Mtakatifu Paulo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mtume Paulo)
Sanamu ya Mtakatifu Paulo mbele ya Kanisa kuu la Roma.
Sura yake kadiri ya wataalamu wa LKA North Rhine-Westphalia, Ujerumani.

Mtume Paulo (7-67 hivi) ni mmisionari mkuu wa Yesu Kristo katika historia ya Kanisa.

Alitangaza kifo na ufufuko wake katika nchi karibu zote zilizopo kaskazini kwa Bahari ya Kati.

Alimaliza ushuhuda wake kwa Yesu kwa kufia dini yake mjini Roma wakati wa dhuluma iliyoanzishwa na Kaisari Nero.

Tangu kale anaheshimiwa kama mtakatifu.

Sherehe yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 29 Juni pamoja na ya Mtume Petro, lakini pia uongofu wake una sikukuu maalumu, tarehe 25 Januari[1].

Maisha kabla ya wongofu[hariri | hariri chanzo]

Mtakatifu Paulo alizaliwa kati ya miaka 7-10 BK katika familia ya Kiyahudi ya kabila la Benyamini (Israeli) na madhehebu ya Mafarisayo iliyoishi katika mji wa Tarsus (kwa sasa mji huo uko sehemu ya kusini mashariki ya nchi ya Uturuki).

Jina lake la kwanza (la Kiebrania) lilikuwa Sauli, lakini kadiri ya desturi ya wakati ule alikuwa pia na jina la Kigiriki: Paulos kutoka Kilatini Paulus (= mdogo). Mwenyewe alikuwa na uraia wa Roma kama wananchi wote wa Tarsus.

Angali kijana alisomea ualimu wa Sheria (yaani wa Torati) huko Yerusalemu chini ya mwalimu maarufu Gamalieli wa madhehebu ya Mafarisayo.

Akishika dini yake kwa msimamo mkali akawa anapinga Ukristo kwa kukamata, kutesa na hata kuua Wakristo, kama vile Stefano Mfiadini.

Alifanya hivyo mpaka alipotokewa na Yesu Kristo mfufuka akiwa njiani kwenda Damaski, Syria (kwa umuhimu wake katika Historia ya Wokovu habari hii inasimuliwa mara tatu katika kitabu cha Matendo ya Mitume: 9:1-19; 21:12-18 na 22:5-16). Jibu lake kwa Yesu lilikuwa (Mdo 22:10): "Nifanye nini, Bwana?"

Habari za wongofu wake katika Mdo 9[hariri | hariri chanzo]

"Barabara iliyonyoka", Mtume Paulo alipobatizwa na Anania wa Damasko, ilivyo leo.

1 Wakati huo Saulo alikuwa akizidisha vitisho vikali vya kuwaua wafuasi wa Bwana. Alikwenda kwa Kuhani Mkuu,

2 akaomba apatiwe barua za utambulisho kwa masunagogi ya Kiyahudi kule Damasko, ili akikuta huko wanaume au wanawake wanaofuata Njia ya Bwana, awakamate na kuwaleta Yerusalemu.

3 Lakini alipokuwa njiani karibu kufika Damasko, ghafla mwanga kutoka angani ulimwangazia pande zote.

4 Akaanguka chini na kusikia sauti ikimwambia: "Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?"

5 Naye Saulo akauliza, "Ni nani wewe Bwana?" Na ile sauti ikajibu, "Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa.

6 Lakini simama sasa, uingie mjini na huko utaambiwa unachopaswa kufanya."

7 Wale watu waliokuwa wanasafiri pamoja na Saulo walisimama pale, wakiwa hawana la kusema; walisikia ile sauti lakini hawakumwona mtu.

8 Saulo aliinuka, na alipofumbua macho yake hakuweza kuona chochote; hivyo wale watu wakamwongoza kwa kumshika mkono mpaka mjini Damasko.

9 Saulo alikaa siku tatu bila kuona, na wakati huo hakula au kunywa chochote.

10 Basi, huko Damasko kulikuwa na mfuasi mmoja aitwaye Anania. Bwana akamwambia katika maono, "Anania!" Anania akaitika, "Niko hapa, Bwana."

11 Naye Bwana akamwambia, "Jitayarishe uende kwenye barabara inayoitwa Barabara ya Moja kwa Moja, na katika nyumba ya Yuda umtake mtu mmoja kutoka Tarso aitwaye Saulo. Sasa anasali;

12 na katika maono ameona mtu aitwaye Anania akiingia ndani na kumwekea mikono ili apate kuona tena."

13 Lakini Anania akajibu, "Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kutoka kwa watu wengi; nimesikia juu ya mabaya aliyowatendea watu wako huko Yerusalemu.

