Carl Gustav Jung
Carl Gustav Jung (mara nyingi hutajwa kwa kifupi zaidi C.G. Jung; 26 Julai 1875 – 6 Juni 1961) alikuwa tabibu na mtaalamu wa saikolojia kutoka Uswisi aliyeandika kwa Kijerumani. Alifanya utafiti wa tiba ya magonjwa ya akili akaunda nadharia mbalimbali zinazoendelea kutumiwa hadi leo. Alianzisha mafundisho ya saikolojia ya kichambuzi (analytical psychology).
Kwa miaka kadhaa alishirikiana na Sigmund Freud kuendeleza mafundisho ya tiba nafsia (psychoanalysis) lakini baadaye waliachana kwa sababu Jung hakukubali na mawazo kadhaa za Freud hasa nadharia yake juu ya libido.
Kati ya mafundisho yake yanayoendelea kutumiwa ni mpangilio wa aina za silika ndani ya nafsi ya watu alipotofautisha watu wenye tabia ya mdani au msondani.
Jung alifundisha pia kama Sigmund Freud ya kwamba kuna sehemu ndani ya akili isiyofikika na fahamu ya mtu mwenyewe lakini ina athira kubwa kwa mawazo na matendo ya mtu. Ndani ya akili hii isiyofikika Jung alitofautisha kati ya sehemu ya binfasi inayotunza maarifa yaliyokusanywa na kila mtu katika maisha yake na sehemu nyingine ya kijamii inayotunza maarifa ya binadamu yaliyokusanywa na watu katika historia na kuendelezwa kwa karne nyingi ndani ya roho za watu kupitia vizazi vingi.