutusaidia tuyaelewe.
Hata hivyo, chini ya tofauti hizo kuna msingi mmoja, kwa kuwa Teresa alijua vya kutosha mang’amuzi ya wafuasi wake aweze kuelewa na kueleza nini inatokea kwa kawaida kwa watu wanaopitia hayo makao saba. Tukitumia maelekezo aliyoyatoa huko na huko tunaweza kubainisha zaidi yaliyo ya lazima na yaliyo ya ziada.
Kimsingi watakatifu hao walielewa vilevile sala ya kumiminiwa, muungano na Mungu unaotokana nayo, na matakaso ya Kimungu yanayohitajika ili kuufikia ule kamili.
Ikifaa kuonyesha tofauti zao, inafaa zaidi kuonyesha wanavyolingana na kutambua teolojia inavyoweza kusaidia katika masuala hayo magumu.
|
|||||