14 Na amekuja hapa akiwa na mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu kuwatia nguvuni wote wanaoomba kwa jina lako."

15 Lakini Bwana akamwambia, "Nenda tu, kwa maana nimemchagua awe chombo changu, alitangaze jina langu kwa mataifa na wafalme wao na kwa watu wa Israeli.

16 Mimi mwenyewe nitamwonyesha mengi yatakayomlazimu kuteswa kwa ajili ya jina langu."

17 Basi, Anania akaenda, akaingia katika hiyo nyumba. Kisha akaweka mikono yake juu ya Saulo, akasema, "Ndugu Saulo, Bwana ambaye ndiye Yesu mwenyewe aliyekutokea ulipokuwa njiani kuja hapa, amenituma ili upate kuona tena na kujazwa Roho Mtakatifu."

18 Mara vitu kama magamba vikaanguka kutoka macho ya Saulo, akaweza kuona tena. Akasimama, akabatizwa.

19 Na baada ya kula chakula, nguvu zake zikamrudia. Saulo alikaa siku chache pamoja na wafuasi huko Damasko.

20 Mara alianza kuhubiri katika masunagogi kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.

21 Watu wote waliomsikia walishangaa, wakasema, "Je, mtu huyu si yuleyule aliyewaua wale waliokuwa wanaomba kwa jina hili kule Yerusalemu? Tena alikuja hapa akiwa na madhumuni ya kuwatia nguvuni watu hao na kuwapeleka kwa makuhani!"

22 Saulo alizidi kupata nguvu, na kwa jinsi alivyothibitisha wazi kwamba Yesu ndiye Kristo, Wayahudi wa huko Damasko walivurugika kabisa.

Habari za wongofu wake katika Mdo 22[hariri | hariri chanzo]

Miaka 22 baadaye, huko Yerusalemu, Paulo alijitetea hivi:

1 "Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni sasa nikijitetea mbele yenu!"

2 Waliposikia akiongea nao kwa Kiebrania wakazidi kukaa kimya zaidi kuliko hapo awali. Naye Paulo akaendelea kusema,

3 "Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Kilikia. Lakini nililelewa papa hapa mjini Yerusalemu chini ya mkufunzi Gamalieli. Nilifundishwa kufuata kwa uthabiti Sheria ya wazee wetu. Nilijitolea kwa moyo wote kwa Mungu kama ninyi wenyewe mlivyo hivi leo.

4 Niliwatesa hata kuwaua wale watu waliofuata Njia hii. Niliwatia nguvuni wanaume kwa wanawake na kuwafunga gerezani.

5 Kuhani Mkuu na baraza lote la wazee wanaweza kushuhudia jambo hilo. Kutoka kwao nilipokea barua walioandikiwa wale ndugu Wayahudi waliokuwa huko Damasko. Nilikwenda Damasko ili niwatie nguvuni watu hao na kuwaleta wamefungwa mpaka Yerusalemu ili waadhibiwe.

6 "Basi, nilipokuwa njiani karibu kufika Damasko, yapata saa sita mchana, mwangu mkubwa kutoka mbinguni ulitokea ghafla ukaniangazia pande zote.

7 Hapo nilianguka chini, nikasikia sauti ikiniambia: `Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?`

8 Nami nikauliza: `Nani wewe, Bwana?` Naye akaniambia: `Mimi ni Yesu wa Nazareti ambaye wewe unamtesa.`

9 Wale wenzangu waliuona ule mwanga lakini hawakusikia sauti ya yule aliyeongea nami.

10 Basi, mimi nikauliza: `Nifanye nini Bwana?` Naye Bwana akaniambia: `Simama, nenda Damasko na huko utaambiwa yote ambayo umepangiwa kufanya.`

11 Kutokana na ule mwanga mkali sikuweza kuona na hivyo iliwabidi wale wenzangu kuniongoza kwa kunishika mkono mpaka nikafika Damasko.

12 "Huko kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Anania, mtu mcha Mungu, mwenye kuitii Sheria yetu na aliyeheshimika sana mbele ya Wayahudi waliokuwa wanaishi Damasko.

13 Yeye alikuja kuniona, akasimama karibu nami, akasema: `Ndugu Saulo! Ona tena.` Papo hapo nikaona tena, nikamwangalia.

14 Halafu Anania akasema: `Mungu wa babu zetu amekuchagua upate kujua matakwa yake na kumwona yule mtumishi wake mwadilifu na kumsikia yeye mwenyewe akiongea.

