Yohane wa Avila
Yohane wa Avila (Almodóvar del Campo, Hispania, 6 Januari 1500 - Montilla, Hispania, 10 Mei 1569) alikuwa padri mwanajimbo wa Hispania aliyeathiri sana Kanisa Katoliki la nchi hiyo na urekebisho wa Kikatoliki katika karne ya 16.
Kwa namna ya pekee mkoa wa Andalusia na watakatifu Teresa wa Yesu, Yohane wa Mungu na Fransisko Borgia walifaidika na utume wake.
Papa Leo XIII alimtangaza mwenye heri tarehe 12 Novemba 1893, halafu Papa Paulo VI akamtangaza mtakatifu tarehe 31 Mei 1970.
Hatimaye Papa Benedikto XVI akamtangaza mwalimu wa Kanisa wa 34 tarehe 7 Oktoba 2012.[1]
Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 10 Mei.
Yaliyomo |
Maisha [hariri]
Utoto na wito [hariri]
Yohane wa Avila alizaliwa huko Almodóvar del Campo katika familia tajiri na yenye imani ya Kikristo[2] ingawa yenye asili ya Kiyahudi.[3]
Alipofikia umri wa miaka 14 alitumwa masomoni kwenye chuo kikuu cha Salamanca ili ajifunze sheria, lakini baada ya miaka miwili akarudi nyumbani akatumia miaka mitatu kufanya toba kali.
Utakatifu wake ulimvutia Mfransisko ambaye alipitia Almodóvar, akamshauri aanze masomo ya falsafa na teolojia huko Alcalá de Henares, alipofundishwa na Mdominiko maarufu, Domingo de Soto.
Wakati wa masomo hayo alifiwa wazazi; hivyo baaada ya upadrisho wake aliuza mali ya familia na kuwagawia maskini mapato yake.
Yeye aliona vifo hivyo kuwa ishara ya Mungu kumwita awe mmisionari akajiandaa kwenda Mexico.
Mwaka 1527, akiwa Seville ili kupata nafasi nzuri ya kusafiri baharini, namna yake bora ya kuadhimisha Misa ilimshangaza padri Hernando de Contreras, ambaye alimuarifu Askofu mkuu wa Seville, na pia Hakimu mkuu Alonso Manrique de Lara.
Askofu huyo alitambua kwamba huyo kijana anafaa sana kuchochea imani mkoani Andalusia, na baada ya kumshauri sana alimfanya akubali kuacha mpango wa kwenda Amerika.
Mtume wa Andalusia [hariri]
Alianza kuhubiri tarehe 22 Julai 1529, akapata mara umaarufu.
Katika miaka tisa aliyofanya utume huko Andalusia, mahubiri yake yote yalisikilizwa na umati wa watu waliobanana.
Hata hivyo, nguvu ya maneno yake kwa ajili ya urekebisho na dhidi ya mwenendo wa matabaka ya juu katika jamii ilisababisha afikishwe mbele ya Hakimu mkuu wa Seville.
Shtaka lilikuwa la kuzidisha hatari ya kiroho inayotokana na utajiri na kuwanfugia matajiri milango ya mbinguni. Lakini aliweza kujitetea vizuri na kuachiliwa mwaka 1533 hata akateuliwa kuhubiri tena.[4]
Kama wanasala wengine wa Hispania wakati huo, alishukiwa mara kadhaa kuhusika na Alumbrados, waliotazamwa kama wazushi.
Urekebisho wa mapadri nchini Hispania [hariri]
Yohane wa Avila anakumbukwa pia kwa kurekebisha maisha ya mapadri nchini.[4]
Ni kwamba alianzisha vyuo kadhaa ambako wanafunzi wake walijitosa kufundisha vijana.[5] Umuhimu wa pekee unacho Chuo kikuu cha Baeza kilichoanzishwa mwaka 1538 kwa hati ya Papa Paulo III[6] na ambacho akawa gombera wake wa kwanza.[7]
Chuo hicho kikawa kielelezo kwa seminari na kwa shule za Wajesuiti, ambao wanamheshimu kwa pekee kwa kuwasaidia kustawi Hispania.[4]
Kifo [hariri]
Baada ya utume wake wa miaka tisa Andalusia, alirudi Seville, ambako aliondoka tu kwa kazi kubwa zaidi huko Cordoba, Granada, Baeza, Montilla na Zafra.
Miaka kuni na nane ya mwisho aliugua mfululizo, kutokana na ugumu wa maisha na wa kazi alizofanya kwa miaka arubaini.
Alifariki tarehe 10 Mei 1569 huko Montilla.
Maandishi [hariri]
Maandishi yake yalikusanywa huko Madrid miaka 1618, 1757, 1792 na 1805; kati yake, maarufu zaidi ni: "Audi Fili" kuhusu ukamilifu wa Kikristo, na "Barua za Kiroho" kwa wafuasi wake[8]
Tanbihi [hariri]
- ↑ Pope to proclaim St John of Avila Doctor of the Universal Church. News.va. Holy See (20 Agosti 2011). Rudishwa juu ya 21 Agosti 2011.
- ↑ Wilke 2003, p. 963
- ↑ Domínguez Ortiz 1992
- ↑ 4.0 4.1 4.2 Wilke 2003, p. 964
- ↑ Smith 1913
- ↑ Introducción Histórica, Universidad de Jaén, 2005-09-26. Accessed online 2010-02-05.
- ↑ José Biedma, Juan de Ávila y la Universidad de Baeza, cibernous.com. Accessed online 2010-02-05.
- ↑ St. John of Ávila 1904
Marejeo [hariri]
- Domínguez Ortiz, Antonio (1992). Los judeoconversos en la España moderna, 2. ed. (in Spanish), Madrid: Mapfre. ISBN 978-84-7100-353-9.
Smith, Ignatius (1913). "Bl. John of Avila". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company.- St. John of Ávila (1904). Letters of Blessed John of Avila. Stanbrook Abbey: Burns & Oates Ltd.
- Wilke, J. C. (2003). "John of Avila, St.". In Catholic University of America. New Catholic Encyclopedia. 7 (Hol–Jub) (2d ed.). Washington, D.C.: Gale. pp. 446–449. ISBN 0-7876-4004-2.
Viungo vya nje [hariri]
| Makala hii kuhusu Mkristo huyu bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Yohane wa Avila kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |
|
|||||