Alberto Mkuu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Alberto Mkuu alivyochorwa na Tommaso da Modena mwaka 1352

Alberto Mkuu (Lauingen, Donau, leo nchini Ujerumani, 1205 hivi - Cologne, Ujerumani, 15 Novemba 1280) ni jina alilopewa kwa heshima askofu Alberto wa Bollstädt (au wa Cologne) kutokana na mchango wake mkubwa upande wa elimu ya kawaida na ile ya dini na vilevile upande wa uchungaji na wa upatanishi wa watu na watawala.

Mtawa wa Shirika la Wahubiri, anahesabiwa kuwa mwanafalsafa na mwanateolojia bora ya Ujerumani katika Karne za Kati.

Alijitahidi kulinganisha imani na akili akiingiza falsafa ya Aristotle katika Ukristo, jambo lililoendelezwa na mwanafunzi wake bora, Thoma wa Akwino.

Alitangazwa na Papa Gregori XV kuwa mwenye heri mwaka 1622, halafu na Papa Pius XI kuwa na mtakatifu na mwalimu wa Kanisa tarehe 16 Desemba 1931.

Mwaka 1941 Papa Pius XII alimtangaza msimamizi wa wanasayansi.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Novemba.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Alberto, mtoto mdogo wa mtawala wa Bollstädt, alizaliwa Lauingen (Svevia, Ujerumani) lakini mwaka haujulikani: 1205, 1206 au 1193.

Vilevile hakuna hakika kuhusu elimu yake ya msingi, kama aliipata nyumbani au shuleni, lakini ujanani alitumwa kwenye chuo kikuu cha Padova (Italia), maarufu kwa masomo yaliyompendeza zaidi.

Mwaka 1223, baada ya kusikia hotuba ya Jordano wa Saksonia, mwalimu mkuu wa pili katika historia ya Shirika la Wahubiri, alijiunga na utawa huo ulioanzishwa na Dominiko Guzman.

Alipomaliza masomo yake, ama Padova au kwingine, alifundisha teolojia huko Hildesheim, Freiburg in Brisgau, Regensburg, Strasburg na Cologne.

Akiwa katika konventi ya mji huo, akisoma Liber Sententiarum ya Petro Lombardo mwaka 1245, aliagizwa kwenda Paris (Ufaransa) alipojipatia digrii katika kituo kikuu chake, maarufu kuliko vyote upande wa teolojia.

Akiwa safarini alisikilizwa na Thoma wa Akwino, kijana mkimya mwenye kutafakari, ambaye Alberto alitambua ukuu wa akili yake akamtabiri umaarufu mkubwa. Huyo mwanafunzi mpya aliongozana naye hadi Paris halafu (1248) Cologne, ambapo Alberto alikuwa amechaguliwa kuwa gombera, wakati Thoma akawa mwalimu wa pili na Magister Studentium ("mwalimu wa wanafunzi").

Katika mkutano mkuu wa Wadominiko uliofanyika Valenciennes mwaka 1250, pamoja na Thoma na Petro wa Tarentaise, alitunga taratibu za masomo na za stahili shirikani.

Mwaka 1254 alichaguliwa mkuu wa kanda ya Ujerumani, wadhifa mgumu alioshughulikia vizuri sana.

Mwaka 1256 alikwenda Roma ili kutetea mashirika ya ombaomba dhidi ya mashambulizi ya Wiliamu wa Saint-Amour, ambaye kitabu chake De novissimis temporum periculis kililaaniwa na Papa Aleksanda IV tarehe 5 Oktoba 1256.

Akiwa Roma, Alberto alishika nafasi ya mwalimu wa nyumba ya Papa na kufafanua Injili ya Yohane.

Mwaka 1257 alijiuzulu kama mkuu wa kanda ili ajitose kusoma na kufundisha.

Mwaka 1260 alipewa daraja takatifu ya uaskofu kwa ajili ya Jimbo la Regensburg, aliloliongoza hadi 1262 ambapo alijiuzulu akarudia kufundisha Cologne.

Mwaka 1270 alimuandikia Thoma, aliyekuwa Paris, ili kumsaidia dhidi ya hoja za Sigieri wa Brabante na wafuasi wa Averroe. Ilikuwa kitabu cha pili dhidi ya huyo mwanafalsafa Mwarabu (cha kwanza kiliandikwa mwaka 1256 kwa jina De Unitate Intellectus Contra Averroem).

Mwaka 1274 aliitwa na Papa Gregori X ashiriki Mtaguso wa pili wa Lyon, ambamo alifanya kazi kubwa. Huko alipata taarifa ya kifo cha Thoma akasema, "Mwanga wa Kanisa umezimika".

Alijitokeza tena kwa nguvu mwaka 1277, ilipotangazwa nia ya Etienne Templier, askofu mkuu wa Paris pamoja na wengine ya kulaani maandishi ya Thoma kama yenye uzushi. Ili kumtetea alifunga safari kwenda Paris.

Mwaka 1278 (alipoandika wasia wake) alianza kusahausahau mambo, na mwili wake uliodhoofishwa na maisha magumu ya kujinyima na ya kazi ulizidi kushindwa na uzee akafa mwaka 1280.

Alizikwa katika kanisa la parokia ya Mt. Andrea ya Cologne.

Maandishi[hariri | hariri chanzo]

Vitabu vyake vinahusu: mantiki, sayansi, elimunafsia, falsafa, maadili, siasa, teolojia, ufafanuzi wa Biblia n.k.

Mtaalamu mkuu wa biolojia wakati wake, aliunganisha vizuri sayansi na ufunuo wa Mungu, falsafa na teolojia. Ulinganifu huo unamfanya awe karibu na watu wa leo katika maswali wanayojiuliza kuhusu asili na maendeleo ya ulimwengu.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]


Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]