Bonaventura wa Bagnoregio

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Bonaventura alivyochorwa na Francisco de Zurbarán

Mtakatifu Bonaventura (takriban 1221 - 15 Julai, 1274) alikuwa mtawa wa shirika la Ndugu Wadogo, halafu padri, askofu na kardinali, kisha kufa alitangazwa mtakatifu na mwalimu wa Kanisa. Kumbukumbu yake inaadhimishwa na Kanisa Katoliki kila tarehe 15 Julai.

Yaliyomo

[hariri] Maisha yake kabla ya kuwa mtumishi mkuu wa shirika

Mwaka aliozaliwa haujulikani kwa hakika, bali ni kati ya 1217 na 1221. Mahali ni Civita di Bagnoregio, karibu na Viterbo. Wazazi wake walikuwa mganga Yohane Fidanza na Maria wa Ritello; kwanza aliitwa kwa jina la baba yake, lakini alipoingia utawani aliitwa Bonaventura (yaani Bahati njema).

Alisoma (1235-1253) akafundisha (1253-1257) katika chuo kikuu cha Paris (Ufaransa), akifuata falsafa ya Plato na Agostino wa Hippo.

Mtumishi mkuu wa shirika Yohane wa Parma (1247-1257), alipolazimika kujiuzulu, ingawa Mkutano mkuu ulitaka aendelee, hakurudi nyuma. Hatimaye walimuomba walau amchague mwandamizi wake, naye akamtaja Bonaventura.

[hariri] Akiwa mtumishi mkuu wa shirika

Kwa miaka 17 (1257-1274) alikuwa Mtumishi mkuu wa shirika, akijitahidi kulinganisha misimamo tofauti ya watawa walioelekea zaidi sala na ufukara na wale walioelekea zaidi elimu na utume. Chini yake ilitungwa katiba ya kwanza katika mkutano mkuu wa Narbone.

Kufuatana na tabia yake, alikubali hali ilivyo na kujitahidi kuepusha shirika na hatari za nje na za ndani alizoziona mapema. Upinzani wa Maaskofu na maparoko dhidi ya Ndugu Wadogo ulikuwa umeungwa mkono na chuo kikuu cha Paris: hapo hazikupingwa tu ruhusa kadhaa walizopewa, bali msingi wenyewe wa mtindo wa maisha wao na wa Wadominiko. Baada ya Bonaventura na Thoma wa Akwino kuutetea, Papa alilaani upinzani na kusifu sana mtindo wa Kiinjili. Mwalimu huyo kuchaguliwa kuwa Mtumishi mkuu kukawa ushindi mwingine mkubwa chuoni.

Mashambulizi ya kutisha zaidi yalitokea ndani, upande wa ndugu “wa Kiroho”. Bonaventura alijipangia kulinganisha uaminifu kwa kanuni na mabadiliko ya shirika, akionyesha hayo hayaendi kinyume cha nia ya mwanzilishi. Ili athibitishe hayo ilimpasa kuziondolea lawama msingi wowote kwa kupigania uaminifu kwa wito wa shirika. Mwenyewe alikubali bila ya wasiwasi matamko ya Mapapa juu ya kanuni kama ufafanuzi rasmi wa wachungaji wakuu wa Kanisa na wa shirika pia.

Kielelezo cha Fransisko wa Asizi kilitakiwa kuzingatiwa na wote kwa umoja, bila ya kupishana kuhusu namna ya kukitazama. Kwa ajili hiyo alitunga kitabu rasmi cha maisha yake kilichopitishwa na mkutano mkuu hata ukaagiza maandishi yote yaliyotangulia juu ya Fransisko yateketezwe. Ndivyo shirika lilivyopotewa kwa muda mrefu na habari nyingi muhimu juu ya mwanzilishi. Kitabu alichokiandika, bila ya kusema uongo, kinaleta baadhi tu ya matendo na mafundisho ya Fransisko yaliyochaguliwa kwa makini ili kumchora kama mfano kamili wa Yesu Kristo msulubiwa na kusisitiza mang’amuzi yake bora ya kiroho, lakini kwa kuficha mambo fulanifulani kuhusu kipeo cha udogo.

Aliheshimu ufukara kama sifa kuu na utukufu wa shirika, ingawa alijali mabadiliko yaliyotokea, yaani konventi kubwa mijini n.k. Kwake elimu pamoja na utume ni sehemu ya lazima ya utendaji wa Kifransisko. Kwa ajili hiyo alikubali ruhusa lilizopewa shirika, ingawa kwa udogo alipenda kupatana na Maaskofu na maparoko.

Basi, chini ya uongozi wake shirika likatulia, kwa jinsi alivyoweza kulinganisha upendo kwa Fransisko na furaha kwa mabadiliko, hamu ya kuishi upwekeni muda mrefu pamoja na ndugu “wa Kiroho” na utetezi wa konventi za mijini.

[hariri] Akiwa kardinali askofu

Baada ya kuteuliwa kardinali mnamo Mei 1273, akiwa askofu wa Albano Laziale, aliandaa Mtaguso wa pili wa Lyon ulioanza mwaka 1254 hasa kwa lengo la kurudisha umoja kati ya Wakatoliki na Waorthodoksi, lakini katikati yake akafa.

[hariri] Kutukuzwa kwake baada ya kifo

Mwaka 1434 walipohamisha masalia yake, walikuta kichwa hakijaoza. Jambo hilo liliharakisha hatua ya kumtangaza mtakatifu iliyochukuliwa na Papa Sixtus IV tarehe 14 Aprili 1482. Halafu tarehe 14 Mei 1588 akatangazwa na Papa Sixtus V kuwa mwalimu wa Kanisa.

[hariri] Vitabu alivyoandika

  • Breviloquium
  • Collationes de decem praeceptis
  • Collationes de septem donis Spiritus Sanctis
  • Collationes in Hexaemeron
  • Commentaria in quattuor libros sententiarum Magistri Petri Lombardi
  • De mysterio Trinitatis
  • De perfectione vitae ad sorores
  • De reductione artium ad theologiam
  • De Regno Dei descripto in parabolis evangelicis
  • De scientia Christi et mysterio Trinitatis
  • De sex alis Seraphin
  • De triplici via
  • Itineriarium mentis in Deum
  • Legenda Sancti Francisci
  • Lignum vitae
  • Officium de passione Domini
  • Quaestiones de perfectione evangelica
  • Soliloquium
  • Summa theologiae
  • Vitis mystica

[hariri] Viungo vya nje

Vifaa binafsi
Maeneo ya wiki

Vibadala
Vitendo
Urambazaji
Vifaa
Lugha zingine