Katerina wa Siena
Katerina Benincasa wa Siena (25 Machi 1347 - 29 Aprili 1380) alikuwa mfuasi wa Dominiko Guzman, mwenye vipaji na karama za pekee.
Anaheshimiwa na Kanisa Katoliki kama mtakatifu bikira na mwalimu wa Kanisa.
Pia ni msimamizi wa Italia (kwa uamuzi wa Papa Pius XII mwaka 1939) na wa Ulaya (kwa uamuzi wa Papa Yohane Paulo II mwaka 1999).
Yaliyomo |
[hariri] Maisha
[hariri] Utoto
Katerina alizaliwa Siena (Italia) kama mtoto wa 24 kati ya 25 wa Jacopo Benincasa, na Lapa Piagenti (au Piacenti). Pacha wake Giovanna (kitindamimba) aliishi miezi tu.
Mwaka uliofuata (1348) Siena na Ulaya kwa jumla zilipatwa na tauni iliyopunguza sana idadi ya watu.
Alisimulia kwamba alipokuwa na miaka sita alianza kupata njozi na akiwa na miaka saba aliweka nadhiri ya ubikira akianza safari ya toba yenye saumu na malipizi mengine.
Kwenye miaka 12 wazazi, wasiojua nadiri yake, walianza kufikiria ndoa yake. Katerina aliitikia hata kwa kunyoa kipara na kujifungia nyumbani. Ili kumshurutisha wazazi walimuagiza kazi nzito nyingi, lakini bure. Siku moja baba alimkuta akisali ana njiwa akielea kichwani pake. Hapo alikubali kumuacha huru ajichagulie maisha.
[hariri] Kujiunga na Wadominiko
Alipokuwa na miaka 16 alijiunga na Utawa wa Tatu wa Mt. Dominiko bila ya kuhama nyumbani.
Alijaribu kusoma vitabu vitakatifu bila ya kufundishwa, mpaka hatimaye alijaliwa kipawa cha kusoma. Baadaye tena akajaliwa kuandika, lakini maandishi yake mengi aliyaandikisha tu.
Alisimulia pia kwamba kabla ya Kwaresima ya mwaka 1367 alitokewa na Yesu pamoja na Bikira Maria na watakatifu wengine ili kumuoa kiimani, akimvika pete yenye rubi aliyoweza kuiona yeye tu.
[hariri] Uhusiano na viongozi wa Kanisa na wa siasa
Katerina hakuogopa watu wakubwa bali aliwaelekea uso kwa uso bila ya unyonge. Kwenye mwaka 1372 hivi alimueleza balozi wa Papa huko Italia, Pietro d'Estraing, haja ya kurekebisha maadili ya makleri, ya kumrudisha Papa toka Avignone (watangulizi wake na yeye walipokaa tangu mwaka 1309) hadi Roma na ya kuendesha vita vya msalaba dhidi ya wasioamini.
Viongozi wa juu wa Kanisa, wakichukizwa na ushujaa wa mwanamke huyo asiye na elimu, walimuita mwaka 1374 huko Firenze mbele ya mkutano mkuu wa Wadominiko. Shirika lao lilitambua usahihi wa imani yake na kumkabidhi kwa uongozi wa kiroho wa Raimondo wa Capua (1330-1399) ambaye baadaye aliandika maisha yake.
Inasemekana kuwa tarehe 1 Aprili 1375 huko Pisa alijaliwa madonda matakatifu yasiyoonekana hadi kifo chake.
Baada ya majaribio mengi, hatimaye alifaulu katika juhudi kuu ya maisha yake: tarehe 17 Januari 1377 Papa alihamia Roma.
Mwanzoni mwa 1378 aliagizwa kupatanisha Ukulu mtakatifu na Firenze.
Lakini tarehe 20 Septemba wa mwaka huohuo, huko Fondi, lilianza Farakano la magharibi litakalodumu miaka 40 kwa madhara makubwa.
Alifariki akiwa na miaka 33 tu, baada ya kushindwa kula na kunywa muda mrefu kutokana na njozi ya Yesu Kristo aliyemjalia kufyonza damu ubavuni mwake.
[hariri] Utukufu
Katerina da Siena alitangazwa na Papa Pius II kuwa mtakatifu mwaka 1461. Papa Paulo VI alimtangaza mwalimu wa Kanisa tarehe 4 Oktoba 1970.
[hariri] Maandishi
- Maongezi ya Maongozi ya Mungu yaani Kitabu cha mafundisho ya Mungu
- Barua 381
- Sala [26/27]
|
|||||