Petro Kanisio

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Sura ya Petro iliyochongwa katika shaba mwaka 1600 hivi

Petro Kanisi (kwa Kiholanzi Pieter Kanijs, au Kanisius, au Kanîs) alizaliwa Nijmegen (leo nchini Uholanzi) tarehe 8 Mei 1521 akafariki Freiburg (Uswisi) tarehe 21 Desemba 1597.

Alikuwa mtawa, mwanateolojia na padri wa Kanisa Katoliki.

Alitangazwa na Papa Pius IX kuwa mwenye heri mwaka 1869, halafu na Papa Pius XI kuwa mtakatifu na mwalimu wa Kanisa tarehe 21 Mei 1925.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe ya kifo chake 21 Desemba, lakini Ujerumani tarehe 27 Aprili.

Kwa kawaida anachorwa akiwa na fuvu la kichwa, sanamu ya Yesu msulubiwa na katekisimu.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Petro alizaliwa na meya wa Nijmegen, katika Dola takatifu la Roma.

Tarehe 8 Mei 1543, siku ya kutimiza miaka 22, alikuwa Mholanzi wa kwanza kujiunga na Shirika la Yesu na mwanashirika wa nane.

Alipenda elimudini na kusoma hasa vitabu vya mababu wa Kanisa.

Alipofanywa mkuu wa kwanza wa kanda ya Ujerumani ya Wajesuiti, alitoa mchango mkubwa katika urekebisho wa Kikatoliki hasa kwa kuanzisha vyuo vingi vya shirika, hata Papa Leo XIII alimtaja "mtume wa pili wa Ujerumani" baada ya Mt. Bonifas. Uwepo wa Wakatoliki wengi Ujerumani na Austria hadi leo unatokana kwa kiasi kikubwa na kazi yake.

Mshauri wa mapapa na watawala, mnamo Januari 1547 aliitwa na askofu wa Augsburg, kardinali Otto von Waldburg, ashiriki Mtaguso wa Trento kama mtaalamu wa teolojia.

Pia alifundisha kwa muda mfupi mjini Bologna, Italia.

Kanisi alikuwa gombera na mwalimu wa teolojia katika chuo kikuu cha Ingolstadt, pia aliongoza jimbo la Wien kati ya 1554 na 1555, ingawa alikataa kuwa askofu ili aweze kuendelea na utume wake huko na huko.

Aliheshimiwa kwa adabu yake, akikwepa kuita Waprotestanti "wazushi" katika mahubiri yake.

Katekisimu yake, ambayo ilitungwa kama jibu kwa Martin Luther na kutolewa mwaka 1555 kwa jina la Summa doctrinae christianae, ilirudia kuchapwa mara 200 hivi wakati wa maisha yake.

Ilitafsiriwa pia katika lugha mbalimbali na kutolewa mara 400 na zaidi.

Aliandika vilevile vitabu vingine ili kufundisha imani kulingana wa mahitaji ya walengwa.

Mwaka 1580 alianzisha huko Freiburg (Uswisi) chuo cha Mt. Mikaeli, ambapo alifariki na kuzikwa.

Maandishi[hariri | hariri chanzo]

Toleo refu (lenye madondoo ya kuthibitishia):

Gombo la 1: Imani, Tumaini, Upendo na Amri za Kanisa
Gombo la 2: Sakramenti
Gombo la 3: Utakaso wa Kikristo, matendo mema, maadili bawaba, vipaji na Matunda ya Roho Mtakatifu, Heri Nane, Mashauri ya Kiinjili n.k.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]