15 Kwa maana utamshuhudia kwa watu wote ukiwaambia yale uliyoyaona na kuyasikia.

16 Sasa basi, ya nini kukawia zaidi? Simama ubatizwe na uondolewe dhambi zako kwa kuliungama jina lake.`

17 "Basi, nilirudi Yerusalemu, na nilipokuwa nikisali Hekaluni, niliona maono.

18 Nilimwona Bwana akiniambia: `Haraka! Ondoka Yerusalemu upesi kwa maana watu wa hapa binadamu hawataukubali ushuhuda wako juu yangu.`

19 Nami nikamjibu: `Bwana, wao wanajua wazi kwamba mimi ni yule aliyekuwa anapitapita katika masunagogi na kuwatia nguvuni na kuwapiga wale waliokuwa wanakuamini.

20 Na kwamba wakati shahidi wako Stefano alipouawa, mimi binafsi nilikuwako pale nikakubaliana na kitendo hicho na kuyalinda makoti ya wale waliokuwa wanamuua.`

21 Naye Bwana akaniambia: `Nenda; ninakutuma mbali kwa mataifa mengine."`

Baada ya wongofu[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kufanya utume katika mazingira ya Kiarabu, Tarsus na Antiokia alianza safari za kitume, akienda mbali zaidi na zaidi, akilenga kumhubiri Yesu mahali ambapo bado hajafahamika, hata Hispania.

Ilikuwa kawaida yake kuanzisha makanisa katika miji mikubwa ili toka huko ujumbe ufike hadi vijijini.

Muda wote wa utume wake Paulo alipambana na dhuluma kutoka kwa Wayahudi wenzake na matatizo mengine kutoka Wakristo wenye msimamo tofauti na wa kwake, hasa Wakristo wa Kiyahudi juu ya haja ya kufuata masharti ya Agano la Kale ili kupata wokovu.

Hatimaye alikamatwa na wapinzani wake Wayahudi mjini Yerusalemu, lakini askari wakoloni walizuia asiuawe.

Baada ya hapo alilazimika kukaa gerezani akisubiri hukumu ya Dola la Roma, kwanza Kaisaria Baharini miaka miwili, halafu akakata rufaa kwa Kaisari akapelekwa Roma, alipofika mwaka 61 akakaa miaka miwili tena kifungo cha nje katika nyumba ya kupanga.

Kisha kufunguliwa (labda kwa sababu washtaki wake hawakuwasili) alisafiri tena ingawa hakuna hakika alielekea wapi.

Kifodini chake[hariri | hariri chanzo]

Aliuawa nje ya kuta za Roma kwa kukatwa kichwa wakati wa dhuluma za Nero kati ya mwaka 64 na 67 B.K.

Juu ya kaburi lake lilijengwa kanisa kubwa ambalo liliteketea kwa moto katika karne ya 18 likajengwa upya na hadi leo linapokea hija za Wakristo wengi, hasa katika "Jubilei ya mtume Paulo" iliyotangazwa na Wakatoliki na Waorthodoksi kwa mwaka 2008/2009.

Maandishi yake[hariri | hariri chanzo]

Agano Jipya

Kati ya barua nyingi alizoandika (kwa makanisa ya Thesalonike, Korintho, Galatia, Roma, Filipi, Kolosai, Efeso, kwa viongozi Wakristo kama Timotheo na Tito, tena kwa Filemoni), katika Agano Jipya zinatunzwa 13.

Ukubwa na ubora wa mchango wa Paulo unaeleweka tukizingatia kwamba alifanya kazi na kuandika kabla ya vitabu vya Agano Jipya kupatikana. Ndiye aliyeanza kuliandika akipanua mawazo aliyoyapokea katika Kanisa kwa kuzingatia Agano la Kale na mafunuo na mang’amuzi yake mwenyewe.

Hapo alifafanua vizuri ajabu maisha ya Kikristo kama neema ya kumshiriki Yesu kwa imani, sakramenti na juhudi za kushinda umimi hadi kugeuka sadaka hai, takatifu na ya kumpendeza Mungu.

