Elimu
Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Elimu ni mojawapo ya sayansi jamii. Inagusa vipengele vya kufundisha, kujifunza, ujuzi maalumu, mawazo na ustadi. Walimu wanatumia mbinu mbalimbali kwa ajili ya kufundisha mtalaa. Mambo hayo yanaelezwa katika majarida na vitabu vingi vya mada za elimu.
Fasihi hiyo inataja aina tofauti za utekelezaji wa mafunzo unaotumia masomo, michezo, mitihani, mipango ya wakati, hamasa, mitambo mbalimbali kama kompyuta na kadhalika. Hata hivyo, kipengele muhimu kabisa ni uhusiano kati ya wanafunzi na tabia ya mwalimu. Sifa za uhusiano huo zinaweza kuwahamasisha wanafunzi wajifunze kwelikweli. Walimu bora wanawasilisha tathmini njema, uzoefu na busara jinsi innavyovuta wanafunzi.
Walimu wakiweza kufahamu wanafunzi kwa ndani, kuepa dhuluma na ubaguzi, kuunda hali ya kufundishika na kutambua uwezekano uliopo, watawawezesha wawe na matarajio makubwa zaidi kwao wenyewe na kwa jamii kwa jumla.
Lengo la elimu ni kuwasaidia wanafunzi wawe wanajamii wanaofaa katika jamii inayoendelea. Watu wa kila kizazi wajifunze utamaduni wao (angalia uendeshaji umma) ili wakomae na kutambua wajibu wao pamoja na mahitaji ya ulimwengu unaozidi kutofautika.
Yaliyomo |
[hariri] Jumla
Imetambuliwa na kukubaliwa na wengi kwamba elimu inaanza mtu anapozaliwa na inaendelea maisha yake yote. Wengine wanaamini kuwa inaanza hata mapema zaidi kama wazazi ambao wanamwimbia au kumsomea mtoto tumboni wakitumaini kwamba mawasiliano hayo yatamsaidia katika maendeleo yake.
Mara nyingi watu wanamaanisha elimu rasmi tu, lakini kila aina ya uzoefu unaojenga ufahamu ni sehemu ya elimu yetu, iwe darasani au katika maisha ya kila siku.
Kuna njia nyingi za kumfundisha mtu aongeze elimu hivyo; kuna tofauti kati ya:
- elimu rasmi katika taasisi kama shule ambako mtu hufundishwa kwa muda maalumu na kupewa uthibitisho rasmi wa maendeleo yake kama cheti, stashahada au diploma.
- elimu ya jadi inayopatikana katika kila jamii ikijumlisha mafundisho ya wazazi, makambi ya unyago, kuwa mwanafunzi wa mganga na kadhalika.
- elimu isiyo rasmi inajumlisha njia nyingi ya kujifunza ama kwa kujisomea, kushika maarifa kazini au kuzungumza na watu.
Kila mtu hupata elimu isiyo rasmi kutoka vyanzo mbalimbali. Elimu ya mtu inasaidiwa sana na familia yake, na siku hizi vyombo vya habari vinaiathiri pia sana.
[hariri] Istilahi
Neno elimu ni neno kopo kutoka Kiarabu علم na تعليم na asili hii ya Kiarabu inaonekana pia katika maneno kama taalamu au taaluma.
[hariri] Falsafa ya elimu
Lengo la falsafa ya elimu ni kutafiti na kuelewa madhumuni, asili, kanuni na mifano kamili ya elimu. Mada nyingine ni ufahamu wenyewe, asili ya akili, shida za mamlaka ya mwalimu, uhusiano kati ya elimu na jamii n.k. Tangu wakati wa Rousseau falsafa ya elimu imehusishwa na nadharia za saikolojia na maendeleo ya binadamu.
