Dunia
Dunia (wakati mwingine pia: ardhi) ni mojawapo ya sayari zinazotembea katika anga ya ulimwengu. Kuna sayari nane zinazolizunguka jua, dunia yetu ikiwa sayari ya tatu katika mfumo wa jua na sayari zake. Masafa baina yake na jua ni kilomita milioni 150 au kizio astronomia 1. Dunia huchukua siku 365.256 kulizunguka jua, na masaa 23.9345 kuuzunguka mhimili wake na upana wake ni kilomita 12,756.
Dunia huwa na mwezi 1.
Yaliyomo |
Muundo wa dunia [hariri]
- - taz. makala "Muundo wa dunia" -
Muundo wa dunia yetu ni ya tabaka mbalimbali zinazofuatana kutoka nje kwenda ndani. Kila moja ina tabia yake.
| Tabaka | Kuanzia kilomita |
|---|---|
| Ganda la nje | 0 - 40 |
| Koti ya juu | 40 - 400 |
| Koti ya kati | 400 - 900 |
| Koti ya chini | 650 - 2900 |
| Kiini cha nje | 2900 - 5100 |
| Kiini cha ndani | 5100-6371 |
Kila ukiingia ndani dunia inazidi kuwa moto mpaka ukifika ndani kabisa daraja ya harara hufikia nyuzi 5000-6000 °C.
Dunia kama mahali pa maisha [hariri]
Dunia yetu ni sayari pekee inayojulikana mpaka sasa ambapo binadamu na viumbe vingine vinaweza kuishi. Hapa kuna sababu mbili
- dunia yetu ina umbali na jua unaofaa kwa maisha kwa sababu sayari zilizoko karibu zaidi na jua (k.m. Zuhura) zina joto kubwa mno na sayari zilizoko mbali zaidi kama Mrihi ni baridi mno.
- dunia yetu ina angahewa yenye asilimia 78 ya naitrojini, asilimia 21 ya oksijini na asilimia 1 ya aina nyenginezo za hewa, na kwa sababu hii uhai na maisha yanamakinika katika ardhi, kinyume na sayari nyenginezo.
Uso wa dunia [hariri]
Sehemu kubwa kabisa ya dunia inafunikwa na bahari, kwani takriban asilimia 70 ya uso wake unafunikwa na maji ya bahari na kutokana na maji yote yaliyokuwepo ardhini, asilimia 97 ni maji ya bahari, na asilimia 3 ni maji matamu. Theluthi inayobaki ni nchi kavu kwenye mabara mbalimali na visiwa vingi.
Sura ya dunia ni 510,066,000 kilomita mraba, ikiwa nchi kavu imechukuwa eneo la 148,647,000 kilomita mraba na maji yamechukuwa eneo la 361,419,000 kilomita mraba.
| Bahari Kuu | Eneo lake | Kina chake |
|---|---|---|
| Pasifiki | maili 64,186,000 muraba | futi 15,215 |
| Atlantiki | maili 33,420,000 muraba | futi 12,881 |
| Bahari Hindi | maili 28,350,000 muraba | futi 13,002 |
| Bahari ya Antaktika | maili 7,848,300 muraba | futi 13,100 - 16,400 |
| Bahari ya Aktika | maili 5,106,000 muraba | futi 3,953 |
Mabara makubwa ni Asia, Afrika, Amerika Kusini na Amerika Kaskazini, Australia na Ulaya.
Angahewa [hariri]
Hewa iliyoko juu ya ardhi vile vile ina tabaka mbalimbali, na kila tabaka ina kazi yake. Hewa kwa jumla ina masafa ya kiasi cha kilomita 560 au maili 348 kuendea juu, na baada ya hapo unaingia kwenye anga ya nje. Hewa hii ndio inayotukinga sisi viumbe na madhara ya jua na mnururisho wa angani ambao unaingia anga la dunia na kuteremka chini.
Tazama pia [hariri]
| Mfumo wa jua na sayari zake |
|---|
| Jua - Utaridi - Zuhura - Dunia (Mwezi) - Mirihi - Mshtarii - Zohali - Uranus - Neptun Sun - Mercury - Venus - Earth (Moon) - Mars - Jupiter - Saturn - Uranus - Neptune |