Kitabu cha Isaya
Kitabu cha Isaya kinashika nafasi ya kwanza kati ya vitabu vya kinabii vya Tanakh (Biblia ya Kiebrania), na katika Agano la Kale ambayo ndiyo sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo.
[hariri] Utunzi na mada
Nabii Isaya (kwa Kiyahudi יְשַׁעְיָהוּ, yaani "YHWH anaokoa") alizaliwa katika ufalme wa Yuda (Israeli Kusini mwaka 765 hivi K.K. akatabiri kwa muda usiopungua miaka 40 (740-700 hivi K.K.) akiingilia kati matukio yote ya siasa, ambayo yalikuwa ya kutisha kutokana na nguvu za Waashuru ambao waliangamiza Israeli na kukaribia kufuta hata ufalme wa Kusini.
Maandishi yake yanapendeza kuliko yote ya manabii, hasa upande wa ushairi.
Lakini ukuu wa Isaya uko hasa upande wa imani.
Kuanzia wito wake (6) alitawaliwa na wazo la utukufu wa Mungu na unyonge wa binadamu anayehitaji kutakaswa naye.
Aliwadai wafalme wote wa Yuda wamtegemee Mungu tu, si mataifa yenye nguvu (7:1-8:18; 20:1-6; 22:1-14).
Lakini toka mwanzo aliambiwa hatasikilizwa, hivyo ikambidi atabiri adhabu.
Pamoja na kufanya hivyo alitabiri kuwa Mungu hataangamiza kabisa taifa lake, bali ataacha mabaki yake ambayo yataleta wokovu: katika mabaki hayo Bikira (kwa Ukristo ndiye Bikira Maria) atamzaa Masiya (Yesu Kristo) ambaye ni Emmanueli, yaani Mungu pamoja nasi, mwana wa Daudi ambaye ataleta amani na haki duniani.
Katika kitabu chake unapatikana pia unabii wa wafuasi wake wasiojulikana, waliofanya kazi katika miaka 550-500 hivi K.K.
Ni kwamba, ingawa nabii Ezekieli alifanya kazi nzuri wakati wa uhamisho wa Babeli, nabii mwingine alitumwa kuwatia moyo Wayahudi wenzake huko kwa kusema Mungu atawarudisha kwao (Is 40:1-11).
Hivyo akawafanya watamani kurudi badala ya kukwama katika kujitafutia maendeleo ya uchumi.
Hatujui jina lake, lakini tunamuita Isaya II (mwaka 550 hivi K.K.) kwa kuwa maandiko yake yamepangwa katika kitabu cha Isaya (40-55): sehemu hiyo inaitwa pia kitabu cha faraja ya Israeli.
Katika sura hizo mna mashairi manne kuhusu mtumishi mteswa wa YHWH ambayo ndiyo utabiri bora juu ya Yesu (42:1-4; 49:1-6; 50:4-9; 52:13-53:12).
Isaya 56 66 ni sura za baadaye tena (Isaya III, mwaka 500 hivi K.K.) ambazo zinawakaribisha watu wa mataifa yote. Kiini chake ni 61:1-3.
[hariri] Ufafanuzi
Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.
[hariri] Viungo vya nje
Kitabu cha Isaya katika tafsiri ya Kiswahili (Union Version)
Mwanzo Kutoka Walawi Hesabu Kumbukumbu Yoshua Waamuzi Ruthu Samueli I Samueli II Wafalme I Wafalme II Mambo ya Nyakati I Mambo ya Nyakati II Ezra Nehemia TobitiDK YudithiDK Esta Wamakabayo IDK Wamakabayo IIDK Yobu Zaburi Methali Mhubiri Hekima DK SiraDK Wimbo Bora Isaya Yeremia Maombolezo BarukuDK Ezekieli Danieli Hosea Yoeli Amosi Obadia Yona Mika Nahumu Habakuki Sefania Hagai Zekaria Malaki - Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.