Kusudi la msingi la elimu ni kwamba mafanikio ya jamii yoyote yanategemea kuwaelimisha vijana wawe raia wanaowajibika, wanaofikiria na walio na ujasiri wa kuendesha umma. Ni jukumu lenye changamoto linalohitaji ufahamu wa ndani wa maadili, nadharia ya siasa, ujumi na uchumi. Pia ni lazima kuelewa tabia na haki za watoto, kwao wenyewe na katika jamii.
[hariri] Asili ya ufahamu
Kwa kawaida, lengo la elimu ni kumpasha mtu ufahamu. Elimu ya ufahamu pia huitwa epistemolojia. Somo hilo linachunguza asili ya ufahamu na uhusiano wake na ukweli na mawazo. Ni lazima kwa wanafunzi kuunganisha maarifa mapya na maarifa ambayo wameshayajua ili kujifunza na kuelewa. Katika ukuaji wa ufahamu elimu inagusa mada kama maarifa, ujuzi, busara na utambuzi nafsia.
[hariri] Saikolojia ya elimu
Saikolojia ya elimu ni somo la jinsi wanadamu wanavyojifunza. Pia huchunguza kufaa kwa elimu katika mazingira fulani, saikolojia ya kufundisha, na saikolojia za asasi za kielimu.
[hariri] Masomo ya kitaalamu
Masomo ya kitaalamu ni matawi ya ufahamu ambayo hufundishwa kwenye chuo kikuu. Mifano ya masomo hayo ni sayansi asili, sayansi umbile, hisabati, sayansi jamii, na sayansi tumizi.
Kila somo lina masomo mengine ndani yake, k.m. ndani ya sayansi umbile kuna fizikia na kemia, au ndani ya sayansi jamii kuna saikolojia, siasa na kadhalika.
[hariri] Elimu rasmi
Elimu rasmi inatokea ukiwepo mtaala ulioundwa kwa ajili ya kuwaelimisha watu. Hutolewa katika taasisi za elimu zinazotajwa kwa majina mbalimbali kulingana na ngazi yake:
- shule ya chekechea (shule ya vidudu) hupokea watoto wadogo sana kuanzia umri wa miaka mitatu hadi sita na kuwaingiza katika elimu kwa njia ya kucheza pamoja na hatua za kwanza za kujua herufi na namba. Kwa watoto wengi inapatikana zaidi katika mazingira ya mjini.
- Shule ya msingi hufundisha watoto kuanzia umri wa miaka sita kwa muda wa miaka 4 hadi 8 kadiri ya utaratibu wa nchi. Nchi nyingi za dunia hujaribu kusomesha watoto wote kwenye ngazi hii. Tanzania huwa na miaka saba na Kenya na miaka minane ya shule ya msingi.
- Shule ya sekondari hupokea watoto waliofaulu vema kwenye ngazi ya msingi na kuongeza elimu kwa miaka ya ziada. Kuna aina mbalimbali na muundo ni tofauti kulingana na utaratibu wa kitaifa. Tanzania huwa na aina mbili za sekondari kwanza shule ya sekondari ya miaka minne inayosomesha wanafunzi wa Form I hadi IV (O-level) halafu ngazi ya juu ya Form V na VI (A-Level) inayochukuliwa na wachache. Kenya ina ngazi moja tu ya sekondari baada ya miaka 8 ya shule ya msingi ikifundisha vijana Form I hadi IV.
- Vyuo mbalimbali hasa chuo kikuu vinavyoendeleza elimu kwenye ngazi za juu.
Tofauti kati ya shule na chuo ni hasa kwamba shuleni wanafunzi hufundishwa masomo mengi tofauti kwa kusudi la kuweka misingi mipana ya elimu, lakini kwenye ngazi ya chuo mwanafunzi anachagua kozi inayotoa mtaala maalumu katika somo fulani, kwa mfano ualimu, matibabu, hisabati, lugha au uhandisi.
