Sirili wa Aleksandria

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Sirili wa Aleksandria (370 hivi - 444) alikuwa Patriarki wa Aleksandria (Misri) (kuanzia mwaka 412) na mwanatheolojia, aliyeshiriki mapambano ya karne ya 4 kuhusu imani juu ya Yesu Kristo.

Alimkomesha Nestori wa Konstantinopoli katika Mtaguso wa Efeso (431) uliomtangaza Bikira Maria kuwa Mama wa Mungu. Vilevile alikuwa mkali dhidi ya wazushi wengine, Wayahudi na Wapagani.

Anaheshimiwa kama mtakatifu, babu wa Kanisa na mwalimu wa Kanisa.

Yaliyomo

[hariri] Asili na ujana

Cyril alizaliwa katika kijiji cha Theodosios, Misri, karibu na El-Mahalla El-Kubra ya leo.

Miaka michache baadaye mjomba wake Theofilo wa Aleksandria alipata kuwa Patriarki wa Aleksandria. Mama yake alibaki karibu na kaka yake, hivyo mtoto alipata malezi mazuri na elimu sanifu ya wakati ule: lugha (390-392), fasihi (393-397) hatimaye teolojia na Biblia (398-402).

[hariri] Patriarki

Sirili katika mavazi ya kiaskofu.

Theofilos alipofariki tarehe 15 Oktoba 412, Cyril alichaguliwa Patriarki wa Aleksandria tarehe 18 Oktoba 412.

Akitumia mamlaka yake katika jiji hilo lenye ushindani na fujo, alifaulu kufunga makanisa ya Wanovatiani na kufukuza Wayahudi wengi.

Pia alitetea msimamo wa teolojia ya Shule ya Aleksandria dhidi ya ile ya Antiokia na haki ya Kanisa la Aleksandria kuwa la pili duniani (baada ya Kanisa la Roma) dhidi ya Kanisa la Konstantinopoli lililopendelewa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli.

Ushindani huo ulikomaa mwaka 428 alipochaguliwa kuwa Patriarki wa Konstantinopoli Nestori, mwenyeji wa Antiokia.

Cyril alipata nguvu pale ambapo padri wa Antiokia alianza kuhubiri huko Konstantinopoli kwamba Bikira Maria hastahili kuitwa "Mama wa Mungu". Waamini walipomshtaki kwa Nestori, huyo akamtetea.

Kwenye Pasaka 429, Cyril aliwaandikia wamonaki barua dhidi ya Nestori. Nakala ilipofika Konstantinopoli, Nestori alihubiri dhidi yake. Ndiyo mwanzo wa mawasiliano makali kwa njia ya barua.

Hatimaye, ili kumaliza mabishano hayo, kaisari Theodosius II aliitisha mtaguso mkuu huko Efeso, palipokuwa upande wa Cyril, ambaye alifungua na kufunga Mtaguso wa Efeso (431) kabla Nestori na wafuasi wake hawajafika; hivyo, mtaguso uliagiza Nestori aondoshwe madarakani na kupelekwa uhamishoni.

Lakini Yohane wa Antiokia na wengine wa upande wa Nestori walipofika Efeso, walifanya mtaguso wa kwao wakimhukumu Cyril kama mzushi, wakidai aondoshwe madarakani.

Theodosius alimkamata Cyril, lakini huyo alikimbilia Misri akaleta fujo hadi kwenye ikulu, hata kaisari alikubali kumfukuza Nestori.

Tukio hilo ni chanzo cha farakano la Waashuru linalodumu hadi leo.

Cyril alifariki mwaka 444 hivi, lakini mashindano yaliendelea hadi Mtaguso wa Kalsedonia (451) na mbele zaidi.

[hariri] Vyanzo

  • McGuckin, John A. St. Cyril of Alexandria and the Christological Controversy. Crestwood, NY: St. Vladimir’s Seminary Press, 2004. ISBN 0-88141-259-7
  • Wessel, Susan. Cyril of Alexandria and the Nestorian Controversy:The Making of a Saint and a Heretic. Oxford 2004. ISBN 0-19-926846-0

[hariri] Viungo vya nje

[hariri] Maandishi yake

[hariri] Vinginevyo

Vifaa binafsi
Maeneo ya wiki

Vibadala
Vitendo
Urambazaji
Vifaa
Lugha zingine