Wokovu huo, utakaokamilika katika ufufuko wa mwili, unapatikana katika Kanisa, ambalo Paulo alilitambulisha kama bibiarusi wa Kristo na mwili wake.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Aulén, Gustaf. Christus Victor (SPCK 1931)
  • Brown, Raymond E. An Introduction to the New Testament. Anchor Bible Series, 1997. ISBN 0-385-24767-2.
  • Brown, Raymond E. The Church the Apostles left behind(Chapman 1984)
  • Bruce, F.F. 'Is the Paul of Acts the Real Paul?' Bulletin John Rylands Library 58 (1976) 283–305
  • Bruce, F.F., Paul: Apostle of the Heart Set Free (ISBN 0-8028-4778-1)
  • Conzelmann, Hans, the Acts of the Apostles—a Commentary on the Acts of the Apostles (Augsburg Fortress 1987)
  • Davies, W. D. "The Apostolic Age and the Life of Paul" in Matthew Black, ed. Peake's Commentary on the Bible. London: T. Nelson, 1962. ISBN 0-8407-5019-6
  • Davies, W. D. Paul and Rabbinic Judaism: Some Rabbinic Elements in Pauline Theology. S.P.C.K., 3rd ed., 1970. ISBN 0-281-02449-9
  • Dunn, James D.G., 1990, Jesus, Paul and the Law Louisville,KY: Westminster John Knox Press. ISBN 0-664-25095-5
  • Dunn, James D. G., Jesus, Paul, and the Gospels (Grand Rapids (MI), Wm. B. Eerdmans, 2011).
  • Hanson, Anthony T. Studies in Paul's Technique and Theology. Eerdmans, 1974. ISBN 0-8028-3452-3
  • Harris, Stephen L. Understanding the Bible. Palo Alto: Mayfield. 1985. ISBN 978-1-55934-655-9
  • Holzbach, Mathis Christian, Die textpragmat. Bedeutung d. Kündereinsetzungen d. Simon Petrus u.d. Saulus Paulus im lukan. Doppelwerk, in: Jesus als Bote d. Heils. Stuttgart 2008, 166-172.
  • Irenaeus, Against Heresies, i.26.2
  • Maccoby, Hyam. The Mythmaker: Paul and the Invention of Christianity. New York: Harper & Row, 1986. ISBN 0-06-015582-5.
  • Kim, Yung Suk. A Theological Introduction to Paul's Letters. Eugene, Oregon: Cascade Books, 2011. ISBN 978-1-60899-793-0
  • MacDonald, Dennis Ronald, 1983. The Legend and the Apostle: The Battle for Paul in Story and Canon Philadelphia: Westminster Press.
  • Murphy-O'Connor, Jerome, Jesus and Paul: Parallel lives (Collegeville, Minn.: Liturgical Press, 2007) ISBN 0-8146-5173-9
  • Murphy-O'Connor, Jerome, Paul the Letter-Writer: His World, His Options, His Skills (Collegeville, Minn.: Liturgical Press, 1995) ISBN 0-8146-5845-8
  • Murphy-O'Connor, Jerome, Paul: A Critical Life (Oxford: Clarendon Press, 1996) ISBN 0-19-826749-5
  • Ogg, George. “Chronology of the New Testament.” Matthew Black, ed. ‘’Peake's Commentary on the Bible.’’ Nelson, 1962. ISBN 0-8407-5019-6
  • Rashdall, Hastings, The Idea of Atonement in Christian Theology (1919)
  • Ruef, John, Paul's First letter to Corinth (Penguin 1971)
  • Sanders, E.P., Paul and Palestinian Judaism (1977)
  • Segal, Alan F. Paul, the Convert, (New Haven/London, Yale University Press, 1990) ISBN 0-300-04527-1.
  • Segal, Alan F., "Paul, the Convert and Apostle" in Rebecca's Children: Judaism and Christianity in the Roman World (Harvard University Press 1986).
  • Horrell, David G. "An Introduction to the Study of Paul." T&T Clark Approaches to Biblical Studies. 2nd edition. London: T&T Clark, 2006

Marejeo mengine[hariri | hariri chanzo]

  • Bart D Ehrman. Peter, Paul and Mary Magdalene: The Followers of Jesus in History and Legend; 304 pages, Oxford University Press (Machi 2008)
  • Bart D. Ehrman. The New Testament: A Historical Introduction to the Early Christian Writings; 608 pages, Oxford University Press (Julai 2011); ISBN 978-0-19-975753-4
  • Hyam MacCoby. The Mythmaker: Paul and the Invention of Christianity; 238 pages, Barnes & Noble Books (1998); ISBN 978-0-7607-0787-6
  • Hans Joachim Schoeps. Paul: The Theology of the Apostle in the Light of Jewish Religious History (Library of Theological Translations); 34 pages, Lutterworth Press (Julai 2002); ISBN 978-0-227-17013-7
  • Pinchas Lapide, Peter Stuhlmacher. Paul: Rabbi and Apostle; 77 pages, Augsburg Publishing House; (Desemba 1984)
  • Pinchas Lapide, Leonard Swidler, Jurgen Moltmann. Jewish Monotheism and Christian Trinitarian Doctrine; 94 pages, Wipf & Stock Publishers (Mei 2002)

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mtakatifu Paulo kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  1. Martyrologium Romanum