Kanisa Katoliki
Kanisa Katoliki ni jina linalotumika hasa kumaanisha Kanisa la Kikristo linalokubali mamlaka ya kiroho ya Papa wa Roma kama mkuu wa urika wa Maaskofu juu yake lote. Ndilo kubwa kabisa kati ya madhehebu yote ya dini hiyo, likikusanya nusu ya wafuasi wote wa Yesu.
Yaliyomo |
Maana ja jina [hariri]
Neno "katoliki" linatokana na kivumishi cha Kigiriki καθολικός (katholikòs), lenye maana ya «kamili, kadiri ya utimilifu». Tunalikuta kwa mara ya kwanza katika maandishi ya Ignas wa Antiokia kwa Wakristo wa Smirna mwanzoni mwa karne II: «Alipo Yesu Kristo ndipo lilipo Kanisa Katoliki» (Ad Smyrnaeos, 8).
Imani yake [hariri]
Kanisa hilo linaamini kuwa ndani yake linadumu moja kwa moja Kanisa pekee lililoanzishwa na Yesu Kristo ambalo wanaunganishwa nalo wote wanaobatizwa katika madhehebu yoyote.
Tofauti ni kwamba baadhi (Wakatoliki) wana ushirika kamili nalo, wakati wengine (hasa Waorthodoksi na Waprotestanti) wana ushirika nalo kwa viwango mbalimbali, kadiri wanavyokubali mafundisho, sakramenti na uongozi wake.
Uenezi wake [hariri]
Kati ya madhehebu ya Kikristo, Kanisa Katoliki linakusanya waamini 1,214,000,000, yaani nusu ya wafuasi wote wa Yesu, na 17.5 % ya binadamu wote, likiwa na asilimia kubwa ya waamini kati ya wananchi wa Amerika na Ulaya.
Miundo yake [hariri]
Kanisa Katoliki linaishi katika majimbo 2,979, ambayo kwa kawaida yanaongozwa na Maaskofu (kwa jumla wako 5,132) wakisaidiwa na mapadri (413,418) na mashemasi, ambao baadhi yao wanajiandaa kupata upadrisho na 41,000 hivi ni wa kudumu.
Kati ya majimbo hayo, mengi yanafuata utaratibu wa Kanisa la Kilatini, ila kuna mengine yanayofuata taratibu za Makanisa Katoliki ya Mashariki.
Majimbo yanagawanyika katika parokia zinazoongozwa na padri anayeitwa paroko.
Kati ya waamini, ambao wengi kabisa kati yao ni wale wa kawaida wanaoitwa walei, wana nafasi ya pekee wamonaki na watawa wengine ambao wanaishi kwa mitindo mbalimbali iliyostawi katika historia ya Kanisa ili kumfuata Yesu kwa karibu zaidi katika useja mtakatifu, ufukara na utiifu, kadiri ya karama maalumu. Masista ni 713,000 hivi na mabruda 55,000.
| Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kanisa Katoliki kama historia yake au uenezi wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |