Kitabu cha Esta

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Gombo la kitabu cha Esta kwa Kiebrania.
Esta na Mardokai, mchoro wa Aert de Gelder.

Kitabu cha Esta (jina lake huandikwa pia Ester na "Esther") ni kitabu cha Biblia ya Kiebrania, na hivyo pia cha Agano la Kale, ambalo ni sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo. Kiliandikwa kwanza kwa Kiebrania.

Tafsiri ya kitabu cha Esta inavyopatikana katika Septuaginta imeongezewa sana; nyongeza hizo za Kigiriki zinahesabiwa na Kanisa Katoliki na wengineo kuwa sehemu za kitabu yenye uvuvio wa Roho Mtakatifu ingawa si sehemu za hadithi asili. Ni katika nyongeza hizo tu kwamba Mungu anatajwa na mtazamo wa imani unajitokeza.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Wakati wa kuandikwa[hariri | hariri chanzo]

Mwandishi wake hajulikani, lakini kufuatana na mapokeo ya Wayahudi, kitabu kiliandikwa takriban mwaka wa 400 KK, muda usio mrefu baada ya matukio kinayoyasimulia. Sababu za mwelekeo huo ni zifuatazo: Sherehe ya Purim ilikuwa husherehekewa kila mwaka wakati wa kuandikwa kwa kitabu, lakini Mfalme Ahasuero hutajwa kama mfalme aliyepita. Ukamilifu wa maelezo kuhusu mila na desturi za dola la Waajemi unadokeza kuwa kitabu kimeandikwa kabla dola hilo halijavamiwa na kuangamizwa na Iskanda Mkuu takriban mwaka wa 330 KK.

Yaliyomo[hariri | hariri chanzo]

Kitabu cha Esta kinahusika na wakati wa taifa la Israeli unaojulikana kama wakati wa baada ya Uhamisho wa Babeli. Kinasimulia Wayahudi walivyoishi katika dola la Waajemi. Wayahudi hao walibaki uhamishoni badala ya kurudi kwao hata baada ya Waajemi kuangamiza utawala wa Babuloni mwaka 539 KK, ambapo Mfalme Koreshi alishinda na kuteka Babeli.

Ingawa Koreshi aliwaruhusu Wayahudi waliofungwa warudi katika nchi yao, wengi wao waliamua kubaki Babeli au Uajemi. Wao walihakikishiwa usalama na uhuru fulani katika nchi ya kifungo chao, kwa hiyo hawakutaka kukabiliana na wasiwasi na ugumu wa maisha mapya huko Yerusalemu. Pamoja na watoto wao waliendelea kuongeza mafanikio ya namna mbalimbali, lakini hawakuonyesha nia ya kuimarisha upya dini yao iwe nguvu ya kiroho katika maisha yao ya kitaifa. Hata hivyo, kadiri Wayahudi walivyoendelea kufuata sheria zao za kidini walisumbuliwa sana na wenyeji. Lakini Mungu alikuwa akiendelea bado kuwalinda watu wake, wawe wamemkubali au sivyo, asiruhusu waangamizwe.

Hivyo kitabu kinaeleza hasa jinsi Hamani, waziri mkuu wa mfalme Artashasta, alivyopanga kuwaangamiza Wayahudi wote. Wakati huohuo, malkia wa Uajemi alikuwa Esta, Myahudi. Pamoja na Mordekai, baba mlezi wake, Esta alifaulu kuzuia mipango ya Hamani. Ushindi huo wa Wayahudi ulianzisha sherehe ya Purim ambayo imekuwa sikukuu maarufu ya Wayahudi ikiadhimishwa kabla ya Pasaka.

Wataalamu wengi wanakubaliana kusema hii ni hadithi tu, si habari ilivyotokea katika historia.

Muhtasari wa sehemu ya Kiebrania[hariri | hariri chanzo]

1:1-2:23 Kuinuliwa kwa Esta kuwa malkia

3:1-7:10 Mikakati ya kuwaangamiza Wayahudi

8:1-10:3 Shangwe ya Wayahudi

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Kitabu cha Esta (kadiri ya Biblia ya Kiebrania) katika tafsiri ya Kiswahili (Union Version)[dead link]


Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.

Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kitabu cha Esta kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.