[hariri] Historia
Mwaka wa 1994, Dieter Lenzen, mwenyekiti wa Chuo Kikuu Huru cha Berlin, alisema kwamba "elimu ilianza ama mamilioni ya miaka yaliyopita ama mwisho mwa mwaka wa 1770". Lenzen alitaka kuonyesha kuwa elimu kama sayansi jamii haiwezi kutengwa na mapokeo ya elimu yaliyotangulia. Uprofesa wa ufundishaji wa kwanza ulianzishwa mwaka wa 1770 kwenye Chuo Kikuu cha Halle, Ujerumani.
Kwa ajili ya maendeleo ya jamii ni lazima watu wazima wawaelimishea watoto wao. Katika jamii isiyo na uandishi, watu walikuwa wanapasha ufahamu kwa mdomo na kwa mifano. Baadaye, maandiko (yawe ishara, yawe herufi) yamesaidia kudumisha ujuzi.
Baada ya kupanua ujuzi wa jamii zaidi ya ustadi wa msingi kama mawasiliano, biashara, kuhifadhi vyakula na kadhalika, ufundishaji na elimu rasmi zilikuwa hufuata. Ufundishaji wa aina hiyo ulikuwepo Misri kati ya miaka 3000 na 500 K.K..
[hariri] Ulaya
Katika nchi za Ulaya elimu iliathiriwa na mashirika ya dini: Mapadre na watawa walitambua umuhimu wa kupasha ufahamu, nao walianzisha shule. Vyuo vikuu vingi vya Ulaya vimeanzishwa na Kanisa Katoliki.
Wakati wa Uangavu (Enlightenment), uhusiano kati ya elimu na dini ulivunjika. Jean-Jacques Rousseau alifanya utafiti katika maendeleo ya akili ya mtoto.
Mwaka 1773, Muungano wa Poland na Lithuania waliunda Tume ya Elimu ya Taifa (kwa Kipoland: Komisja Edukacji Narodowej, kwa Kilithuania: Nacionaline Edukacine Komisija) inayohesabika kama Wizara ya Elimu ya kwanza katika historia ya binadamu.
[hariri] Uchina
Katika nchi ya Uchina, elimu ilianza na maandiko ya serikali, siyo ya kidini. Kwa ajili ya kuwaelimisha wafanyakazi wao, Mfalme Mkuu wa Uchina alianzisha mfumo wa mitihani ya kitaifa kati ya mwaka wa 206 K.K. na wa 220 B.K.. Mfumo huo uliendelea mpaka mwaka wa 1911 ulipobadilishwa kufuata mfumo wa elimu kutoka Ulaya.
[hariri] Japani
Katika nchi ya Japani, elimu ilianza na dini ya Ubudha.
[hariri] Uhindi
Nchi ya Uhindi ina historia ndefu ya elimu rasmi. Mfumo wa elimu wa Gurukul ni mmojawapo wa mifumo ya kwanza duniani. Wanafunzi walipata mafunzo katika dini ya Kihindu, falsafa, maandiko ya Kisanskriti, upigaji vita, siasa, uganga wa Ayurveda na historia.
[hariri] Elimu duniani kwa sasa
Katika miaka ya mwisho iliyopita hali ya kutokujua kusoma wala kuandika imepungua sana. Kwa mfano idadi ya watu wasiokwenda shuleni ilipungua kutoka asilimia 36 mwaka wa 1960 kwenda asilimia 25 mwaka wa 2000.
[hariri] Marejeo
- Brief review of world socio-demographic trends shows world illiteracy trends.
- Dubois, H.F.W., Padovano G. & Stew, G. (2006) Improving international nurse training: an American–Italian case study. International Nursing Review 53(2): 110–116.
- Lucas, J. L., Blazek, M. A., & Raley, A. B. (2005). The lack of representation of educational psychology and school psychology in introductory psychology textbooks. Educational Psychology, 25, 347-351.
[hariri] Viungo vya nje
- Wikipedia Education category tree
- WikEd is a Wiki set up specificially for educators and education research.
- The Encyclopedia of Informal Education
- The Theory Into Practice Database