Laurenti wa Brindisi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Laurenti wa Brindisi, "mwalimu wa kitume".

Laurenti wa Brindisi ni jina la kitawa la Giulio Cesare Russo ( Brindisi, leo nchini Italia, 22 Julai 1559 - Belém, Ureno, 22 Julai 1619), padri na mkuu wa shirika la Ndugu Wadogo Wakapuchini.

Alitangazwa mwenye heri na Papa Pius VI mwaka 1783, mtakatifu na Papa Leo XIII mwaka 1881, hatimaye mwalimu wa Kanisa na Papa Yohane XXIII mwaka 1959.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 22 Julai.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kufiwa baba yake utotoni, alisoma kwenye shule ya Wafransisko Wakonventuali huko Brindisi, akavaa kanzu yao tangu mwaka 1565 hadi 1567 kama maandalizi ya kujiunga nao. Wakati huo ndipo alipoanza kuhubiri, kadiri ya desturi yao.

Kisha kufiwa mama na kupatwa na hali ngumu kiuchumi alihamia Venezia kwa ndugu yake padri alipoendelea kusoma na kuzingatia wito hadi kujiunga na Wakapuchini tarehe 18 Februari 1575 kwa kuvaa kanzu yao na kubadilishiwa jina.

Huko Padova aliendelea kusoma mantiki na falsafa, halafu akarudi Venezia kusomea teolojia. Kwa wakati huohuo alikuwa anafundisha pia, kutokana na ujuzi wake mkubwa ajabu, hasa wa Biblia katika lugha zote asili, uliomsaidia hata kuhubiria kwa mafanikio Wayahudi.

Tarehe 18 Desemba 1582 alipata upadrisho akaendelea kutumia utaalamu wake kwa ajili ya Urekebisho wa Kikatoliki baada ya Mtaguso wa Trento. Kwa kuwa alijua lugha mbalimbali, alihubiri katika nchi nyingi za Ulaya.

Mwaka 1589 alianza kupata vyeo vikubwa shirikani. Pamoja na hayo, alitumwa Ujerumani kuongoza wanashirika wanaokwenda kuishi na kufanya utume huko.

Mnamo Oktoba 1601 aliomba kuwa mmojawapo wa mapadri wa kuhudumia kiroho wanajeshi wa Kikristo wakipambana na Waturuki wavamizi.

Tarehe 24 Mei 1602 alichaguliwa kuwa mkuu wa shirika, mwenye jukumu la kutembelea kanda zake zote.

Mwaka 1618 alitumwa na wananchi wa Napoli walionyanyaswa na makamu wa mfalme wa Hispania akawatetee kwa mfalme mwenyewe, Filipo III. Baada ya kukwepa njama mbalimbali, alitabiri kuwa mwenyewe atakufa mapema, na mfalme atamfuata kabla ya miaka miwili kwisha, kama ilivyotokea.

Kati ya majukumu mazito ndani ya shirika na ya Kanisa kwa jumla aliendelea kuwa mfuasi mnyenyekevu wa Fransisko wa Asizi, mbali ya kuandika vitabu vingi - vya ufafanuzi wa Biblia, vya maadili, vya hoja za kidini - vilivyomstahilia jina la “Doctor Apostolicus”, yaani "Mwalimu wa Kitume".

Katika maandishi yake, alizungumzia mara nyingi liturujia.

Anakumbukwa pia kwa ibada yake kwa ekaristi na kwa neema za pekee alizokuwa anazipata wakati wa kuiadhimisha, zilizomfanya achukue masaa kila siku kuadhimisha Misa, ambayo kwake ilikuwa hai.

Alifariki tarehe 22 Julai 1619, labda kwa sumu.

Maandishi[hariri | hariri chanzo]

'Opera omnia, yaani maandishi yake yote katika magombo 15 yametolewa kitaalamu huko Quaracchi miaka 1926-1956. Kati yake kuna:

 • Mariale
 • Lutheranismi hypotyposis
 • Explanatio in Genesim
 • Quadragesimale primum
 • Quadragesimale secundum
 • Quadragesimale tertium
 • Quadragesimale quartum
 • Adventus
 • Dominicalia
 • Sanctorale
 • Sermones de tempore

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]